Bado hakuna tarehe thabiti ya uchaguzi iliyotangazwa; katiba ya mpito inapendekeza angalau mwaka wa utawala unaoongozwa na jeshi kabla ya kurudi tena kwa uchaguzi wa kiraia, lakini ratiba hii inapingwa na mashirika ya kiraia na makundi ya kisiasa.
Mnamo Oktoba 2025, huku kukiwa na maandamano makubwa yaliyoongozwa na vijana dhidi ya ufisadi, ukosefu wa ajira na huduma duni, kitengo cha jeshi kinachojulikana kama CAPSAT kilijitenga na kutangaza kuchukua udhibiti wa nchi.
Rais wa wakati huo, Andry Rajoelina, alikimbia nchi na kushtakiwa na wabunge. Viongozi wa kijeshi walitangaza mapinduzi na kumtaja Kanali Michael Randrianirina kuwa kiongozi mpya.
Madagascar imekuwa na vipindi vya machafuko ya kisiasa na uchaguzi uliopingwa hapo awali, lakini udhibiti kamili wa kijeshi haukuwa kitu cha kawaida. Unyakuzi wa 2025 unafuatia miezi ya kuongezeka kwa mfadhaiko wa umma na kuvunjika kwa imani na serikali yao.
Hali ya hivi punde Madagascar
Mtawala mpya wa kijeshi amesimamisha taasisi kuu za kisiasa, zikiwemo katiba na vyombo vya uchaguzi.
Awali serikali ilikadiria uchaguzi ndani ya miezi 18 hadi miaka miwili, lakini hili bado limegubikwa na utata.
Harakati sambamba za kurejesha utawala wa kiraia zinaongezeka miongoni mwa makundi ya upinzani.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, uchaguzi unatarajiwa mapema zaidi ya katikati ya 2027 ikiwa jeshi litaweka ratiba yake iliyotangazwa. Hata hivyo, hakuna ramani inayotambulika kimataifa ya kurudi katika utawala wa kiraia.
Mali – Jaribio la mapinduzi lililotibuka (Agosti 2025)
Mamlaka nchini Mali iliwakamata maafisa wa kijeshi na raia wanaotuhumiwa kupanga njama dhidi ya utawala wa kijeshi wa Mali. Haya yanajiri huku nchi hiyo ikisalia chini ya udhibiti wa kijeshi kufuatia mapinduzi ya mwaka 2020 na 2021.
Uchaguzi wa urais ulipangwa kufanyika nchini Mali tarehe 27 Februari 2022, kufuatia mapinduzi ya 2021. Baada ya kuahirishwa, mnamo Julai 2022 uchaguzi uliratibiwa upya hadi tarehe 4 Februari 2024. Mnamo Septemba 2023, uongozi wa kijeshi ulisema kwamba uchaguzi “utaahirishwa kidogo kwa sababu za kiufundi,” bila kutoa tarehe mpya.
Burkina Faso – Jaribio la mapinduzi lililotibuka (Aprili 2025)
Serikali ya kijeshi inayotawala iliripoti kwamba ilizuia mapinduzi yaliyopangwa, ambayo yanadaiwa kuhusisha askari wa sasa na wa zamani wenye uhusiano wa nje.
Uchaguzi uliokusudiwa kurejesha serikali ya kiraia ya kidemokrasia nchini Burkina Faso mnamo Julai 2024 haukupewa “kipaumbele” na uliahirishwa kwa muda usiojulikana na utawala wa kijeshi unaoongozwa na Kapteni Ibrahim Traoré tangu alipochukua madaraka kwa nguvu Septemba 2023.
Katika maeneo ya Afrika Magharibi na Kati, mapinduzi ya hivi karibuni na majaribio ya mapinduzi yameibua wasiwasi kuhusu utaratibu wa kikatiba. ECOWAS imetangaza hali ya hatari ya kikanda ili kukabiliana na “wimbi hili la mapinduzi” na kuahidi hatua iliyoratibiwa ili kuhifadhi utawala wa kikatiba.
Msururu huu wa mapinduzi na majaribio ya mapinduzi wakati mwingine hujulikana kama “Ukanda wa Mapinduzi ya Afrika,” kuonyesha jinsi mapinduzi ya kijeshi yalivyojikita katika eneo hilo huku kukiwa na taasisi dhaifu, matatizo ya kiuchumi, na mgawanyiko wa kisiasa.
Muungano wa Afrika AU umeendelea kukemea hatua zozote za mapinduzi ya kijeshi. Mashirika na taasisi za kikanda na bara zima limetumia diplomasia na upatanishi ili kuzuia kuzorota kwa hali ya usalama.