
Rais Masoud Pezeshkian ameeulezea ushirikiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Umoja wa Kiuchumi wa Ulaya na Asia EAEU kama mkakati wa muda mrefu wa kuimarisha mamlaka ya kitaifa ya kujitawala na kuanzisha kitovu cha nguvu ya kikanda.
Rais wa Iran ameyasema hayo katika ujumbe wake kwa Baraza Kuu la Umoja wa Kiuchumi wa Ulaya na Asia (EAEU), ambao ulisomwa jana Jumapili na Balozi wa Iran nchini Russia, Kazem Jalali, katika mkutano wa baraza hilo uliofanyika mjini St. Petersburg, Russia.
Mkutano huo wa ngazi ya juu umehudhuriwa na marais wa Russia, Belarus, Kazakhstan, Kyrgyzstan, na Waziri Mkuu wa Armenia, ukiashiria lahadha muhimu iliyofikiwa katika upanuzi wa kambi hiyo ya kiuchumi.
Rais Pezeshkian amesisitiza kuwa Iran inajitahidi kuanzisha kigezo kilichofanikiwa cha muunganiko wa kikanda kwa kuzingatia masuala ya pamoja ya kiutamaduni na kihistoria.
“Mustakabali mwema ni wa mataifa yanayofungua njia ya maendeleo kupitia ushirikiano na kuaminiana kati ya pande zote,” ameeleza Rais Pezeshkian.
Rais wa Iran amebainisha maeneo kadhaa muhimu ya ushirikiano wa kimkakati, ikiwa ni pamoja na uwezeshaji wa biashara na usafiri, usalama wa nishati na maendeleo ya teknolojia, miundombinu ya kifedha, na uhusiano wa baina ya watu na watu.
Pezeshkian amebainisha kuwa licha ya Iran kuwa ni mwanachama hai wa mashirika kadhaa ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na BRICS, Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO), na ECO, lakini EAEU ina nafasi ya kipekee katika sera ya nje ya Iran.
Ameuelezea utekelezaji wa Mkataba wa Biashara Huria kati ya Iran na kambi hiyo ulioanza mwezi Mei kama mwanzo wa ushiriki wenye tija katika eneo hili muhimu la kijiografia.
Kwa mujibu wa Rais Pezeshkian, uwezo halisi wa ushirikiano wa kibiashara kati ya Iran na nchi tano wanachama wa EAEU ni mkubwa zaidi kuliko viwango vilivyofikiwa kwa sasa, na kwamba Tehran imejitolea kwa dhati kupiga zaidi “hatua ya kibiashara” ambayo itapelekea kuwepo ongezeko kubwa zaidi la viwango hivyo katika miaka ijayo…/