DAR ES SALAAM; Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Patrobas Katambi, amelitaka Baraza la Ushindani (FCT) kuendelea kulinda na kusimamia ushindani wa haki, ili kuondokana na vitendo vya ukiritimba, upangaji wa bei na makubaliano haramu katika shughuli za kibiashara, vinavyoweza kuathiri biashara na kuumiza walaji.
Ametoa agizo hilo leo Desemba 22, 2025 jijini Dar es Salaam, wakati wa ziara yake ya kikazi katika ofisi za FCT, ikiwa ni sehemu ya ukaguzi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa majukumu ya taasisi zilizo chini ya wizara hiyo.
Naibu Waziri alipata fursa ya kupata maelezo kuhusu majukumu ya FCT katika kusimamia na kulinda ushindani wa haki katika masoko ya ndani, ambapo alisisitiza FCT ina wajibu wa kuhakikisha walaji na watumiaji wa bidhaa na huduma wanalindwa ipasavyo, huku bei zikiwa za haki na bidhaa zinazotolewa zikiwa na ubora unaokubalika.
Ameipongeza FCT kwa juhudi zake za kuimarisha mazingira ya ushindani wa haki, hatua inayochochea uwekezaji na kuimarisha ustawi wa sekta ya viwanda na biashara nchini.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Mwenyekiti wa Baraza la Ushindani, Onesmo Kyauka, amesema baraza limejipanga vyema kusikiliza na kushughulikia mashauri yote kwa haraka, haki na kwa kuzingatia weledi.
Amesema baraza litafanya kazi bila upendeleo wala ushawishi wa aina yoyote, ili kuhakikisha haki inapatikana kwa pande zote.

Naye Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Audax Bahweitima, amesema upatikanaji wa haki katika masuala ya kibiashara ni chachu muhimu ya kukuza uchumi wa Taifa.
Amesema hali hiyo hujenga mazingira bora ya biashara, huongeza ushindani wenye tija na kuvutia uwekezaji kwa manufaa ya Taifa na wananchi kwa ujumla.