
Mkutano wa dharura kuhusu mgogoro wa mashariki mwa Kongo ulioongozwa na Rais wa Uganda Yoweri Museveni ulimalizika hapo jana Jumapili kwenye ikulu ya mjini Entebe.
Wajumbe kutoka mataifa 12 wa nchi wanachama kwenye kongamano la kimataifa kuhusu Kanda ya maziwa makuu walihudhuria mkutano huo ulioitishwa kujadili kwa undani umuhimu wa mataifa hayo ya Afrika kutoachwa nyuma katika kutafuta suluhu kwa mgogoro huo.
Pande zote mbili katika mzozo huo yaani Rwanda na jamhuri ya kidemorkasia ya Congo zilizojumuisha maafisa wa ngazi za juu walitoa mapendekezo yao ya kuwezesha kusitishwa kwa vita. Ila kila upande umendelea kulaumu mwingine kwa kutoheshimu mikataba mbalimbali inayolenga kutoa suluhu la kudumu kuhusu mzozo kati yao.
Kiongozi wa ujumbe wa Rwanda waziri wa masuala ya kigeni na ushirikiano wa kimataifa Vincent Biruta ametoa msimamo wa Rwanda akisema kuwa suluhu kwa mzozo huo litapatikana tu ikiwa chanzo cha mzozo huo ambacho ni DRC kuunga mkono waasi wa FDRL kitashughulikiwa ipasavyo.
Rais Felix Tshisekedi aliyehutubia mkutano huo kwa kupitia mtandaoni aliliezea masikitiko yake kwamba mikataba mbalimbali ikiwemo ile ya Nairobi Doha na Washington haijaheshimiwa na Rwanda na waasi wa M23. Ameyataka mataifa ya kanda kuhakikisha kuwa yanashiriki moja kwa moja katika kutatua mzozo huo badala kuyaachia mataifa ya kigeni kama Marekani na Qatar. Akitoa angalizo kuwa wageni hawawezi kujitokeza na suluhu la kudumu kuhusu mgogoro huo ambapo nchi hiyo inailaumu Rwanda kwa kuunga mkono M23, madai ambayo utawala wa Kigali umendelea kukanusha vikali.
Ijapokuwa maafikiano ya kilele ya mkutano huo hayakutolewa mara moja ambapo wakati ukiendelea wanahabari hawakuruhusiwa kuhudhuria, waziri wa nchi wa masuala ya kigeni wa Uganda John Mulimba amefahamisha kuwa walikubaliana kuendeleza mchakato wa Jumuiya ya Kiuchumi za Afrika Mashariki na Afrika ya Kusini SADC sambamba na ile iliyotokana na mikataba ya Doha na Washington.
Licha ya mikataba ya Doha na Washington kusainiwa hivi karibuni ikihusisha Rwanda DRC na hata kwa kiwango fulani M23, hali inazidi kuwa mbaya maeneo ya Mashariki mwa Congo hususan eneo la Uvira. Shirika la Umoja Mataifa linaloshughulikia wakimbizi UNHCR limetoa mwito ya misaada kwa idadi kubwa ya wakimbizi wanaongia Burundi wakikimbilia usalama wao.