Tanroads Mbeya yaagizwa kumsimamia mkandarasiTanroads Mbeya yaagizwa kumsimamia mkandarasi

SERIKALI imemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mbeya amsimamie mkandarasi anayejenga barabara ya Katumba–Lupaso wilayani Rungwe ili ujenzi huo usisababishe kukatika mawasiliano kwa wananchi.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya ametoa agizo hilo  mwishoni mwa wiki wakati wa ziara kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami. SOMA: TANROADS Tabora yarejesha mawasiliano Bukumbi – Kahama

Mradi huo unalenga kuunganisha halmashauri za Busokelo na Rungwe na kuboresha usafiri katika ukanda huo. Barabara hiyo yenye urefu wa zaidi ya kilometa 35.3 inapita katika maeneo ya milimani hali inayosababisha maporomoko ya udongo mara kwa mara na kuifanya kujifunga, jambo linaloathiri mawasiliano na shughuli za kijamii na kiuchumi za wananchi wa Busokelo na maeneo ya jirani.

Kasekenya amewataka wasimamizi wa mradi huo kuhakikisha mkandarasi anatumia fedha alizolipwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo pekee, na si kuzihamishia kwenye miradi mingine, akibainisha kuwa tabia hiyo imekuwa ikichelewesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Meneja wa Tanroads Mkoa wa Mbeya, Suleiman Bishanga amesema barabara hiyo inajengwa kwa gharama ya Sh bilioni 54 na serikali imemlipa mkandarasi fedha za awali Sh bilioni 4.7. Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Jaffar Haniu alisema barabara hiyo ni sehemu ya mradi mkubwa wa Katumba– Lupaso–Mbambo–Tukuyu.

Amemtaka mkandarasi kuwa tayari kuirekebisha wakati wowote itakapojifunga, hasa ikizingatiwa kuwa mvua huanza Desemba na kuendelea hadi Julai.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *