Askofu Bagonza aanika ‘sumu’ za maridhianoAskofu Bagonza aanika ‘sumu’ za maridhiano

ASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza ametaja sumu tano zinazoua maridhiano. Amesema hayo wakati wa ibada ya ubarikio wa wachungaji na wadiakonia katika dayosisi hiyo mkoani Kagera.

Ametaja sumu ya kwanza kuwa ni hila na akawaasa watu kujiepusha nayo katika maridhiano. “Wakati mwingine, hila inapewa jina la nia njema au maslahi mapana ya taifa… Tujiepushe na hila kutafuta maridhiano,” alisema Askofu Bagonza.

Pia, amesema watu wanapaswa kujiepusha na kutafuta ushindi katika maridhiano kwa kuwa kuweka mazingira ya kuwa na mshindi kwenye maridhiano huandaa vurugu ya baadaye. “Tatu, kukwepa ukweli, maridhiano yanapatikana endapo ukweli umeonekana hata kama ukweli huo unaumiza pande zote, duniani kote maridhiano hujengwa katika ukweli pasipo kulaumiana,” alifafanua.

Amewashauri wenye madaraka kuyaweka pembeni kwanza na kuingia katika maridhiano na kwamba wahusika wote katika maridhiano huwa kama majeruhi wanaotafuta uponyaji. SOMA: Wasira aahidi kuendeleza maridhiano

Ametaja sumu nyingine kuwa ni kujinufaisha na maridhiano ambapo alisema wanaoongoza maridhiano wasitawaliwe na tamaa ya kutaka kunufaika na wanachojadili au kupendekeza. “Unakuta mtu anapiga kelele za maridhiano lakini anachotafuta ni nafasi baada ya maridhiano, sasa watu wa namna hiyo muwasome na msiwahusishe kwenye maridhiano kwa sababu tayari wana mgongano wa maslahi,” alisisitiza.

Amesema  anaelewa kuwa serikali ina mambo mengi ya kushugulikia lakini maridhiano ya kweli ni jambo la muhimu zaidi Askofu Bagonza alisema mijadala ambayo imekuwepo kuhusu kipi bora kati ya amani na haki kwa sasa si muhimu, hivyo badala yake watu wanapaswa kutambua kila mmoja ni mshindi.

Amesema nje ya maridhiano hakuna uhakika wa nchi kufika inakokwenda kwa sababu taifa lenye manung’uniko ni ngumu kuliongoza hivyo, nchi inahitaji maridhiano kwa gharama yoyote. “Zipo gharama za kisiasa kiuchumi, kijamii na kisera tutatakiwa kuzikubali ili kuipata tena Tanzania tulioizoea, inabidi tupitie gharama chungu kuweza kuipata tena Tanzania tuliyoipoteza iliyotuponyoka katika mikono yetu. Kuna miiko tumeikiuka na dawa yake ni toba, taifa letu ndilo madhabahu yetu tuiheshimu na kuitunza,” alisema Askofu Bagonza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *