KESHOKUTWA ni siku ya Mkesha wa Sikukuu ya Krismasi inayosherehekewa Desemba 25, 2025. Siku kama hiyo wiki ijayo; Alhamisi, Januari Mosi, 2026 ni Sikukuu ya Mwaka Mpya. Hizi ni sikukuu za kiroho zinazostahili si shamrashamra za kimwili, bali za kiroho zaidi maana siku hizi kumaliza mwaka ni kazi.
Kwamba Krismasi si tu kula mapochopo ya kuku wa kukaanga ama supu, ‘kitimoto,’ soda, juisi na maji baridi au vilevi kwamba watu wale na kunywa hadi ‘kuchakaa’ na kubebwa huku wakijidhalilisha kimwili na kiroho.
Hizi si sikukuu za kuonesha ubingwa na utalaamu wa ufuska; uzinzi na uasherati hadi ‘kutengeneza’ mimba zisizo na baba anayefahamika au kuzoa maradhi ya kuambukiza kupitia ngono, la hasha! Krisimasi na Mwaka Mpya ni sikukuu za kumshukuru Mungu zaidi kwa wema anaowatendea wanadamu hata kuwapa zawadi ya amani na uhai; tunu zenye thamani kubwa zaidi kuliko nyingine zote duniani.
Ni sikukuu za kutafakari na kubaini watu wanajikwaa wapi na wameangukia wapi ili wafanye marekebisho kwa ‘kuzaliwa upya.’ Kwa mfano, mwaka huu Watanzania wajiulize na kutafakari kisha wamwombe radhi Mwenyezi Mungu hususani kuhusu ‘walipojikwaa’ katika suala la amani ya nchi.
Hii ni kutokana na vurugu zilizotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Okotba 29, 2025 na kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali za umma na za watu binafsi sambamba na miundombinu. Kisha wamwombe radhi Mungu wakisema, “Mwenyezi Mungu mwaka 2025, tumekosa sisi, tumekosa sana; tunaomba utusamehe na ututie nguvu huku ukitupa macho ya kuona ukweli kwamba, tumekosea, hivyo tusirudie kosa.”
Wakati Watanzania wakifanya hilo katika sherehe hizi za mwisho wa mwaka, waepuke kasumba ya kunyoosheana vidole na kutafuta ‘wachawi’ na kunyosheana vidole maana hiyo nayo ni ‘dhambi na ugonjwa wa kuambukiza usiopona.’ Kila Mtanzania akumbuke kuwa, unapomnyoshea mwezio kidole, vidole vingine vinakuelekea wewe.

Hii inamaanisha kuwa, kila mmoja ana nafasi na mchango alioutoa katika kujenga na hata kufanya kosa la kujaribu kubomoa amani ya nchi. Kisha, Watanzania ‘wakae chini na kwenda msituni kutafuta fito’; waje waunganishe nguvu na kujenga nyumba yao; Tanzania iliyo bora zaidi maana kupotea njia ndiko kujua njia.
Watambue kuwa, sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya si sikukuu za kuvaa nguo mpya, viatu vipya wala kumiliki simu mpya, kutelekeza familia na kufanya yasiyopendeza jamii na Mungu, bali kutafakari Amani na Upendo wa Mungu.
Sikukuu za Krismasi 2025 na Mwaka Mpya 2026, zinasherehekewa huku kwa kazi na mikono yao, Watanzania kwa kujidanganya na kukubali kudanganyika, wamelazimisha askari katika maeneo mbalimbali ama kupigwa vumbi, jua au mvua na kuumwa na mbu ili kulinda amani na usalama wa nchi, raia na mali zao usichezwe tena; kwa kweli Watanzania hawana budi kusema, “Kwa kukubali kudanganywa na kujidanganya, tumekosa sisi, tumekosa sana.”
Kuzaliwa kwa Yesu Kristo kuwaamshe Watanzania ili wazaliwe na Yesu kiroho na kiakili. Aidha, ‘kuzaliwa’ kwa mwaka mpya, kuwafanye Watanzania wazaliwe upya. Kila mmoja alenge kulinda upendo na amani tangu alipo, familia yake, jamii na taifa kwa ujumla. Kuzaliwa kwa Yesu Kristo katika Krismasi kulete mabadiliko na fikra chanya. Matashi ya haki za kisiasa, yasitumike kuangamiza haki ya amani na nchi kwa ujumla.
Watanzania watumie kipindi hiki kumwombna Mungu ‘awape macho’ ya kuona hila za wanyonyaji na makupe wa kimataifa kupitia vibaraka wa ndani na nje ya nchi wasidanganye Watanzania ‘kukata tawi la mti walilokalia’ au kupiga kwenzi ncha ya mkuki.Kipindi hiki kiwape Watanzania jicho dhidi ya vurugu, ubaguzi na chuki za namna yoyote ama ziwe za kijinsia, kikabila, kimajimbo, kisiasa wala kidini
Hizo ni sumu kali maana madhara yake hayabagui wala kuzalisha mshindi wala mshindwa; pande zote huathirika vibaya katika nyanja mbalimbali. Watanzania watumie kipindi hiki kumwomba Mungu kama anavyowapa uzima, basi pia azidi kuwapa amani ili wawe nayo, kisha wawe nayo tele.

Ndiyo maana ninasema, Novemba 18, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan alitenda vyema. Aliunda tume huru kuchunguza matukio ya vurugu yaliyotokea Oktoba 29, 2025 wakati wa Uchaguzi Mkuu na baada ya hapo. SOMA: Makosa ya kifedha katika Krismasi, Mwaka Mpya
Tume hiyo yenye wajumbe wanane inaongozwa na Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman. Rais amefanya jema ili kujua kiini cha vurugu hizo na kutafuta dawa; amefanya jema maana kichuguu hakimalizwi kwa kuzoa udongo wa juu, bali kwa kumuondoa malkia wa mchwa yaani, tatizo huondolewa kwa kupata na kuondoa kiini cha tatizo.
Wimbo ‘Kichuguu’ wa Kinondoni SDA Church Choir unasisitiza hilo ukisema, “Dhambi ni kama mchwa mharibifu unaokula mbao za nyumba. “Kadiri mwenye nyumba anavyowaua wengine hutokeza zaidi; leo kama utawazuia kwa saruji keshokutwa mbao zimeliwa. Walipopita hakujulikani, dawa ni kumuondoa malkia, ni kuchimba kichuguu tu, utampata malkia (kiini cha tatizo)…
” Tume chini ya Jaji Chande ‘itachimba kichuguu’ kupata kiini cha tatizo ili kipatiwe dawa na hatimaye, Watanzania wasirudie kosa la kuchezea amani ya nchi yao ama kwa kujidanganya, kudanganywa au yote kujidanganya na kudanganywa, maana kufanya kosa si kosa, bali kurudia kosa na kupotea njia, ndiyo kujua njia.
Viongozi wa dini na taasisi zote za dini watumie kipindi cha sikukuu za mwisho na mwanzo wa mwaka kuhimiza utu, upendo, mshikamano, umoja na amani bila kunyoosheana vidole, bali kuoneshana ‘njia ile iendayo uzimani.’
Kupitia Krismasi, Mungu analeta amani na ukombozi wa ulimwengu. Watanzania wachangamkie na kupokea ukombozi huo kwa mikono miwili ya shukurani maana kuzaliwa kwa Yesu Kristo kunakuja kudumisha tunu ya amani ili watu waishi kwa amani na kupata maendeleo.
Ijulikane kuwa, bila amani hakuna maendeleo ama watu kiroho au kimwili, wala maendeleo ya vitu; hakuna. Wanaposherehekea sikukuu hizi, kila mmoja apanie kukomesha, kuua na kuzika chuki zote zikiwamo hatari zadi za kidini na hiyo iwafanye Watanzania na Tanzania yao wazidi kuwa ‘Kisiwa cha Amani’ katika ‘Bahari ya Umoja.’
Wiki iliyopita akiwa mkoani Songwe, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba alisisitiza umuhimu wa amani nchini akisema moja ya faida zake ni upendo unaowafanya Watanzania wa jamii mbalimbali kushirikiana katika mambo mengi yakiwamo ya sherehe za kiimani bila ubaguzi.
Dk Mwigulu anasema Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliwaachia Watanzania amani itokayo kwa Mungu kiasi kwamba, wakati wa sikukuu hata za kidini kama Krismasi watoto wa Waislamu, Wakristo na wengine huomba na kununuliwa nguo mpya na wote wakaenda kutembea na kufurahi kwa pamoja bila shida.
Anasema hata yeye ni miongoni mwa wanaovaa kanzu na kwamba, mara nyingi kipindi cha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani hualikwa kufuturu kuliko hata Waislamu wengi waliofunga. Dk Mwigulu anasema hilo ni jambo la Watanzania kujivunia na kumshukuru Mungu. Kimsingi, Watanzania wanaposherehekea Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya, wazaliwe kiroho na kiakili.
Asiwepo Mtanzania wa imani yoyote anayejidanganya au kukubali kudanganywa kuchezea amani ya Tanzania kwa kisingizio chochote ama cha siasa, au dini; amani ni zawadi ya Mungu.
Watanzania wailinde tunu hiyo, wasiipuuze wala kuikataa maana kama watafanya kosa la kuonea aibu amani yao ambayo ni zawadi kutoka kwa Mungu, ipo siku amani hiyo nayo itawaonea aibu mbele za Mungu na hapo, patakuwa na kulia na kusaga meno. Kila la heri ya Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya 2026 wenye amani.