Morocco ina kibarua kigumu kwenye michuano ya mwaka huu kutokana na matumaini makubwa ya mashabiki wake ndani na nje. Wanafungua dimba dhidi ya Comoros.

Kwenye mkesha wa mashindano ya AFCON 2025, kulikuwa na habari ambazo zilitolewa na Shirikisho la Kandanda Afrika – CAF.

Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika – AFCON itakuwa inafanyika kila baada ya miaka minne baada ya michuano ya 2028. Haya ni mabadiliko makubwa kwa tamasha hilo linaloandaliwa kila baada ya miaka miwili.

Rais wa CAF Patrice Motsepe alitangaza mabadiliko hayo kama sehemu ya marekebisho muhimu ya mchezo huo wa kimataifa barani humo ili kuusaidia kuendana vyema na kalenda ya kimataifa iliyofurika mashindano.

Rais wa CAF Patrice Motsepe
Michuano ya AFCON itakuwa inafanyika kila baada ya miaka minne baada ya michuano ya 2028Picha: Wu Tianyu/Xinhua/IMAGO

Chanzo kipya cha mapato

Kombe la AFCON kila baada ya miaka miwili lilikuwa chanzo muhimu cha mapato kwa mashirikisho ya kitaifa ya Afrika, lakini Motsepe amesema kuanzishwa kwa mashindano mapya ya kila mwaka ya Ligi ya Mataifa ya Afrika — sawa na yale ya Ligi ya Mataifa ya UEFA – sasa yatasaidia kuingiza kipato badala yake.

“Lengo letu sasa ni katika AFCON hii lakini mwaka 2027 tutaenda Tanzania, Kenya na Uganda, na AFCON baada ya hapo itakuwa mwaka 2028,” Motsepe aliwaambia waandishi wa habari mjini Rabat siku ya Jumamosi, usiku wa kuamkia mchezo wa ufunguzi wa Kombe la Mataifa linaloandaliwa na Morocco mwaka huu.

Alisema mchakato wa zabuni utafunguliwa kwa mataifa yenye nia ya kuandaa Kombe la Mataifa la 2028.

Kombe la Mataifa ya Afrika - AFCON 2025
Uwanja wa Al Madina mjini Rabat ni moja ya vitakavyotumika kwa mechi za AFCON 2025 nchini MoroccoPicha: Abdel Majid Bziquat/AFP/Getty Images

“Kisha baada ya Kombe la Dunia la Vilabu la FIFA mwaka 2029 tutakuwa na mashindano ya kwanza ya Ligi ya Mataifa ya Afrika… yenye fedha zaidi kwa washindi, rasilimali zaidi, na ushindani zaidi.”

Kombe la Mataifa ya Afrika kwa kawaida limekuwa likifanyika kila baada ya miaka miwili tangu mashindano ya kwanza kabisa mwaka 1957, lakini katika kipindi cha miaka 15 iliyopita limepata changamoto kupata nafasi inayofaa katika kalenda ya kimataifa.

Mashindano ya mwaka huu nchini Morocco yatakuwa ya nane kufanyika kuanzia mwaka wa 2012 nchini Guinea ya Ikweta na Gabon.

Suluhisho la mrundikano wa mechi za kimataifa

Mashindano ya 2019 nchini Misri yalifanyika Juni na Julai, tofauti ilivyozoeleka mwanzoni mwa mwaka ambayo ilionekana kama njia ya kufurahisha vilabu vikubwa vya Ulaya kwa kuepuka kucheza katikati ya msimu wao.

Washindi wa AFCON 2024 Ivory Coast
Mshindi wa AFCON 2025 atapata zawadi ya dola milioni 10 kutoka dola milioni 7 walizopata Ivory Coast 2024Picha: FRANCK FIFE/AFP

Lakini AFCON mbili za mwisho, nchini Cameroon mwaka wa 2022 na Ivory Coast mwaka wa 2024, zilirejea Januari-Februari ili kuepuka kuingiliana na msimu wa mvua katika maeneo hayo.

Motsepe anasema mashindano mapya ya Ligi ya Mataifa yataanza kwa kuzingatia mfumo wa kikanda, ambapo timu 16 kutoka kila kanda; mashariki, magharibi na kati kusini, na sita kutoka kanda ya kaskazini.

Mechi zitachezwa Septemba na Oktoba, huku timu za kwanza kutoka kila kanda zikikutana kwenye fainali zitakazochezwa katika eneo moja mwezi Novemba.

Wakati huo huo, fedha za mshindi wa AFCON nchini Morocco zitaongezwa hadi dola milioni 10, ikiwa ni kutoka dola milioni saba ambazo washindi wa Ivory Coast walitia kibindoni mwaka wa 2024.     

AFP, DPA, AP, Reuters

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *