Iran imezindua kifaa kipya cha kusaidia upasuaji wa saratani ya matiti kinachoitwa Cancer Diagnostic Probe (CDP), ambacho kinapunguza muda wa kugundua mipaka ya tishu zilizoathirika kutoka dakika 45 hadi sekunde 15 pekee.

Kifaa hiki, kilichotengenezwa na kampuni ya Aria Health Nanosensors, kinatumia sindano yenye kipimo cha patholojia na kutoa matokeo kwa haraka kwenye skrini, yakionekana kama hasi, yenye shaka au chanya kulingana na viwango vya Shirika la Afya Duniani (WHO).

Meneja wa mauzo wa kampuni hiyo, Mohammad Hossein Yazdi, alisema kifaa hiki ni cha kwanza duniani chenye uwezo wa kubaini kwa usahihi mipaka ya saratani wakati wa upasuaji. Majaribio ya kitabibu yameonesha kuwa CDP hugundua takribani asilimia 30 ya mipaka ya saratani ambayo mbinu za kawaida za “frozen section” na patholojia ya kudumu hukosa. Katika upasuaji wa saratani ya matiti, kifaa kimeonesha usahihi wa zaidi ya asilimia 90, na baadhi ya majaribio yakifikia zaidi ya asilimia 93.

Kwa kawaida, mbinu ya “frozen pathology” huchukua hadi dakika 45 na usahihi wake ni takribani asilimia 70. CDP hupunguza muda wa maamuzi ya daktari, huongeza usahihi wa uchunguzi, na kupunguza hatari ya kurudi kwa saratani. Kulingana na takwimu za kimataifa, mwanamke mmoja kati ya watano hupata kurudi kwa saratani baada ya upasuaji, mara nyingi kwa hali kali zaidi. Nchini Iran, kiwango cha kurudi kwa saratani kinakadiriwa kufikia asilimia 30, na sehemu kubwa inahusishwa na mapungufu ya mbinu za ‘patholojia ya baridi’. Yazdi alisema kifaa hiki kinaweza kupunguza angalau asilimia 20 ya makosa hayo.

Kifaa kimeidhinishwa na madaktari bingwa wa upasuaji wa matiti nchini Iran na kinatumika katika hospitali kadhaa ikiwemo Shohadaye Tajrish na Imam Khomeini mjini Tehran, Maryam Hospital (Alborz), Seyed al-Shohada (Isfahan), na Shiraz Central Hospital. Kichwa cha kifaa hutupwa baada ya matumizi ili kuzuia maambukizi na kulinda usalama wa wagonjwa na wahudumu wa afya. Bei ya kifaa ni bilioni 2.5 tomani, huku serikali ikitoa ruzuku ya asilimia 40 kwa hospitali za umma.

Zaidi ya hati miliki tano za teknolojia hii zimesajiliwa Marekani, na matokeo ya tafiti yanaendelea kuchapishwa katika majarida ya kimataifa. Yazdi alieleza kuwa kwa kuwa teknolojia hii ni mpya kabisa, majaribio ya kimataifa yakikamilika, kifaaa hiki kitaanza kusambazwa duniani.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *