
Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesifu “kuongezeka kwa uwepo wa Iran baharini” nje ya eneo la Asia Magharibi, akitangaza kwamba meli kadhaa za kivita za jeshi hilo zinaelekea Afrika Kusini.
Akizungumza katika mkutano wa maulamaa ulioandaliwa na Jeshi la Majini Jumapili, Admeri Shahram Irani alisema Jamhuri ya Kiislamu ni miongoni mwa wachangiaji wakuu wa usalama wa baharini katika eneo na kwingineko.
Ameongeza kwamba kutumwa kwa vikosi hivyo kunadhihirisha utegemezi unaokua wa jeshi hilo kwa uwezo wa ndani, uzoefu wa kiutendaji wa kuvuka maeneo, na uwepo endelevu katika maji ya wazi.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, moja ya vikosi hivyo limepewa jukumu la kusindikiza meli za kibiashara, huku Kikosikazi cha 103 kikitarajiwa kushiriki katika mazoezi ya pamoja ya majini na nchi wanachama wa BRICS. Nchi hizo ni pamoja na Brazil, Russia, India, China, Afrika Kusini, Argentina, Misri, Ethiopia, Iran, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu
Admeri Irani amesema kuwa ushiriki huo unafuata maelekezo ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei na unalenga kuimarisha ulinzi na diplomasia ya baharini.
Aidha, aliongeza kuwa nafasi ya Iran katika nyanja za baharini imejengeka kwa uthabiti, na Jeshi la Majini limekuwa “miongoni mwa wahusika wenye ushawishi katika usalama wa baharini ndani ya eneo na nje yake.”
Kamanda huyo alikosoa juhudi za vyombo vya habari vinavyopinga Iran kwa kujaribu kuonyesha Iran kama lililotengwa, akisema kwamba majaribio hayo yameshindwa hapo awali na yataendelea kushindwa.
Katika maelezo mengine, alibainisha kuwa makamanda wa kijeshi wa kigeni wanakiri kuhusu nafasi na ushawishi wa uongozi wa Iran. Alifafanua kwamba kauli za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu huchunguzwa katika ngazi za juu za kijeshi nje ya nchi, jambo linaloonyesha athari ya Iran katika matukio ya kikanda na kimataifa.