Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa uwezo wa kiulinzi wa nchi hii kimsingi umeratibiwa kwa lengo la kuzuia mashambulizi yoyote ya wavamizi na si suala la kujadiliwa.

Esmail Baqaei amesema haya katika mkutano wa kila wiki na waandishi wa habari hapa Tehran wakati akijibu swali aliloulizwa kuhusu taarifa ya vyombo vya habari vya Israel na Marekani kuhusiana na uwezekano wa mashambulizi mpya wa kijeshi dhidi ya Iran kwa kisingizio cha miradi yake ya makombora.

Baqaei amesema kuwa Iran imeimarisha miradi yake ya makombora kwa shabaha ya kuhami mamlaka yake ya kujitawala.

Amekosoa unafiki na sera za kindumakuwili za Marekani na utawala wa Kizayuni mkabala wa miradi ya makombora ya Iran ili kuidhihirisha miradi hiyo kama tishio na kusema: Tel Aviv na Washington zinatoa kauli hizi katika hali ambayo silaha hatari na za maangamizi ya halaiki zinaingizwa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel ili kutumika katika mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.  

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa vikosi vya ulinzi vya Iran vimejizatiti kwa silaha ipasavyo ili kuilinda nchi inapobidi.

“Bila kujali kampeni hizi mbovu za vyombo vya habari, wananchi wa Iran, vikosi vya ulinzi na taasisi zote za serikali zitaendeleza njia yao kwa kujikita katika majukumu yao,” amesema Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje.

Juni 13 mwaka huu, Israel ilianzisha vita dhidi ya Iran na kuwaua shahidi makamanda kadhaa wa ngazi ya juu wa jeshi, wanasayansi wa nyuklia na raia wa kawaida. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *