Afrika kuendelea kushirikiana na UrusiAfrika kuendelea kushirikiana na Urusi

SERIKALI ya Tanzania imetaja vipaumbele vya kuzingatiwa katika ushirikiano kati ya Afrika na Urusi. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, ametaja vipaumbele hivyo alipoongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Pili wa Jukwaa la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Urusi uliofanyika Desemba 19 na 20, jijini Cairo, Misri. Balozi Kombo alisema ni muhimu kuendeleza ushirikiano wa muda mrefu kati ya Urusi na mataifa ya Afrika.

Amesema ushirikiano huo unapaswa kuweka kipaumbele katika kuongeza ushirikiano wa kiuchumi, hususani kwenye sekta za kimkakati za miundombinu na usafirishaji, nishati na nishati mbadala, teknolojia, Tehama na afya. SOMA: Tanzania, Urusi kushirikiana utalii

Amesema kuimarisha usalama wa chakula barani Afrika kunahitaji uwekezaji zaidi wa Urusi katika kilimo, ikiwemo kilimo endelevu, viwanda vya usindikaji wa kilimo na uzalishaji wa mbolea. Mkutano huo ulihudhuriwa na mawaziri wa mambo ya nje wa Afrika, jumuiya za kikanda za bara hilo pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi. Mkutano huo ulifanyika chini ya wenyeviti wawili; Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Dk Badr Abdelatty na Waziri wa Mambo ya Nje wa Shirikisho la Urusi, Sergey Lavrov.

Katika mkutano huo, nchi za Afrika na Urusi zilijadiliana na kukubaliana masuala muhimu yanayogusa maslahi ya pamoja katika nchi zao na ndani ya Umoja wa Mataifa (UN) na mashirika yake. Mawaziri hao walisisitiza umuhimu wa UN na mashirika yaliyo chini yake kufanyiwa marekebisho ili kuongeza uwakilishi wa Afrika, kuimarisha uwajibikaji na ufanisi, kuwa na mfumo wa biashara wa dunia unaozingatia usawa na kutoa nafasi sawa kwa kila nchi kushiriki kikamilifu katika uamuzi unaoigusa dunia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *