Watu waliokuwa na silaha, usiku wa kuamkia leo, wamefyatua risasi kiholela katika kitongoji kimoja karibu na Johannesburg nchini Afrika Kusini na kuua takriban watu 9 na kujeruhi wengine kadhaa.

Taarifa ya polisi imeeleza kuwa baadhi ya wahanga wa tukio hilo walifyatuliwa risasi kiholela mitaani. Awali polisi ilitangaza kuwa watu kumi wameuawa lakini baadaye ilisahihisha taarifa yake hiyo.

Ufyatuaji risasi huo umetokea karibu na eneo la watu maskini karibu na baadhi ya migodi mikubwa ya dhahabu nchini Afrika Kusini. Ni takriban kilomita 40 (maili 25) kusini magharibi mwa Johannesburg.

Polisi tayari imeanzisha msako kuwatafuta wahusika na mauaji hayo. Afrika Kusini ina idadi kubwa ya silaha haramu licha ya sheria kali za umiliki. 

Mnamo Desemba 6, takriban watu 12, akiwemo mtoto wa miaka mitatu waliuawa wakati washambuliaji walipofyatua risasi katika hosteli kwenye kitongoji cha Saulsville, magharibi mwa Pretoria. Watu 14 walijeruhiwa katika uhalifu huo.

Katika tukio lingine lililojiri Septemba mwaka jana, watu 18 waliuawa kwa kupigwa risasi katika jimbo la Eastern Cape. 

Data za polisi zinaonyesha kuwa wastani wa watu 63 waliuawa kila siku kati ya Aprili na Septemba huko Afrika Kusini. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *