Manchester, England. Erling Haaland anaendelea kuonyesha kwa nini ni mmoja wa washambuliaji bora zaidi duniani, baada ya juzi kumpita Cristiano Ronaldo na kufikia idadi sawa ya mabao na Didier Drogba katika Ligi Kuu ya England.

Bao lake ndani ya dakika tano za mwanzo katika mechi ya Manchester City dhidi ya West Ham United kwenye Uwanja wa Etihad lilikuwa bao la 18 msimu huu na la 103 kwake kwa jumla katika Ligi Kuu England.

Hilo lilimweka Haaland sambamba na jumla ya mabao ya Ronaldo aliyoyafunga akiwa Manchester United, ingawa Haaland alifikia idadi hiyo katika mechi 113 pekee za Ligi Kuu, mechi 119 chache kuliko Ronaldo aliyoecheza mechi 232 na kufunga bao lake la mwisho katika ligi hiyo dhidi ya Everton tarehe 9 Oktoba 2022.

Kisha katika kipindi cha pili, Haaland alifikisha jumla ya mabao 104, sawa na Didier Drogba, ambaye alifunga mabao yote 104 akiwa Chelsea katika chati ya wafungaji bora wa muda wote wa Ligi Kuu. 

Mechi hiyo pia ilikuwa ya 10 msimu huu ambayo Haaland amefunga bao la kwanza.

Umuhimu wa Haaland kufunga bao la kwanza kwa Man City ni kwamba hawajapoteza mechi yoyote katika michezo yao 11 ya mwisho ya Ligi Kuu wanapofunga kwanza, tangu walipopoteza 2-1 dhidi ya Brighton & Hove Albion tarehe 31 Agosti 2025.

Kwingine, Viktor Gyokeres alimaliza ukame wa mabao aliokuwa nao baada ya kuifungia Arsenal bao pekee la ushindi kwa mkwaju wa penalti ugenini dhidi ya Everton juzi.

Tangu mwanzo wa msimu wake wa kwanza akiwa Sporting CP (2023–24), Viktor Gyökeres amefunga penalti zote 19 alizopiga katika mashindano ya ligi (17/17 katika Ligi Kuu Ureno na 2/2 katika Ligi Kuu England).

Katika mashindano yote, Arsenal wamefunga bao la kwanza katika mechi 19 msimu huu, na kushinda mechi zote 19.

Arsenal wameshinda mechi ya Ligi Kuu kwa bao 1-0 kupitia penalti kwa mara ya kwanza tangu Agosti 2023 dhidi ya Crystal Palace, ambapo nahodha Martin Ødegaard ndiye aliyefunga siku hiyo.

Msimu wa 2025–26 ni msimu wa tano Arsenal kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu England siku ya Krismasi (pia 2002/03, 2007/08, 2022/23 na 2023/24).

Hata hivyo, ‘Washika Mitutu wa London’ wameshindwa kutwaa ubingwa katika misimu yote minne iliyotangulia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *