
Serikali ya Rwanda imeyafunga zaidi ya makanisa 10,000 ya kiinjili nchini humo baada ya kushindwa kufuata sheria ya mwaka 2018 iliyowekwa kudhibiti maeneo ya ibada.
Rwanda ilianzisha sheria mpya kuhusu afya, usalama na ufichuzi wa kifedha na inawataka wahubiri wote kuwa na mafunzo ya kitheolojia.
Rais Paul Kagame ameendelea kuwa na msimamo mkali dhidi ya makanisa hayo yanayokua kwa kasi katika nchi za ukanda wa Maziwa Makuu ya Afrika.
“Iwapo ingewezekana, nisingefungua kanisa hata moja,” alisema Kagame wakati akizungumza na waandishi wa habari mwezi uliopita.
“Kwenye changamoto zote za maendeleo tunazokabiliana nazo, vita, uhai wa nchi yetu, ni nafasi gani makanisa haya yanaichukulia? Wanaajiri watu? Wengi ni wizi tu; baadhi ya makanisa ni banda la wezi,” aliongeza.
Karibu Wanyarwanda wote ni Wakristo, kulingana na sensa ya mwaka 2024, na wengi sasa wanapaswa kusafiri umbali mrefu ili kupata sehemu za kusali. Sheria ya mwaka 2018 inataka makanisa yote yatume mipango ya mwaka ikieleza jinsi yanavyokidhi maadili ya taifa, huku michango yote ikitakiwa kupitiwa kwenye akaunti zilizosajiliwa.
Kwa upande wake, Askofu Sam Rugira, ambaye makanisa yake mawili yalifungwa mwaka jana kwa kushindwa kukidhi masharti ya usalama wa moto, alisema sheria hizo zinaathiri zaidi makanisa mapya ya kiinjili yaliyoanzishwa hivi karibuni.
Rais Kagame ameyataja makanisa hayo kama ‘kibaki cha ukoloni’ na kuongeza kuwa historia hiyo bado inaathiri nchi.