
Dodoma. Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limekana taarifa zinazosambazwa kupitia mitandao ya kijamii zikidai Katibu wa Chadema Kanda ya Kati Ashura Masoud amekamatwa na vyombo vya dola, likibainisha kuwa madai hayo si ya kweli.
Kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa leo Desemba 21,2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Gallus Hyera ineeleza kuwa hakukamatwa bali aliitwa kufika kituo cha Polisi kwa ajili ya mahojiano ya kawaida, kwa mujibu wa taratibu za kisheria.
“Taarifa zinazoeleza kuwa Jeshi la Polisi limemkamata Katibu wa Chadema Kanda ya Kati si za kweli. Ukweli ni kwamba aliitwa kufika kituoni kwa mahojiano, jambo ambalo ni la kawaida na linaruhusiwa kisheria,” taarifa ya kamanda huyo imeeleza.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa kuwepo na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi wakidai kuwa Jeshi la Polisi lilipaswa kutoa wito rasmi badala ya kumkamata mtu.
Hata hivyo, taarifa hiyo imesisitiza kuwa kwa mujibu wa sheria za nchi, Polisi wana mamlaka ya kumwita au kumkamata mtu yeyote anayehusishwa na kosa la jinai au ambaye mwenendo wake unaashiria uwezekano wa kutenda uhalifu.
“Jeshi la Polisi linafanya kazi zake kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo. Hatua zozote zinazochukuliwa hulenga kulinda usalama wa raia na mali zao,” sehemu ya taarifa hiyo imeeleza.
Aidha, Jeshi la Polisi limetoa onyo kwa watu wanaoeneza taarifa za uongo kupitia mitandao ya kijamii, likieleza kuwa kitendo hicho ni kosa la jinai na kinaweza kuchukuliwa hatua za kisheria dhidi ya wahusika.
“Taarifa za uongo hazijengi jamii wala kusaidia amani ya nchi. Tunatoa wito kwa wananchi kupata taarifa sahihi kutoka vyanzo rasmi na kuacha kusambaza upotoshaji,” imesisizwa kwenye taarifa hiyo
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limewahakikishia wananchi kuwa litaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi, haki na kwa kuzingatia misingi ya utawala wa sheria.