
Arusha. Ili kuboresha huduma kwa watalii, Kituo cha Utalii na Diplomasia kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji nchini, wanatarajia kuwa na Kituo cha Huduma Jumuishi (One Stop Center) ili waweze kuhudumia watalii kwa haraka.
Kituo hicho kitakachofanya kazi kwa muda wa saa 24, kinatajwa kusaidia kuharakisha utoaji huduma kwa watalii ikiwemo wanaopoteza hati zao za kusafiria ambapo kupitia kituo hicho wataweza kufanya mchakato na kupata hati ya kusafiria ya dharura.
Hayo yamesemwa leo Jumapili Desemba 21, 2025 na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Utalii na Diplomasia Arusha, Mrakibu wa Polisi, Waziri Tenga, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kituo mkakati wa kuwapo kituo hicho.
Amesema kuwa wanatarajia hivi karibuni kuwa na kituo hicho kwa ajili ya kutoa huduma kwa watalii ili wanapokuwa na changamoto ziweze kutatuliwa kwa haraka.
Amesema kuwa kutokana Idara ya Uhamiaji kutoa nyaraka za kusafiri na wao kutoa nyaraka za ‘loss report’ pale mgeni anapopoteza hati ya kusafiria, hivyo kupitia kituo hicho watalii wataweza kuhudumiwa kwa saa 24.
“Kituo kitafanya kazi kwa saa 24 maana wageni wanaingia muda wote bila kujali wikiendi au sikukuu, sasa ikitokea mgeni amepoteza mfano hati ya kusafiria, ili asipoteze muda mwingi kuja hapa, kupitia kituo hicho ataweza kuhudumiwa kwa haraka.
Tenga amesema kuwa usalama wa wageni nchini umeendelea kuimarika ikiwemo kuhakikisha wanadhibiti vitendo vya kihalifu ambapo pia kupitia doria za mtandaoni na vituo maalumu kwa magari ya utalii vilivyopo maeneo mbalimbali nchini, vimesaidia kutatua changamoto wanazokutana nazo watalii.
“Miezi kama mitatu au minne tulikuwa na mwigizaji maarufu kutoka nchini India ambaye alikuja eneo la Chemka mkoani Kilimanjaro na tulivyozungumza naye kwa nini amechagua eneo hilo alisema ni kwa sababu ya usalama pamoja na ukarimu wa Watanzania,”amesema
Kuhusu doria mtandaoni, amesema wana timu ya wataalamu ambao wanafuatilia mienendo ambayo inaweza kuwapa viashiria nani anataka kufanya nini na maeneo gani na wakachukua hatua, hivyo teknolojia imekuwa na inasaidia katika kuimarisha usalama.
Akizungumzia nyumba za kupangisha wageni maarufu kama Airbnb, amesema zimesajiliwa na wamekuwa na vikao na wamiliki lengo likiwa ni kuangalia namna gani usalama unaboreshwa ili na wao waongeze doria katika maeneo mahsusi.
Tenga amesema hadi sasa wameshasajili zaidi ya nyumba 178 katika kipindi hiki cha wageni wengi wanatembelea na kukagua ili kujiridhisha hali ya usalama bado ipo, kwani nyumba hizo hupangishwa kwa wageni wa ndani na nje ya nchi.
Mmoja wa wadau wa utalii jijini Arusha, Francis Jonathan amesema tangu kuanzishwa kwa Kituo hicho, kimewezesha kusaidia kuboresha usalama na kusimamia usalama wa watalii kwa haraka.
“Tangu kuanzishwa kwa Kituo Utalii na Diplomasia kimesaidia katika utoaji wa huduma kwa watalii wetu hapa nchini ambapo wakiwa na changamoto ya aina yoyote wanahudumiwa kwa haraka, tofauti na ilivyokuwa awali ambapo walikuwa wakihudumiwa katika vituo vya polisi vya kawaida,”amesema.
Amesema anaamini kitakapoanzishwa Kituo cha Huduma Jumuishi (One Stop Center), hali itakuwa bora zaidi kwani mtalii atapata huduma zote mahali pamoja.