Mwigulu aja kivingine ukaguzi miradiMwigulu aja kivingine ukaguzi miradi

WAZIRI Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ameagiza wakuu wa mikoa wote wapewe wataalamu watakaokagua miradi ya majengo kwa kutumia vifaa maalumu ili kuthibitisha kama imefanyika kwa usahihi. Dk Mwigulu ametoa agizo hilo kwa nyakati tofauti alipotembelea Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea na Chuo cha Uuguzi na Ukunga wilayani humo, Mkoa wa Lindi.

Mwigulu yupo kwenye ziara ya kikazi ya kukagua miradi inayoendelea kujengwa nchini na kuagiza utumike utaalamu kama uliotumika wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru. “Nikiwa kwenye gari nimeambiwa yule mtaalamu aliyekuwa kwenye mbio za Mwenge anaitwa Azizi, yupo Pwani… Naagiza wakuu wa mikoa wote kila mkoa uwe na seti ya wataalamu wa aina hiyo na kwa vile muda wa bajeti haujafika bado, basi wakuu wa mikoa kama hawana hivyo vifaa hilo liwekwe kwenye mikakati ya kununua vifaa vinavyohitajika,” alisema.

Amesema ukaguzi huo wa kitaalamu utasaidia kubaini kama kuna udanganyifu uliofanyika wakati wa ujenzi wa majengo husika na kuchukua hatua. “Wataalamu wakipita wanapima wanaona kama vipimo vipo sahihi… na katibu wangu, hebu niletewe yule kijana wa mbio za Mwenge nizunguke naye, yeye awe anatangulia kufanya vipimo tukifika anatuambia,” alisema.

Amesema ni vigumu kukagua jengo lililokwishajengwa na kupakwa rangi na kugundua makosa isipokuwa kwa kutumia vifaa maalumu vya kitaalamu inakuwa rahisi. “Tutaweza kugundua kama hapa zilitakiwa nondo sita lakini zimewekwa nne. Nyie mnakagua nje mnaona sawa, mnauziwa mbuzi kwenye gunia. Nakuagiza Naibu Waziri wa Tamisemi, Reuben Kwagilwa waandikieni barua wakuu wa mikoa wote kuhakikisha kila mkoa una vifaa na wataalamu wa kukagua majengo hayo,” alisema.

Aidha, waziri mkuu alikumbushia agizo lake la kupitiwa kwa miradi yote ili kujua kama thamani ya fedha iliyotolewa inalingana na kazi iliyotekelezwa. Ameagiza Wizara ya Afya kupitia Naibu Waziri wake, Dk Florence Samizi kuhakikisha hospitali zote zinaweka utaratibu wa kuwahudumia wagonjwa kwa haraka badala ya kuwaweka muda mrefu bila matibabu.

Ametoa agizo hilo alipokagua Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea na kukuta baadhi ya wagonjwa wakisubiri matibabu. “Watu tunaamini hospitali, mtu anaumwa anakuja hospitali lakini anatakiwa kusubiri daktari kwa muda mrefu. Natoa agizo hospitali zote ziweke utaratibu mzuri wa kuhudumia wagonjwa haraka,” alisema.

Agizo lingine alilolitoa kwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack ni kuhakikisha mradi wa barabara wa Somanga unakamilika haraka kabla mvua hazijaanza ili miundombinu isiharibike. Pia aliwatoa wasiwasi wananchi kwa kusema Rais Samia Suluhu Hassan atatekeleza miradi yote aliyoahidi katika Ilani ya Uchaguzi na iliyo kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesisitiza nidhamu kazini na kuheshimu sekta binafsi ili kukuza uchumi wa taifa na kutimiza ahadi za maendeleo. Aidha, aliwahimiza wananchi kuendelea kutunza amani na kuepuka chokochoko zinazoweza kusababisha maafa. SOMA: Dk Mwigulu akagua maendeleo ujenzi madaraja Lindi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *