Katika bustani ya Hoteli ya Serena mjini Goma, wanamitindo walitembea kwenye jukwaa wakionyesha mavazi ya kifahari ya jioni pamoja na mitindo ya kisasa iliyoongozwa na mavazi ya jadi ya Kiafrika. Tukio hilo ni la nne la Wiki ya Mitindo ya Kivu, iliyoanzishwa mwaka 2022 na mbunifu wa Kongo, Voyance Batinda.
Maonesho haya ya mitindo yanafanyika katika mji ambao miezi michache iliyopita ulikuwa kitovu cha mapigano, baada ya waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda kuuteka mji wa Goma. Hali ya usalama mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo bado ni tete, licha ya makubaliano ya amani yaliyoratibiwa na Marekani mapema mwezi huu.
Siku chache zilizopita, waasi wa M23 waliteka mji mwingine mashariki mwa Kongo katika mashambulizi yaliyosababisha vifo vya raia. Hata hivyo, waandaaji wa Wiki ya Mitindo ya Kivu wanasema ni muhimu kuendelea na tukio hilo kama ishara ya matumaini na mshikamano.
Voyance Batinda, mwanzilishi wa Wiki ya Mitindo ya Kivu, anasema lengo la mwaka huu ni kuwaleta pamoja watu wa mataifa mbalimbali, hasa kutoka ukanda wa Afrika Mashariki.
“Lengo la maonyesho haya ya nne nne lilikuwa kuzileta pamoja jamii mbalimbali, hasa za mashariki. Ndiyo maana tuliwaalika wageni kutoka Rwanda, Uganda na nchi nyingine. Tulitaka kuwasilisha ujumbe wa amani na kuishi pamoja kwa amani kimataifa.”
Maisha lazima yaendelee licha ya mgogoro uliopo
Mbunifu mwingine, Vainqueur Akilimali, naye anasema tukio hilo ni njia ya kuwakutanisha watu waliokumbwa na mateso ya vita kwa muda mrefu.
“Tulitaka kuwaleta pamoja watu hawa wote ambao wameathiriwa kwa muda mrefu na vita, katika roho ya ustahimilivu, matumaini na mshikamano.”
Zaidi ya makundi 100 yenye silaha yanapigania udhibiti wa rasilimali mashariki mwa Kongo, eneo lenye utajiri mkubwa wa madini. Mgogoro huo umeendelea kwa zaidi ya miongo mitatu na umetajwa kuwa miongoni mwa majanga makubwa zaidi ya kibinadamu duniani, ukisababisha vifo vya zaidi ya watu milioni sita.
Licha ya hayo, wasanii na wakazi wa Goma wanasema maisha lazima yaendelee. Mwimbaji wa Kongo, Dety Darba, ambaye alihudhuria maonesho hayo, anasema ni muhimu kuonesha kuwa maisha hayajasimama licha ya vita.
“Nadhani hii ni njia nyingine ya kulaani kinachoendelea, na kuonesha kuwa kinachotokea nchini kwetu siyo mabaya tu. Zaidi ya vita, tunaishi, tunaumba, tuna ustahimilivu na tunajaribu kusonga mbele kadri tuwezavyo.”
Wiki ya Mitindo ya Kivu inabaki kuwa jukwaa la sanaa, matumaini na mshikamano, ikitoa ujumbe kwamba hata katikati ya vita na machungu, amani na ubunifu vinaweza kuota.