Rabat, Morocco. Kabla ya mchezo wa ufunguzi wa mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 kati ya Morocco dhidi ya Comoros kuanza, wengi waliitabiria makubwa sana timu ya Taifa ya Morocco ambayo ilionekana kupewa nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo ambao ulipigwa kwenye dimba la Prince Moulay Abdallah, jijini Rabat nchini Morocco ambako ndiko yanafanyika mashindano hayo yanayotarajiwa kufikia tamati Januari 18, 2026.
Dakika 45 za kwanza
Katika mchezo huo ambao wenyeji walionekana kuwa na nafasi kubwa ya ushindi, mambo hayakuwaendea vizuri katika dakika 45 za kipindi cha kwanza ambazo ziliacha maswali mengi ni kwanini Morocco haikupata bao. Pengine mkwaju wa penalti alikosa mshambuliaji, Soufiane Rahimi dakika ya 11 ungeifanya timu hiyo kuondoka kifua mbele kwenda mapumziko lakini uimara wa golikipa wa Comoros, Yannick Pandor ulifanya kipindi cha kwanza kiwe kigumu kwa wenyeji hao baada ya kupangua penalti hiyo.
Hata hivyo, Comoros ilicheza kwa ukomavu wa hali ya juu huku ikiwaheshimu wapinzani wake ambao walionekana wakilisakama lango kwa kufanya mashambulizi kadhaa ambayo hayakuzaa matunda hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zilipomalizika milango ikiwa bado migumu.
Dakika 45 za pili
Kipindi cha pili kilipoanza Morocco iliingia kwa kasi zaidi huku ikiendelea kufanya mashambulizi ya kupata bao la uongozi. Dakika 10 zilitosha kuwafanya Simba wa Milima ya Atlas kupata bao ambalo lilifungwa na Brahim Diaz, nyota anayekipiga kwenye Klabu ya Real Madrid ya Hispania ambaye alimalizia pasi ya Noussair Mazraoui, mlinzi kutoka Man United ya England.
Katika dakika ya 74 Ayoub El Kaabi, mshambuliaji aliyetambulishwa mchezoni dakika ya 65 kuchukua nafasi ya Soufiane Rahimi aliandika bao la pili kwa ustadi mkubwa baada ya kumalizia pasi ya Anass Salah-Eddine. El Kaabi anayechezea Olympiacos ya Ugiriki alifunga bao hilo la kuvutia ambalo lilidumu hadi dakika 90 za mwamuzi Jean-Jacques Ndala Ngamo kutoka DR Congo zilipomalizika.
Hali ya vikosi
Licha ya Morocco kupata matokeo ya ushindi lakini haikuwa rahisi kuikabiri Comoros ambayo kwa kiasi kikubwa ilikuwa na wachezaji wazoefu ambao wengi wanacheza ligi za kulipwa nje ya taifa hilo hususani Ulaya na Uarabuni. Kama uliangalia vizuri kikosi chao utagundua kuwa wachezaji 11 walioanza kwa upande wa Comoros wote wanatokea Ulaya na baadhi ya timu za Qatar na Saudi Arabia.
Golikipa, Yannick Pandor anatokea Klabu ya Francs Borains inayoshiriki ligi daraja la pili Ubelgiji, yupo beki wa kushoto, Ismael Boura anachezea Troyes inayoshiriki ligi daraja la kwanza Ufaransa, Kenan Toibibou huyu ni beki wa kulia anayekipiga NK Bravo inayoshiriki Ligi Kuu nchini Slovenia, Ahmed Soilihi huyu ni mlinzi wa kati anacheza Toulon inayoshiriki ligi daraja la nne Ufaransa, Yannis Kari pia ni beki wa kati anayekipiga Frejus Saint Raphael inayoshiriki ligi daraja la nne Ufaransa.
Wapo viungo kama Zaydou Youssouf anayecheza Al Fateh inayoshiriki Ligi Kuu ya Saudi Arabia ‘Saudi Pro League’, Iyad Mohamed huyu anaichezea Casa Pia inayoshiriki Ligi Kuu nchini Ureno ‘Liga Portugal’, mwingine ni Benjaloud Youssouf anayecheza Sochaux inayoshiriki ligi daraja la tatu Ufaransa, Youssouf M’Changama huyu ni kiungo mshambuliaji anayechezea Al Batin inayoshiriki ligi daraja la kwanza Saudi Arabia. Wapo washambuliaji kama Faiz Selemani anayekipiga Qatar SC ya Qatar pamoja na Rafiki Said anayekipiga kwenye Klabu ya St. Liege inayoshiriki Ligi Kuu nchini Ubelgiji.
Kilichoibeba Morocco
Mchezo wa jana ulionekana kuwa mgumu kwa upande wa Morocco ambao waliitaji matokeo ya ushindi kuliko sare ambayo ingekuwa ni faida kwa upande wa Comoros lakini yapo mambo ambayo yaliwafanya Simba wa Milima ya Atlas kuibuka na ushindi dhidi ya wapinzani walioonekana kuwa wagumu. Faida ya kucheza kwenye ardhi ya nyumbani mbele ya mashabiki 60180 walioingia uwanjani ilikuwa ni siraha tosha ya kuwapa wenyeji hamasa kupata matokeo dhidi ya wageni waliokuwa na namba ndogo ya mashabiki.
Ubora wa mchezaji mmoja mmoja na uzoefu ni moja ya vitu vilivyoipa Morocco ushindi katika mchezo wa jana kwani ukiachana na kikosi cha Comoros kilichokuwa kimejaa wachezaji wengi kutoka ligi mbalimbali za kulipwa Ulaya na Uarabuni hawakuweza kufua dafu dhidi ya nyota wa Morocco ambao wengi wao wanatokea kwenye Ligi Kuu za Mataifa ya Ulaya wenye uzoefu katika michezo ya ushindani tofauti na nyota wa Comoros ambao wengi wanachezea ligi za madaraja ya chini Ulaya.
Nyota kama Brahim Diaz aliyefunga bao la kwanza ni miongoni mwa wachezaji wakutegemewa na kocha, Xabi Alonso pale Madrid, mshambuliaji El Kaabi aliyefunga bao la pili kwa ustadi mkubwa pia ni nyota anayetegemewa kwenye kikosi cha Olympiacos ya Ugiriki. Ukiachana na hao wapo nyota wengine kama Noussair Mazraoui, mlinzi wa Man United ya England, Ismael Saibari huyu ni kiungo wa PSV ya Uhoranzi, Sofyan Amrabat kiungo mkabaji anayekipiga Real Betis mwingine ni Azzedine Ounahi anayetokea Girona zote za Hispania.
Ilikuwa ni vigumu sana kwa Comoros kushikilia mchezo kutokana na ushindani walioupata kutoka kwa nyota wa Morocco waliokuwa na ubora zaidi uwanjani. Hata hivyo Comoros haikuonyesha unyonge kwa vigogo hao wanaoshika nafasi ya 11 katika viwango vya timu bora duniani na namba moja kwa Bara la Afrika.
Comoros iliibukaje?
Katika kipindi cha miaka ya nyuma Comoros ilikuwa timu dhaifu sana ambayo haikuweza hata kushindana na timu za madaraja ya kati jambo ambalo lilikuwa likiifanya timu hiyo kutoka visiwani kuambulia vipigo katika michezo yake mingi iliyokuwa ikishiriki kwenye mashindano mbalimbali.
Mchakato wa kuanza kuitengeneza timu ya Comoros ulianza rasmi mwaka 2014 baada ya Amir Abdou kuchaguliwa kuwa kocha mkuu wa timu hiyo. Abdou ambaye alizaliwa Marseille nchini Ufaransa na wazazi wake wenye asili ya Comoros alianza kufanya utafiti wa kufuatilia wachezaji wenye asili ya Taifa hilo wanaocheza ligi mbalimbali Ulaya.
Katika ripoti yake ilieleza kuwa wapo watu takribani laki tatu wenye asili ya Comoros wanaoishi Ufaransa, ndipo alipoanza kuwafuatilia wachezaji wenye asili ya Comoros wanaocheza kwenye ligi za Ufaransa. Alianza kuwaita kwenye kikosi cha timu ya Taifa akiwajenga kwa umoja na mshikamano huku akisisitiza umoja wa timu pasipo kutegemea wachezaji masupastaa.
Ilivyoanza kubadilika
Matokeo yalianza kuonekana mwaka 2021, Comoros ilipofuzu kwa mara ya kwanza michuano ya mataifa ya Afrika (AFCON), yaliyofanyika mwaka 2023 nchini Cameroon ambapo iliaga mashindano hayo katika hatua ya makundi baada ya kumaliza nafasi ya tatu kwa jumla ya pointi tatu nyuma ya Morocco iliyomaliza vinara wa kundi kwa pointi saba na Gabon iliyomaliza ya pili kwa pointi tano ikiishinda Ghana iliyomaliza mkiani kwa pointi moja pekee.
Katika hatua ya makundi ya kufuzu michuano ya AFCON ya mwaka huu, Comoros imezidi kuimarika ikifuzu kwa mara ya pili baada ya kumaliza katika hatua ya makundi bila kupoteza mchezo wowote ikikusanya jumla ya pointi 12 katika kundi A lililokuwa na timu za Tunisia iliyomaliza ya pili kwa pointi 10 zikifuatiwa na Gambia na Madagascar ambazo zilitupwa nje. Katika hatua hiyo Comoros ilishinda mechi tatu na kutoa sare mara tatu katika michezo sita iliyocheza.
Ushindani bado unaendelea
Licha ya kupoteza mchezo wa kwanza, bado Comoros inayo nafasi ya kufanya vizuri katika michezo yake miwili iliyobakia ambayo itakabiriana na Zambia, Desemba 26 kabla ya kuvaana na Mali, Desemba 29 mwaka huu.