Leo ni Jumatatu tarehe Mosi Rajab 1447 Hijria, mwafaka na 22 Disemba 2025.
Leo ni tarehe Mosi Rajab, mwezi uliojaa rehema na fadhila tele. Mwezi huu na miezi miwili inayofuata yaani Sha’aban na Ramadhan ni kipindi muhimu kwa ajili ya kujisafisha mwanadamu na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Kuhusiana na mwezi huu wa Rajab, Mtume Muhammad (SAW) amesema: “Mwezi wa Rajab ni mwezi mkubwa wa Mwenyezi Mungu…kupigana vita na makafiri ndani ya mwezi huu ni haramu. Rajab ni mwezi wa Mwenyezi Mungu, Sha’aban ni mwezi wangu na Ramadhan ni mwezi wa umma wangu.”
Kufunga Saumu katika mwezi huu kumesisitizwa sana na kuna thawabu nyingi. Baadhi ya hadithi zimesisitiza sana kufunga Saumu na kuomba maghfira na msamaha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu katika mwezi huu.
Katika mwezi huu kuna matukio mawili muhimu. Tukio la kwanza ni kuzaliwa Imam Ali (as) tarehe 13 ya mwezi huu na tukio la pili ni kubaathiwa na kupewa Utume Mtume Muhammad (saw) tarehe 27 ya mwezi huu wa Rajab.

Siku kama ya leo miaka 2171 iliyopita, duru ya tatu na ya mwisho ya vita vya kihistoria na vya umwagaji damu kati ya tawala za kifalme za Carthage na Roma ilimalizika kwa kupata ushindi Waroma na kuanguka utawala wa Wacartharge.
Vita vya falme hizo mbili vilijulikana kwa jina mashuhuri la vita vya Punic. Utawala wa kifalme wa Carthage ulikuwa moja kati ya tamaduni kongwe huko kaskazini magharibi mwa Afrika na katika pwani ya Bahari ya Mediterrania.

Siku kama ya leo miaka 1390 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia alizaliwa Imam Muhammad Baqir AS mjukuu mtukufu wa Mtume Muhammad (SAW) na mmoja wa Maimamu watoharibu kutoka katika kizazi chake.
Imam Baqir AS alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina na kupata umashuhuri katika uwanja wa elimu, ambapo alikuwa akijibu maswali na masuala magumu ya zama na kwa sababu hiyo alipewa lakabu ya Baqir yaani mchimbua elimu.
Kipindi cha Uimamu wa mtukufu huyo kiliambatana na kudhoofika kwa utawala wa Bani Umayyah suala ambalo lilimpa fursa nzuri ya kulea Waislamu wa zama hizo kifikra na kielimu. Imam Baqir (as) alisifika kwa ukarimu, kuwasamehe waliomkosea, kuwasaidia masikini na kuwatembelea wagonjwa.

Miaka 386 iliyopita katika tarehe kama ya leo, alizaliwa Jean Racine malenga na mwandishi wa michezo ya kuigiza wa Kifaransa.
Racine alianza kazi ya uandishi katika uwanja huo baada ya kusoma kwa muda fulani na kuhitimu akiwa na umri wa miaka 18. Hata hivyo muda fulani baadaye alianza kukosoa kazi hiyo baada ya kuandika mchezo wa tanzia alioupa jina la Andromaque na kupata umashuhuri.
Alianza kuakisi matukio ya mfalme wa wakati huo wa Ufaransa. Jean Racine alifariki dunia mwaka 1699.

Katika siku kama ya leo miaka 332 iliyopita, ulitokea mtetemeko mkubwa wa ardhi katika kisiwa cha Sicily kusini mwa Italia.
Kufuatia zilzala hiyo, miji mitatu mikubwa ya kisiwa hicho ilibomolewa na kusababisha hasara kubwa kwa miji mingine yakiwemo makao makuu ya kisiwa hicho yaani Palermo.
Mtetemeko huo wa ardhi unahesabiwa kuwa mkubwa zaidi kuwahi kutokea nchini Italia. Zaidi ya watu 80,000 walipoteza maisha yao katika janga hilo la kimaumbile.
