Makosa ya kifedha katika Krismasi, Mwaka MpyaMakosa ya kifedha katika Krismasi, Mwaka Mpya

BADO takriban siku mbili Wakristo nchini waungane na wenzao duniani kusherehekea kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo yapata miaka milioni mbili iliyopita, yaani Noel; Sikukuu ya Krismasi itakayofuatiwa na mkesha wa Mwaka Mpya kuuaga mwaka 2025 na kuanza mwaka mpya Januari Mosi, 2026.

Katika kipindi hiki hadi baada ya Sikukuu ya Mwaka Mpya, ni nadra kusikia jina la mwezi Januari likitajwa kwa wema. Januari ni lango la mwaka mzima na mwezi ambao mzaliwa wa kwanza wa mwaka. Baada ya Januari 2 au wiki moja zaidi, ndipo kila mmoja anaanza kusingizia Januari ama kukwepa majukumu, kuficha uzembe wake katika kupanga na kutumia usijulikane au kutafuta njia ya kuombea misaada na mikopo.

Mwezi Januari baada ya Krismasi na Mwaka Mpya, ni kipindi ‘kichafu’; kipindi ambacho baadhi ya watu wanafikia hatua ya ‘kuua’ ndugu zao. Kwa kisingizio cha Januari, ‘wanatengeneza’ misiba ya watu wao wa karibu ili wapate rambirambi na michango mbalimbali ya kuwavusha. Aibu na kosa kubwa.

Wengi wao, kabla ya hapo husikika mara nyingi wakisema, “Januari ngumu sana” au “Hali ngumu sana mwezi huu.” Kimsingi, kwa watu wenye kipato cha chini na cha kati, Januari ni wakati ambao wengi wanalia kutokana na masuala ya ada, kuandaa na kusafirisha wanafunzi, pango la nyumba, pango la vibanda vya biashara na matumizi mengine ya msimu, yakiwemo ya kilimo.

Mmoja anaandika mtandaoni akisema, “Kwa watu wengi, hiki ni kipindi chenye mahitaji makubwa ya kifedha, huku kipato kikiwa kile kile na pengine kimepungua.” Januari ni mwezi unaofuata baada ya Desemba ambao ni mwezi unaokuwa na shughuli nyingi za kijami na kifamilia, zikiwamo shamrashamra wa sikukuu za mwisho wa mwaka, yaani Krismasi na Mwaka Mpya.

Uchunguzi na uzoefu wa HabariLEO umebaini kuwa, hizo ni sikukuu zinazotumia gharama kubwa kuzisherehekea huku watu wengi wakiwa na mihemko na hisia kali za ‘kula maisha’ bila kujali kuwa kuna maisha baada ya sikukuu. Mwandishi Mwandamizi wa Shirika la gazaji la Uingereza (BBC), Leonard Mubali ananukuliwa mtandaoni akisema,

“Januari inabebwa na mshahara wa mwezi Desemba kwa wanaofanya kazi na mshahara wa Desemba kwa taasisi nyingi, hasa binafsi hutoka mapema na huisha mapema pia, na hicho kinasababisha ugumu wa mwezi Januari kwa wengi.” SOMA: Watoto 38 wazaliwa mkesha wa krismas Arusha

Vyanzo mbalimbali vinataja sababu kadhaa za Januari kuwa mwezi mgumu kifedha, vikisema ni pamoja na matumizi makubwa ya fedha kwa wengi wanaokwenda likizo za Mwaka Mpya na Kisrimasi. Januari hutanguliwa na Desemba ambao ni mwezi wa sherehe, zawadi na likizo za familia. Chanzo kimoja kinasema, “Watu wengi hutumia fedha nyingi kununua zawadi, kwenda likizo na kusherehekea mwaka mpya kwa mavazi mapya yao na ya watoto.”

Aidha, hutumia ‘vyakula vipya’ na vya kipekee ambavyo wakati mwingine huliwa kwa ‘kufuru’, kwani hakuna anayetaka yeye au familia yake kuonesha unyonge katika matumizi wakati wa Krismasi na Mwaka Mpya. Imebainika pia kuwa, hiki ni kipindi cha mihemko ya matumizi ya fedha, hatari sana.

Ndio maana baadhi ya watu huathirika kisaikolojia na kulewa kupindukia, huku wengine wakifanya maonesho ya makusudi ili watambulike. Ukarimu ni muhimu lakini wengine huonesha ukarimu wa bandia katika makundi mbalimbali ya starehe.

Kimsingi, Januari ndio mwezi wa mapambazuko na kupiga hesabu za mapato na matumizi ya wakati wa sikukuu hizo; ndio mwezi wa kurekebisha hali ya kifedha, huku wengi wakipaswa kulipa kodi ya nyumba kwa msimu mpya na mahitaji ya shule kwa watoto.

Ikumbukwe kuwa, baadhi ya biashara au kampuni hupunguza idadi ya kazi, wafanyakazi au mishahara wakati wa msimu wa likizo. Wengine hushindwa kufanya mauzo makubwa kama wakati wa sherehe za mwisho wa mwaka. Hii ina maana kwamba, watu wanakuwa na mapato madogo kuliko kawaida, huku gharama za kila siku zikiendelea.

Baadhi ya watu wanajikuta wakikopa ili kufanikisha sherehe za mwaka mpya au shughuli nyingine za Desemba. Januari huwa ni mwezi wa kurejesha mikopo hiyo. Hii huwa changamoto kubwa kwa watu wengi, hasa wale wanaokopa kwa riba kubwa, kwani marejesho yanaweza kuwa mzigo mkubwa wa kifedha.

Katika mazungumzo na HabariLEO, Ofisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Ngorongoro, Arusha, Benezeth Bwikizo anasema, “Tatizo kubwa katika kipindi hiki ni kuwapo kwa hali ya kuiga mkumbo na mivuto ya kijamii… Hii ni pamoja na baadhi ya watu kutaka wanunue vitu kama mavazi au vyakula vya gharama kubwa ili waonekane kwa wengine.”

Anaongeza: “Kwa mfano, watu wengi wanataka kununua nguo mpya na mapambo mbalimbali, yakiwamo ya nyumbani… Ndiyo sababu hata bei ya bidhaa nyingi kama nyama na hata mifugo kama kuku hupanda bei,” anasema. Anasistiza: “Si sahihi kukopa kwa ajili ya sikukuu au sherehe na vitu kama zawadi kwa wapendwa, maana si dharura.” “Upendo haupimwi kwa zawadi pekee; basi viandaliwe bajeti yake maana sikukuu za mwisho wa mwaka si dharula ya kukufanya ukope,” anasema.

Mtaalamu huyo wa masuala ya kijamii anasisitiza kuwapo maandalizi ya mapema kwa ajili ya sikukuu hizo ili kuepuka kuvuruga bajeti. “Tupange na kujiandaa kwa ajili ya sikukuu hizi tangu Januari, tukijua kuna sikukuu za mwisho wa mwaka na mwanzo wa mwaka,” anasema. Anabainisha siri: “Moja ya njia rahisi na muhimu ni kuanzisha ‘kibubu’ chako ama cha nyumbani au benki kwa ajili ya mambo ya sikukuu.

Kila mahitaji yaandaliwe mpango na bajeti yake mapema na kuwekeza kidogokidogo.” Mtaalamu wa masuala ya fedha katika East African Insurance Agency, Amani Waziri anasema si busara kukopa kwa ajili ya sikukuu na kufanya sherehe, maana sikukuu huwa siku moja lakini mkopo hudumu kwa siku na miezi mingi.

Anasema ikibidi kukopa, mtu akope ili kuzalisha mali na kuongeza thamani kama elimu au kuwekeza lakini si kukopa kwa ajili ya sherehe. Waziri ananunukuliwa katika kipindi cha Amka na BBC Desemba 16, mwaka huu akisema njia bora ya kusherehekea sikukuu bila kuwa na msongo wa mawazo ni kuwa na mfumo wa wazi wa bajeti mapema.

Kwamba, ni vizuri kuzingatia na kutumia asilimia 25 ya mapato yako kwa ajili ya akiba na uwekezaji, asilimia 50 kwa mahitaji ya msingi kama chakula, malazi na huduma za afya na asilimia 25 inayosalia, kwa maisha binafsi na mipango maalumu.

Katika kipindi hicho cha BBC, mtaalamu mwingine wa masuala ya fedha, Beatrice Kimaro wa Moshi, Kilimanjaro anasema yapo makosa mengi yanayofanywa na watu katika msimu wa sikukuu, ikiwa ni pamoja na kutumia zaidi kuliko kipato chao halisi.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Consumer Behaviour Index Mwaka 2023, wastani wa asilimia 35 hadi 45 ya watu hutumia zaidi ya bajeti na mishahara yao katika msimu wa sikukuu, hususan za mwisho wa mwaka. Beatrice anataja kosa lingine linalofanya watu wengi kuona Januari katika ugumu kuwa ni kutotofautisha kati ya mahitaji muhimu na ya lazima na matashi.

“Watu wengi wanatumia kuliko uwezo wao kwa kusukumwa na mambo kama ‘discounts’ (punguzo maalumu la bei), sherehe mbalimbali na zawadi… ,” anasema Beatrice. Hii ina maana kuwa, watu wapanga matumizi na kuandaa bajeti mapema.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo wa masuala ya fedha, mwishoni mwa mwaka mahitaji ya watu kwa vitu mbalimbali kama vyakula, mavazi na mahitaji mengine huongezeka. “Mahitaji yanapoongezeka kwa zaidi ya asilimia 30, wauzaji huongeza bei ili kupunguza msongamano wa wanunuzi na hata kuongeza faida,” anasema. Vyanzo na wataalamu mbalimbali wa mambo ya fedha na uchumi wanasema mfumuko wa bei una athari kuu nne kwa mtu binafsi.

Hizo ni pamoja na kuathiri vibaya ununuzi wa bidhaa muhimu, kwani hupungua, matumizi ya lazima kama chakula hupanda bei, huongeza tabia ya kukopa. Kwa mujibu wa taasisi mbalimbali za kifedha, mfumuko wa bei huathiri uwekaji wa akiba.

Vyanzo vinasema mwishoni mwa mwaka watu wengi hawaweki akiba, bali hutumia akiba walizonazo huku matumizi kwa mfano ya mwezi Desemba yakiathiri vibaya matumizi ya Januari. Beatrice anasema mfumuko wa bei huathiri matumizi ya leo na kuharibu mipango ya bajeti.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *