Rwanda imefunga zaidi ya makanisa 10,000 ya kiinjilisti kwa kushindwa kufuata sheria ya mwaka 2018 iliyoanzishwa kwa ajili ya kusimamia maeneo ya ibada.
Sheria hiyo imeainisha kanuni mpya kuhusu afya, usalama na uwazi katika masuala ya kifedha na inawataka wahubiri wote kuwa wamepata mafunzo ya theolojia.
Rais Paul Kagame wa Rwanda amekuwa akiyakosoa makanisa hayo ya kiinjili ambayo yameibuka katika nchi hiyo ndogo ya eneo la Maziwa Makuu barani Afrika.
“Kama ingekuwa juu yangu, nisingefungua tena hata kanisa moja,” Kagame alisema katika kikao cha waandishi wa habari mwezi uliopita. Katika kikao hicho, Rais Kagame aliuliza: “Katika changamoto zote za maendeleo tunazokabiliana nazo, yaani vita na ustawi wa nchi yetu, ni ipi nafasi ya makanisa haya? Je, yanatoa ajira? Mengi ni wezi tu; makanisa mengine ni pango la majambazi tu.”

Inafaa kuashiria hapa kuwa, idadi kubwa ya Wanyarwanda ni Wakristo. Hii ni kwa mujibu wa sensa ya mwaka jana.
Sheria hiyo ya kusimamia makanisa nchini Rwanda ya mwaka 2018 inayataka kila mwaka kuwasilisha mipango yao ya utekelezaji inayoweka wazi namna yanavyofungamana na thamani za kitaifa.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, michango yote inapasa kupitia katika akaunti zilizosajiliwa.
Mchungaji Sam Rugira, ambaye matawi mawili ya kanisa lake yalifungwa mwaka jana huko Rwanda kwa kushindwa kutimiza kanuni za usalama wa moto, amesema sheria hizo zinaathiri zaidi makanisa mapya ya kiinjili ambayo “yameibuka katika miaka ya hivi karibuni.