Duru moja ya habari nchini Marekani imefichua kuwa, meli ya mafuta iliyotekwa kiharamia na Marekani nje ya pwani ya Venezuela ni mali ya China si ya Venezuela.

Shirika la Habari la Mehr limenukuu mitandao ya habari ya Al-Mayadeen na Bloomberg News ikitangaza kwamba: Meli ambayo Marekani iliiteka kwenye maji ya karibu na pwani ya Venezuela ilikuwa ni meli kubwa ya mafuta yenye bendera ya Panama, ambayo mmiliki wake yuko nchini China.

Waziri wa Vita wa Marekani amedai kuwa, kuzuiwa meli za mafuta zilizowekewa vikwazo na Marekani kutaendelea. Waziri huyo wa Vita wa Marekani, Pete Hegsett pia amesema kuwa, Pentagon itaendelea kufanya operesheni za kukamata meli zilizowekewa vikwazo na Marekani.

Naye Waziri wa Usalama wa Ndani wa Marekani, Kristin Noem amethibitisha habari kuwa, walinzi wa fukwe za Marekani kwa kusaidiana na Wizara ya Vita ya nchi hiyo Pentagon, waliiteka nyara meli ya mafuta ambayo ilitia nanga mara ya mwisho nchini Venezuela siku ya Jumamosi.

Serikali ya Venezuela inautaja uhalifu huo wa Marekani kuwa ni uharamia na kusisitiza kuwa, Caracas ina haki zote za kulipiza kisasi na kujihami mbele ya jinai hizo za Marekani. 

Uthibitisho wa kutekwa nyara kiharamia meli ya mafuta nje ya pwani ya Venezuela umekuja saa chache baada ya maafisa watatu wa Marekani kuiambia Reuters kwamba Washington ilikuwa kwenye operesheni ya kuteka meli nje ya pwani ya Venezuela.

Katika ripoti nyingine, Reuters imesema kuwa hiyo ni miongoni mwa meli ambazo Marekani imeziwekea vikwazo kwa upande mmoja na sasa inatekeleza sheria za Marekani dhidi ya meli hizo kwenye maji ya kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *