
Refa ambaye Simba wamekuwa na bahati naye katika mashindano ya kimataifa, Jean-Jacques Ndala Ngamo kutoka DR Congon ndiye amepangwa kuchezesha mechi ya ufunguzi wa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 baina ya Morocco na Comoro leo Jumapili, Desemba 21, 2025 katika Uwanja wa Prince Moulaye Abdellah, Rabat, Morocco kuanzia saa 4:00 usiku kwa muda wa Tanzania.
Simba haijawahi kupoteza mchezo wowote wa kimashindano ambao imewahi kuchezeshwa na refa huyo mwenye umri wa miaka 38.
Ndala ndiye alichezesha mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita ambayo Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0.
Msimu wa 2023/2024 Ndala alisimama kati wakati Simba ilipotoka sare ya bao 1-1 ugenini na Al Ahly katika mechi ya marudiano ya mashindano ya African Football League.
Pia alishika filimbi katika mechi ya kwanza ya Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022/2023 ambayo Yanga ilipoteza nyumbani dhidi ya USM Alger kwa mabao 2-1.
Katika mechi ya leo, atasaidiwa na waamuzi wasaidizi, Bongele Guylain na Mwanya Gradel wote kutoka DR Congo huku Messie Nkounkou kutoka Congo akiwa mwamuzi wa akiba.
Refa aliyeteuliwa kusimamia teknolojia ya video ya usaidizi kwa waamuzi ni Dahane Beida na msaidizi wake ni Babacar Sarr wote wakitokea Mauritania.
Dahane ameshawahi kuzichezesha Yanga na Simba kwa nyakati tofauti kwenye mashindano ya Klabu Afrika.