
Wakati kundi la waasi la M23 likipanua udhibiti wake wa kimaneo katika mkoa wa Kivu Kusini na kutawala vyombo vya habari, tishio lingine linaendelea kuwakabili wakazi wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo: lile la Vikosi vya ADF, vinavyohusishwa na kundi la kigaidi la Islamic State (ISIS).
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Mnamo mwezi Novemba, kabla ya kuanguka kwa Uvira, kundi hili lilihusishwa na vifo vingi zaidi nchini, huku raia wasiopungua 123 wakiuawa, ikilinganishwa na 75 mwezi uliopita, kulingana na shirika la utafiti linalofuatilia na kuripoti visa vya ghasia, uhalifu, na uvunjaji wa haki za binadamu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Kivu Security Tracker (KST).
Kitovu cha vurugu hizi kiko katika eneo la Lubero, haswa katika eneo la uchifu la Baswagha na sekta ya Bapere, ambapo ADF imejikita katika mashambulizi yake, utekaji nyara, na mauaji mwezi Novemba. Uvamizi wao mbaya zaidi ulitokea Novemba 14: raia 29 waliuawa huko Byambwe, wengi wao wakiuawa kwa mapanga katika kituo cha afya ambacho baadaye kilichomwa moto.
Wiki iliyofuata, mashambulizi kumi na tano yalilenga eneo la uchifu la Baswagha pekee. Kati ya haya, ni mawili tu yaliyozuiwa, licha ya uwepo wa muungano wa FARDC-UPDF (jeshi la Uganda) katika sehemu ya operesheni Shujaa. Kuibuka tena kwa vurugu kunasababisha watu wengi kuhama kuelekea Butembo, Kirumba, na Musienene. Kundi hilo linaonyesha uthabiti wa kiutendaji unaotia wasiwasi, licha ya juhudi za muungano huu, ambao “umeongeza mashambulizi yake dhidi ya kundi linalohusishwa na ISIS,” kulingana na ripoti, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya anga yaliyoanzishwa kutoka eneo la Uganda.
Katika eneo la Mambasa, idadi ya matukio imepungua, lakini mbali na mauaji, ADF inaimarisha udhibiti wake kupitia ushuru wa kulazimishwa na sherehe za kuhubiri Uislamu. Ripoti hiyo pia inaashiria kuwepo kwa vituo vipya vya mafunzo.
Hata hivyo, ripoti ya shirika la KST ya Novemba iinaonyesha kudhoofika kwa CRP, kundi la kisiasa na kijeshi lililoanzishwa na Thomas Lubanga mwaka huu. “Mashambulizi yaliyofanywa na FARDC wakati wa mwezi wa Oktoba yalidhoofisha wanamgambo hawa,” ripoti hiyo inasema.