Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Muda wa kusoma: Dakika 3
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imetoa tathmini ya hali ya usalama katika mji wa Uvira, kufuatia tangazo la waasi wa AFC/M23 kwamba wanaanza kujiondoa taratibu kutoka mji huo.
Akizungumza na waandishi wa habari, msemaji wa serikali Didier Kabi alisema tangazo hilo ni “onesho lililopangwa” na waasi hao, akidai kuwa linalenga kupunguza shinikizo kutoka kwa washirika wao wa kimataifa.
Kwa mujibu wa serikali, kuna taarifa za kuaminika zinazoashiria kuwa kinachoonekana kama kujiondoa ni mbinu ya kuficha ukweli. Msemaji huyo alisema kuwa katika video zilizosambazwa mitandaoni, magari ya waasi yalionekana kuwa tupu, yakibeba madereva pekee au watu wachache sana.
Aidha, alisema maelezo kuhusu kujiondoa huko hayako wazi, kwa kuwa waasi hawajaeleza wanajiondoa hadi wapi, wala zoezi hilo halijasimamiwa ili kuthibitisha kuwa wamefikia maeneo yao ya awali.
Bw. Kabi aliongeza kuwa usiku huo huo, waasi wengine walionekana wakipita kwa miguu kupitia njia ya Muami, wakipitia vilima vya Kashekebwe kuelekea nyanda za juu za Uvira, ili kuungana na washirika wao katika eneo la Fizi, jambo ambalo, kwa mujibu wa serikali, linaashiria jaribio la kuuzingira mji wa Uvira.
Alisema wanajeshi waliokuwa wakielekea Makobola wakipitia Baraka bado wako umbali wa kilomita tisa kutoka Uvira, wakiwa na silaha zao nzito, na hawajaonesha nia ya kuondoka.
Serikali pia ilidai kuwa wanajeshi wa Rwanda wanaodaiwa kuhusishwa na M23 walionekana katika mzunguko wa Kavimvira, ingawa hawakuingia ndani ya mji wa Uvira. Kwa mujibu wa serikali, hali hiyo inaunga mkono madai kwamba tangazo la kujiondoa lilikuwa ni hila ya kupotosha maoni ya umma wa kitaifa na kimataifa.
Zaidi ya hayo, serikali ilisema watu wasiofahamika waliovalia mavazi ya kiraia wameonekana mjini Uvira watu ambao hawajawahi kuonekana hapo awali. Inadaiwa kuwa ni waasi waliovua sare za kijeshi ili kujificha kama raia wakisubiri mashambulizi mapya.
Kutokana na hali hiyo, serikali ya DRC imesema inaendelea kuwa na shaka kuhusu madai ya kujiondoa kwa M23, hasa kwa kuwa vikosi vya serikali bado havijarejea kikamilifu mjini humo.
Shirika la Msalaba Mwekundu limesema kuwa linaendelea kupokea na kutibu majeruhi wapya, ishara kwamba mapigano bado hayajaisha.
Kwa nini Uvira ni muhimu kwa M23?
Chanzo cha picha, AFP
Mchambuzi wa masuala ya eneo la Maziwa Makuu, Christian Moleka, anasema hakuna uhakika kwamba waasi hao wamejiondoa kweli, kwani hakuna uwepo wa serikali mjini Uvira wa kuthibitisha hali hiyo.
Anasema hatua hiyo inaonekana zaidi kuwa ni mwitikio wa shinikizo kutoka Marekani. Kwa mujibu wake, Uvira ni mji wa kimkakati kwa waasi, kwa kuwa ni ngome muhimu katika jimbo la Kivu Kusini na njia ya kuelekea Katanga.
“Uvira uko kando ya Ziwa Tanganyika, jambo linalowezesha kufikia Kalemie na kuweka ushawishi Katanga. Pia ni kitovu cha usafirishaji kuelekea Burundi kwa kuwa uko karibu na Bujumbura,” anaeleza.
Shinikizo la kimataifa na mashaka ya raia
Chanzo cha picha, Reuters
Kundi la M23 lililiteka jiji la Uvira wiki iliyopita lilisema linaanza kujiondoa, likiahidi kukamilisha zoezi hilo Alhamisi, kufuatia shinikizo kutoka Marekani.
Hatua hiyo ilikuja siku chache baada ya kusainiwa kwa makubaliano ya amani kati ya serikali za DRC na Rwanda huko Washington, yakisimamiwa na Marekani. Hata hivyo, waasi wa M23 hawakuwa sehemu ya makubaliano hayo, ingawa walihusika katika mchakato sambamba wa mazungumzo ulioratibiwa na Qatar.
Baadhi ya wakazi wa Uvira waliiambia BBC kuwa bado haijabainika kama waasi wameondoka kabisa, wakisema kuwa magari yao bado yalionekana yakizunguka mjini humo.
Msemaji wa serikali, Patrick Muyaya, alisema tangazo la M23 lililenga kupotosha juhudi za upatanishi za Marekani, ingawa alilitaja kama “ishara chanya” inayohitaji kuthibitishwa.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mashambulizi ya Uvira yamesababisha vifo vya makumi ya watu, zaidi ya 100 kujeruhiwa, na zaidi ya watu 200,000 kuyahama makazi yao. Takribani raia 30,000 wamekimbilia nchini Burundi.