Mkuu wa BKA  Holger Münch, aliyezungumza na gazeti la The Bild la kila Jumapili nchini Ujerumani,  amesema matukio ya kuonekana kwa droni yanaleta kitisho kikubwa cha usalama.

Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz, alisema mwezi Oktoba kwamba serikali ya Ujerumani inaamini Urusi, inahusika na matukio mengi ya kuonekana kwa droni katika anga ya Ujerumani.

Münch aliliambia gazeti la Bild kwamba kile kinachotokea hakiwezi kuwekewa uhakika wa moja kwa moja kuwa kinafanywa na serikali ya Urusi, lakini akaongeza kuwa anaamini anaerusha droni kuelekea anga ya Ujerumani ana nia ya kuleta hali ya sintogahamu nchini humo.

Droni zimeonekana uwanja wa ndege wa Berlin na Munich

Matukio hayo ya droni kuonekana angani nchini Ujerumani, yamevuruga shughuli katika viwanja vya ndege, ikiwemo kufutwa kwa safari za ndege na usumbufu kwa wasafiri.

Kwa mfano, Uwanja wa Ndege wa Munich ulisitisha shughuli zake Oktoba 3, wakati mji huo ulipokuwa unaendesha tamasha maarufu la bia la Oktoberfest.

Ujerumani | Droni zatoa kitisho cha usalama Ujerumani
Safari nyingi za ndege zilifutwa katika viwanja vya Ujerumani kufuatia kuonekana droni katika anga ya taifa hilo. Picha: Nicolas Economou/NurPhoto/picture alliance

Mwezi Novemba, Uwanja wa Ndege wa Berlin Brandenburg nao pia ulilazimika kusitisha shughuli zake kwa takriban saa mbili kutokana na kuonekana kwa droni ambazo hazijulikani zilikotoka.

Ujerumani yatafuta njia bora ya kukabiliana na droni hizo

Ujerumani sasa inatafuta njia bora ya kupambana na droni hizo kwa ufanisi. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Alexander Dobrindt, alifungua kituo cha pamoja cha kukabiliana na droni (GDAZ) mjini Berlin, ambacho kitakuwa na jukumu la kuratibu uwezo wa serikali ya shirikisho na majimbo katika ulinzi dhidi ya droni.

“Taasisi ya pamoja ya kukabiliana na droni inafanya kazi saa 24 na imekusudiwa kujibu haraka vitisho vya usalama,” ilisema taarifa ya serikali ya Ujerumani.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa taasisi itaunda mfumo imara wa mawasiliano endelevu, tathmini za hali kwa pamoja na hatua za uratibu katika ulinzi dhidi ya droni.”

Dobrindt ametaka kuwepo pia na kitengo cha ulinzi wa droni kusaidia viwanja vya ndege na maeneo mengine pale matukio ya droni yanapotokea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *