Dhoruba za majira ya baridi kali zimesababisha vifo vya Wapalestina wasiopungua 17 katika Ukanda wa Gaza mwezi huu wa Duisemba pekee.
Haya ni kwa mujibu wa ripoti za mamlaka husika za serikali za mitaa, huku Israel ikiendelea kuweka vizuizi vikali vya kpelekwa vifaa vya makazi na misaada mingine ya kibinadamu katika eneo hilo lililoathiriwa na vita.
Kitengo cha Ulinzi wa Raia katika Ukanda wa Gaza kimeripoti kuwa Wapalestina wasiopungua 17 wameaga dunia mwezi huu wa Disemba huku mvua kubwa, upepo na baridi kali ikiangusha mahema ya Wapalestina waliolazimika kuwa wakimbizi kutokana na mauaji ya kimbari ya Israel.
Duru za tiba zimearifu kuwa, watu walioaga dunia ni pamoja na watoto wanne waliopoteza maisha kwa baridi kali.

Mahmoud Bassal, msemaji wa Kitengo cha Ulinzi wa Raia katika Ukanda wa Gaza amesema kuwa hali ya joto hupungua sana nyakati za usiku na kutahadharisha kuwa “baridi kali inatishia maisha ya watoto wachanga kwa kukosa mahali pa kulala penye joto.”
Majengo 17 ya makazi yameporomoka kikamilifu mwezi huu wa Disemba huku mvua kubwa inayoambatana na upepo mkali ukiendelea kuutatiza maisha ya watu wa Ukanda wa Gaza.
Makazi ya dharura 44 yaliyoanishwa wiki hii yamekumbwa na mafuriko kufuatia kuziba njia za mifereji ya kupitishia maji.