Serikali imelitangaza eneo ulipokuwa mgodi maarufu wa dhahabu wa Buzwagi kuwa sehemu ya kujengwa eneo maalumu la kongani ya viwanda β€œBuzwagi Special Economic Zone” baada ya kuhitimishwa kwa shughuli za uchimbaji katika eneo hilo.

Hatua hiyo imewekwa wazi na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na maeneo maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Gilead Teri na kuongeza kuwa tayari serikali kwa kushirikiana na wawekezaji imeanzisha Buzwagi Special Economic Zone ambayo ina mpango wa kuwa kitovu cha uzalishaji, usindikaji na usambazaji wa bidhaa za mgodi kwa soko la Tanzania, Afrika Mashariki na Afrika ya Kati.

Kwa upande wake Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ameongeza kuwa zaidi ya viwanda 30 vitajengwa katika sekta mbalimbali ikiwamo nishati, elimu, uzalishaji bidhaa za migodini, bidhaa za kuchakata madini na bidhaa zingine zinazotumika kwenye sekta ya madini ikiwemo vipuli vya viwandani.

“Zaidi ya wawekezaji 30 wameonesha nia ya kuanzisha viwanda katika eneo la Buzwagi na tayari mwekezaji mmoja aitwaye East Africa Conveyors Supplies ameanza kuzalisha bidhaa zinazotumika migodini.” Amesema Mavunde

Mbali ya mwekezaji huyo, Mavunde ameongeza kuwa kampuni ya Tembo Nickel inatarajiwa kuwekeza katika ujenzi wa tajenga kiwanda cha kuongeza thamani madini ya metali (Multi-Metal Refinery Facility) kitakachotumia teknolojia ya kisasa ya Hydromet kuyeyusha kwa joto kali.

Mgodi wa Buzwagi ulikuwa ukimilikiwa na kampuni ya Acacia Mining sambamba na migodi ya Bulyanhulu na Mara ambayo kwa pamoja mwaka 2014 ilizalisha aunsi 719,000 za dhahabu.

Imeandaliwa na @moseskwindi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *