Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya Libya amesema kuwa hali ya usalama huko Tripoli imeboreka kwa kiasi fulani kufuatia mipango mipya ya usalama, hata hivyo ametahadharisha kuwa ukosefu wa usalama unaendelea kushuhudiwa katika mji huo mkuu na katika mikoa ya magharibi mwa Libya.

Hanna Tetteh ameuambia mkutano wa Baraza la Usalama wa Umoja wa Mataifa kwamba mazingira ya usalama katika mji mkuu ni ya utulivu kwa kiasi fulani kutokana na mipango mipya ya usalama.

Amesema, makubaliano ya kudumisha amani yanaendelea kushika kasi lakini hali ya mji mkuu, Tripoli na magharibi mwa Libya bado ni tete ambapo mapigano ya silaha yamekuwa yakiibuka mara kwa mara katika maeneo ya kusini mwa Tripoli na kwingineko huko Libya.

Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa huko Libya amezitolea wito pande zote husika kufanya kazi pamoja ili kutekeleza mipango ya usalama iliyokubaliwa na kuendeleza mageuzi muhimu ili kurejesha utulivu nchini humo.

Kwa upande wa uchumi,  Hanna Tetteh ameeleza kuwa Umoja wa Mataifa bado una wasiwasi mkubwa kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake, wahamiaji, watoto wadogo na vifo vinavyotokea vizuizini. 

Kabla ya kusherehekea Siku ya Uhuru wa Libya inayoadhimishwa kila mwaka Desemba 24, Bi Tetteh amewataka viongozi wa Libya kutegea sikio matakwa ya wananchi wa Libya na kuweka kando tofauti zao kwa maslahi ya umoja na mshikamano wa taifa la Libya.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *