
Mbeya. Mbunge wa Mbeya vijijini ,Patali Shida amewaomba wazee wa mila (machifu),kutumika kama daraja la kuisaidia Serikali kuhamasisha kundi la vijana kuchagamkia fursa ya kupata ujuzi kupitia mafunzo ya uanagenzi ili waweze kujiajiri.
Patali amesema Leo Jumapili Desemba 21,2025,akiwa mgeni rasmi katika mkutano machifu zaidi 500 uliofanyia katika Shule ya Sekondari Mbalizi na kuhudhuriwa na watendaji wa Serikali akiwepo Mkurugenzi wa Halmashauri Erica Yegella.
“Tuwaombe machifu katika maeneo yenu toeni elimu kwa jamii kujua umuhimu wa kupata ujuzi kupitia mafunzo ya uanagenzi yanayo tolewa katika vyuo mbalimbali vya Ufundi Stadi (Veta),ili waondokane na utegemezi, “amesema.
Patali amesema mpango huo mahususi umeletwa na Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa lengo la kuwajengea ujuzi vijana hususani walio hitimu elimu ya msingi kuweza kujiajiri na kuondokana na utegemezi.
Katika hatua nyingine amewaomba kuwa sehemu ya kuombea amani na kukemea uovu kwa baadhi ya watu wasio waadilifu katika jamii.
Amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa machifu na kwamba itaendelea kuwa bega kwa bega hususani kutatua changamoto zao na kuboresha miradi ya maendeleo.
“Mbeya vijijini tuna mipango mikakati yetu ya kuhakikisha tuna boresha miradi ya maendeleo kwa kuweka kipaumbele ikiwepo kuboresha na kujenzi miundombinu ya barabara korofi, “amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya,Erica Yegella ameungana na Mbunge huyo kuhamasisha vijana kuchangamkia fursa ya mafunzo ya uanagenzi ili kuweza kujiajiri .
“Machifu Serikali inatambua mchango wenu mkubwa tunaomba mtufikishe ujumbe kwa wananchi katika maeneo yenu wajitokeze kuchangamkia fursa ya kupata ujuzi bure, “amesema.
Katika hatua nyingine, Yegella amehamasisha jamii kujiunga na mfuko wa bima ya afya kwa wote baada ya Serikali kufanya maboresho ya viwango vya juu.
“Serikali imefanya maboresho ambapo kwa kila Kaya watakata kadi za bima ya afya kwa gharama ya Sh 150,000 ambazo zitanufaisha watu sita kupata huduma katika Vituo vya Afya,Zahanati, Hosptali za Rufaa,”amesema.
Kiongozi wa Wazee wa Mila ,Chifu Soja Masoko wameomba Serikali kutanya kila jitihada kuwakutanisha na Rais Samia Suluhu Hassan .
“Tunaomba nasi tupate fursa ya kuongea na Rais kwani tuna jambo letu hususani kujadiliana masuala mbalimbali ikiwepo yaliyo jitokeza Oktoba 29,2025,amesema.
Wakati huo huo ametoa tamko la kurahani matukio ya uvunjifu wa amani yaliyo tokea Oktoba 29,2025, sambamba na kuwataka vijana kuwa wazalendo kwa kulinda na kutetea rasilimali za Taifa la Tanzania.
Masoko pia ameomba kundi hilo likumbukwe katika upatikanaji wa mikopo asilimia 10 kwa lengo la kubuni miradi ya kujikwamua kiuchumi.