JAMHURI ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kiarabu ya Misri zimekubaliana kushirikiana katika kukuza na kuendeleza utalii wa kitamaduni na mali kale kati ya nchi hizo mbili.
Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa kikao kati ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi, na Waziri wa Utalii na Mali Kale wa Misri, Sherif Fath Attia, kilichofanyika jijini Cairo tarehe 20 Desemba, 2025.
Katika mazungumzo hayo, Kabudi alimueleza mwenyeji wake kuwa Tanzania imejipanga kupanua wigo wa soko la utalii kwa kuibua fursa mpya, hususan katika maeneo ya mali kale, makumbusho na utalii wa kitamaduni. SOMA: Serikali, wadau kushirikiana kuboresha miundombinu utalii
“Kwa muda mrefu Tanzania imekuwa ikifanya vizuri katika utalii wa mbugani (Safari Tourism). Kwa sasa Serikali imejipanga kupanua soko la utalii kwa kuongeza nguvu katika utalii wa kitamaduni na mali kale,” alifafanua Mhe. Kabudi.
Kwa upande wake, Attia alisema Serikali ya Misri iko tayari kutoa ujuzi na wataalamu waliobobea katika masuala ya mali kale na makumbusho kwa ajili ya kuwajengea uwezo wataalamu wa Tanzania.

“Nchi ya Misri ina wataalamu wenye uzoefu mkubwa katika masuala ya mali kale, ujenzi, usimamizi na uendeshaji wa makumbusho pamoja na utalii wa kitamaduni. Tupo tayari kuwaleta wataalamu hao nchini Tanzania kutoa mafunzo, na pia wataalamu wa Tanzania watapata fursa ya kuja Misri kujifunza,” alisisitiza Mhe. Attia.
Aidha, alisema Wizara ya Utalii na Mali Kale ya Misri itaratibu jukwaa maalum la wawekezaji litakalowakutanisha wataalamu na wadau wa utalii kutoka Tanzania kwa lengo la kutangaza na kujadili fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya utalii nchini Tanzania.
Katika ziara hiyo, Kabudi aliambatana na James Maziku, Mkurugenzi wa Uwekezaji kutoka TISEZA, Nasriya Nassor, Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Misri, pamoja na maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.