OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) imesema itaendelea kushirikisha wadau wazielewe ripoti za ukaguzi na kuchangia katika kuimarisha uwajibikaji wa matumizi ya rasilimali za umma. Mchumi Mwandamizi wa NAOT, Emanuel Lazaro amesema hayo alipowasilisha mada kuhusu njia na aina za ukaguzi wakati wa mafunzo ya ukaguzi kwa waandishi wa habari mkoani Morogoro .
Lazaro amesema watu wenye ulemavu wa uoni hafifu wanahitaji ripoti zilizopo kwenye karatasi za nukta nundu na kwamba ofisi hiyo imejielekeza huko kwa kuandaa ripoti ambazo ni za nukta nundu. SOMA: TET yatoa elimu matumizi ya vitabu vya nukta nundu
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere; Mkaguzi Mkuu wa Nje Mkoa wa Morogoro, Baraka Mfugale amesema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi.
Mfugale amesema mpango huo unalenga kuimarisha ushirikishaji wadau, hususan vyombo vya habari, katika mchakato wa uwajibikaji wa matumizi ya rasilimali za umma. Mfugale amesema ofisi hiyo imejipanga kuendelea kuboresha uwazi katika utoaji wa taarifa za ukaguzi, kuimarisha mawasiliano na wadau, na kujenga uelewa mpana kuhusu kazi, majukumu na mipaka yake.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Ofisi hiyo, Focus Mauki amesema, ofisi inaamini mafunzo hayo yatawajengea uwezo zaidi wa kuuliza maswali ya kitaalamu, kufanya uchambuzi wa kina na kuibua mijadala chanya inayosaidia serikali, bunge na taasisi nyingine kuchukua hatua stahiki kulingana na mapendekezo ya ukaguzi.
