Kocha wa zamani wa Bafana Bafana, Pitso Mosimane, amesema soka la Afrika ni la tofauti na kwamba majina makubwa katika orodha ya wachezaji hayana maana kubwa inapofika wakati mgumu wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.
Mosimane ni mmoja ya makocha waliofanikiwa zaidi katika historia ya soka la Afrika Kusini, ingawa kipindi chake akiwa na Bafana Bafana haikufuzu AFCON, ni wachache sana wanaojua soka la bara hili vizuri kuliko kocha huyo wa zamani wa Mamelodi Sundowns na Al Ahly.
Kocha huyo mwenye mafanikio makubwa Afrika alisema anaamini kuwa Bafana ina nafasi sawa na timu yoyote katika fainali za 2025 zitakazofanyika Morocco, wanapojiandaa kuikabili Angola katika mechi yao ya ufunguzi Jumatatu.
“(Kocha mkuu) Hugo Broos, Helman Mkhalele na benchi zima la ufundi wamefanya kazi nzuri sana katika kuunda timu hii. Wamefanya mambo kwa usahihi,” Mosimane aliandika katika safu yake ya News24.
“Hiyo ndio sababu timu hii haishiriki tu AFCON mfululizo, bali pia ilimaliza nafasi ya tatu katika mashindano yaliyopita na mwaka ujao tunaenda Kombe la Dunia.
“Timu imekuwa na uwiano mzuri kwa sababu wana uwezo wa kubadilisha mtindo wa mchezo wao, ikiwemo kuwa na nguvu za kimwili pale inapohitajika. Tunapaswa kuzipongeza klabu za Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL) kwa sababu zimewekeza sana kwenye sayansi ya michezo na maandalizi ya kimwili ya wachezaji.
“Haya yote, pamoja na Bafana kuimarisha benchi lao la ufundi kwa wachambuzi na wanasayansi wa michezo zaidi, yanawaweka katika nafasi nzuri.”
Mosimane anaamini kikosi cha sasa kina ubora wa kutosha kwenda hadi mwisho, hata kama si timu inayotajwa kuwa lainilaini.
“Ninaamini kuwa Bafana Bafana wana uwezo wa kushinda Kombe la Mataifa ya Afrika. Nasema hivyo kwa sababu walimaliza nafasi ya tatu katika AFCON iliyopita. Wamejiwekea kiwango cha juu sana, na wanaweza tu kuboresha zaidi kutoka hapo.
“Baada ya kufika nusu fainali kwenye AFCON iliyopita, watataka kwenda hatua moja mbele zaidi na kufika fainali, na ukiwa kwenye fainali, ni bora kabisa ushinde kombe.
“Bafana si kama washindani wengine wakubwa, na tofauti hiyo inaweza kufanya kazi kwa faida yao.
“Macho ya bara zima yako katika timu kama Ivory Coast, Misri, Nigeria, Senegal na bila shaka Morocco. Timu hizi zina wachezaji wanaocheza katika ligi bora kabisa duniani.
“Bafana hawana hilo; hawana sifa ya kuwa ‘timu ya nyota’. Tuna Lyle Foster pekee anayekipiga England, lakini hakuna wachezaji wengine katika ligi kubwa za Ulaya kama Ligue 1, La Liga, Bundesliga au Serie A.
“Kikosi chetu kinaundwa zaidi na wachezaji wa PSL. Lakini si rahisi kukabiliana na timu za PSL.”
Mosimane anasema mtindo wa uchezaji wa Bafana, ambao ni wa kipekee kwa kiasi kikubwa barani Afrika, unawafanya kuwa timu ngumu kwa wapinzani wote.
“Faida yetu kubwa ni kwamba sisi ni tofauti. Tunacheza soka kwa namna tofauti na timu za kaskazini na hata magharibi mwa Afrika. Mchezo wetu wa pasi fupi ni silaha yetu kubwa. Unawaingia kwenye mishipa ya wapinzani,” alisema.
“Soka la Afrika ni mnyama tofauti. Huwezi tu kuangalia makaratasi na kusema huyu atashinda.
“Lazima mucheze kwa ajili ya wenzenu. Lazima muwe na njaa ya ushindi. Msitishwe na majina yaliyo katika orodha ya timu, kwa sababu ukitazama majina ya timu kama Mali, kwa mfano, utaanza kutokwa na jasho hata kabla ya mchezo kuanza.”