Afrika imeazimia ipasavyo kulipwa fidia ya kipindi cha utumwa kutoka nchi za Magharibi, na katika suala hili, Rais wa Ghana amechukua jukumu la kudai fidia ya kipindi cha utumwa Wazungu barani Afrika.

Rais wa Ghana, John Dramani Mahama, amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa kimataifa unaotaka kulipwa fidia ya utumwa na ukoloni, akikubali jukumu la kujaribu kudai fidia kutoka nchi za Magharibi kwa utumwa na ukoloni wa nchi hizo barani Afrika. Ujumbe huo ambao unaundwa na wataalamu kutoka Afrika, Karibia, Ulaya, Amerika Kusini na Marekani, umejadili hatua za kipaumbele cha ajenda ya kulipwa fidia ya Umoja wa Afrika.

Suala la kulipwa fidia za mateso na manyanyaso ya enzi ya utumwa limekuwa takwa la nchi za Afrika kwa muda mrefu, kwa sababu utumwa sio ukurasa wa giza tu katika historia ya Afrika; bali pia ni jeraha kubwa na la kudumu kwenye mwili wa Afrika ambalo halijapona licha ya kupita karne nyingi za umwagaji damu, machozi na waafrika kuhamishwa kutoka sehemu moja hadi nyingine ya dunia na kuuzwa kama watumwa. Leo, nchi za Kiafrika zinadai fidia kutoka kwa nchi za Magharibi, lakini lengo lao si tu kupokea fidia ya hasara za kimaada, bali pia kurejeshewa heshima na hadhi ya binadamu, Wazungu kukiri kwamba walifanya jinai na uhalifu wa kutisha, na kurekebishwa miundo inayoendeleza utumwa katika mfumo wa ubaguzi wa rangi, dhulma na umaskini.

Maafisa wa nchi za Afrika wanaamini kwamba, utajiri ambao Magharibi imepata ni matokeo ya unyonyaji wa watu wa Afrika. Kwa mujibu wa rekodi za kihistoria, katika karne tano zilizopita, kwa uchache Waafrika milioni 12.5 walitekwa nyara na kusafirishwa kwa nguvu na meli za Wazungu, kisha wakauzwa utumwani kuanzia karne ya 15 hadi 19. Kwa hakika, utumwa haukuwa tukio la kupita, bali mradi uliopangwa uliowatenganisha mamilioni ya watu na nyumba, familia na tamaduni zao. Binadamu hao hawakuwa vibarua wa kazi tu, bali pia walitumiwa kama nishati ya injini ya Mapinduzi ya Viwanda ya Ulaya na ustawi wa uchumi wa Marekani. Wakati huo huo, karne nyingi za utumwa zimelinyima bara la Afrika rasilimali watu, vipaji na uwezo wa maendeleo na hivyo kulibakisha nyuma na kulifanya tegemezi; mambo ambayo athari zake bado zinashuhudiwa hadi hii leo.

Mmilioni ya Waafrika waliuzwa na Wazungu kama watumwa

Historia ya utumwa inaonyesha kwamba nchi nyingi za Ulaya zilishiriki katika uhalifu huo, ikiwa ni pamoja na Ureno, Uingereza, Ufaransa, Uholanzi na Uhispania. Ureno ilikuwa mstari wa mbele katika biashara ya watumwa kutoka Afrika, hasa katika karne za 15 na 16, ikipanua makoloni yake huko Brazil na sehemu nyingine za dunia kwa kutumia kazi za watumwa. Uingereza na Ufaransa pia zilikuwa wafaidika wakuu wa biashara ya watumwa, zikianzisha mitandao tata ya biashara hiyo na kusafirisha mamilioni ya watumwa kutoka Afrika kwenda Amerika na Karibea. Kwa kutumia nguvu kazi ya Waafrika, nchi hizi zilijikusanyia utajiri mkubwa, ambao athari zake bado zipo katika miundo yao ya kiuchumi na kijamii na ile ya makoloni yao. Kwa maneno mengine tunapaswa kusema kuwa, utajiri mkubwa ambao nchi za Magharibi zinajivunia hivi sasa ulijengwa juu ya mateso na unyonyaji wa watu wa Afrika, na bado unazalishwa duniani kote katika mfumo wa ukosefu wa usawa wa kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Viongozi wa Afrika wanasisitiza kwamba kudai fidia ya kipindi cha ukoloni na utumwa wa Wazungu si takwa la kisiasa tu, bali ni dharura ya kimaadili na kihistoria. Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa zamani wa Tume ya Umoja wa Afrika, anasema kuhusu suala hili kwamba: “Hakuna jamii inayoweza kujengwa juu ya kusahau uhalifu. Kukiri na kulipa fidia ni masharti ya suluhu ya kweli.”

Rais wa Ghana, John Dramani Mahama, ambaye sasa amekubali kubeba jukumu la kufanya juhudi za kudai fidia ya sulubu za kipindi cha utumwa, amesisitiza mara kwa mara kwamba viongozi wa bara la Afrika lazima wachague ujasiri badala ya kuketi na kufarijika tu. Mahama alisisitiza katika mkutano wa hivi karibuni wa Umoja wa Mataifa kwamba: “Tukiendelea kubalia kimya, ukimya huu utakuwa na maana ya kukubali mwendelezo wa dhuluma. Lazima tuungane ili kuwa sauti za mamilioni ya roho zilizozikwa katika vina vya bahari ambazo bado zinadai haki. Takwa hili ni mwangwi wa maumivu ya kihistoria na wito wa kuchukua hatua kwa pamoja.”

John Dramani Mahama

Sababu za kudai fidia ya utumwa ziko wazi sana. Kwanza, ni haki ya kihistoria. Hakuna taifa au taasisi inayoweza kukwepa jukumu lake la kuhusika na utumwa. Kama ambavyo ulimwengu umekubali kuanzisha mahakama na kulipa fidia kwa uhalifu wa kivita na mauaji ya kimbari, vilevile utumwa unapaswa kufuatiliwa kwa kiwango sawa cha uzito.

Pili, ni udharura wa kurekebishwa miundo ya taasisi za kimataifa. Mfumo wa kiuchumi na kisiasa wa kimataifa bado unazalisha ukosefu wa usawa unaotokana na kipindi cha ukoloni na utumwa. Fidia inaweza kuwa mwanzo wa kurekebishwa dhulma hizi.

Tatu, ni udharura wa kupambana na ubaguzi wa rangi. Ubaguzi wa rangi wa kisasa una mizizi katika utumwa. Kulipa fidia na kukiri rasmi uhalifu huo ni hatua ya kwanza ya kuondoa doa hilo katika dhamiri ya kimataifa.

Nne, ni kuiwezesha Afrika. Rasilimali za kifedha na misaada ya kisiasa inayotokana na fidia hiyo inaweza kusaidia kukuza miundombinu, elimu, afya na kujenga upya jamii za Kiafrika.

Kwa kuzingatia hayo yote, Afrika inapaswa kuungana katika kusisitiza takwa hili. Umoja wa Waafrika katika kudai fidia ya kipindi cha utumwa wa Wazungu si takwa la kisiasa tu, bali pia ni wajibu wa kimaadili na kihistoria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *