
Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema mabadiliko ya jina la Chemba ya Taifa ya Biashara Tanzania (TNCC), ni hatua ya kimkakati inayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kukuza uchumi wa Taifa na kufikia Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050.
Akizungumza leo Jumapili Desemba 21, 2025 jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa mabadiliko ya jina la Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) na kuzindua nembo mpya ya TNCC, Mpogolo amesema hatua hiyo inaakisi mageuzi ya kimfumo na kiuendeshaji yatakayoiwezesha TNCC kuwa taasisi imara, shindani na yenye sauti ya kuaminika kwa wafanyabiashara ndani na nje ya nchi.
Mkuu huyo wa wilaya amesisitiza kuwa sekta binafsi ni mhimili muhimu wa maendeleo ya kiuchumi na Serikali kwa kulitambua hilo, itaendelea kuboresha mazingira ya biashara nchini.
Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Rais wa TNCC, Vicent Minja amesema mabadiliko hayo yanafungua zama mpya za kuimarisha uwakilishi wa wafanyabiashara, kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana, pamoja na kukuza mchango wa sekta binafsi katika uchumi wa Taifa.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa TNCC, Oscar Kissanga amesema mabadiliko ya jina na nembo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuboresha utoaji wa huduma kwa wanachama na kuimarisha ushindani wa wafanyabiashara wa Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Wakizungumzia hatua hiyo ya uzinduzi wa nembo hiyo, wadau wa sekta ya biashara nchini, akiwamo Happy Simbeye amesema hatua hiyo inaweza kufungua ukurasa mpya wa mwelekeo na uongozi wa chemba hiyo.