Hujambo mpenzi mskilizaji na karibu tuangazie baadhi ya matukio makubwa ya spoti yaliyoshuhudiwa ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbali mbali za dunia ukiwemo ufunguzi wa michuano ya AFCON 2025 nchini Morocco.

Kombe la Hazfi; Miamba yatinga robo fainali

Klabu za soka za Malavan na Foolad zimefanikiwa kutinga robo fainali ya michuano ya Kombe la Hazfi (Muondoano) ya Iran. Malavan iliigaragaza Mes Shar-e Babk mabao 3-0 mjini Bandar Anzali katika mchuano wa kukata na shoka uliopigwa Jumamosi. Mes ilipoteza kwa Gol Gohar kwa mabao 4-1 kupitia mikwaju ya penalti, baada ya mechi kumalizika kwa sare tasa. Havadar na Saipa ziliambulia sare ya mabao 2-2 katika muda wa kawaida, huku Saipa ikishinda mechi hiyo kwa mikwaju ya penalti kwa mabao 7-6. Aidha Jumamosi hiyo, Foolad aliitandika Chadormalou mabao 2-0, kupitia mabao ya Mohammadreza Soleymani na Abolfazl Zadeh Attar dakika ya 51 na 90 huko Ahvaz. Mchuano uliosisimua zaidi hata hivyo ni ule wa Alkhamisi, ambapo klabu ya Teractor Sazi (Watengeneza matrekta) ilipoishinda Persepolis mabao 8-7 kwenye mikwaju ya penalti katika mechi ya Raundi ya 32 ya Kombe la Hazfi la Iran kwa msimu huu wa 2025/26. Mechi hiyo ilimalizika kwa sare ya bao 1-1 katika muda wa kawaida, lakini hakuna timu iliyoweza kuona lango katika muda wa ziada.

Katika mechi hiyo iliyofanyika katika Uwanja wa Yadegar-e Emam mjini Tabriz, Mehdi Torabi aliifungia Teractor bao dakika ya 56 lakini beki wa Persepolis, Hossein Kananizadegan alisawazisha bao hilo kwa kichwa katika dakika za mwisho za mechi. Teractor itacheza na Shams Azar kusaka baraka za kusonga mbele. Baada ya dakika 120 zenye mvutano, mechi hiyo iliisha 1-1, na Tractor hatimaye ikashinda kwa penalti. Pamoja na kuwa ilikuwa mechi ya kusisimua, lakini ilishuhudia mihemko na vuta nikuvute si haba. Sepahan imeshindwa kutinga robo fainali ya Kombe la Hazfi baada ya kuchanbangwa mabao 3-1 na Kheybar katika Uwanja wa Naghsh-e Jahan siku ya Jumapili. Mohsen Sefid Choghaei alianza kufunga bao kwa timu hiyo ya wageni dakika tano tu baada ya mechi kuanza, lakini Mohammad Askari alisawazisha dakika ya 15. Ali Khanzadi aliiweka Kheybar mbele dakika ya 47. Kiungo wa kati wa Sepahan Omid Nourafkan alipata nafasi ya kusawazisha bao kwa penalti dakika ya 65 lakini alikosa, huku penalti yake ikiokolewa. Amirhossein Farsi alifunga matokeo kwa bao la tatu kwa Kheybar dakika ya 74.

Kwingineko, Paykan iliizaba Naft bao 1 la uchungu bila jibu, kutokana na bao la dakika za mwisho kutoka kwa Mehdi Najafi. Esteghlal ndio mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Soka ya Iran. Kabla ya hapo, Zob Ahan ililazimishwa sare ya bila kufungana na Shams Azar katika mechi ya 14 ya Ligi Kuu ya Iran ‘Persian Gulf Pro League (PGPL) kwa msimu wa 2025/26 Jumatano. Zob Ahan ilishindwa kutumia fursa ya uenyeji na kubaki katika nafasi ya 11 katika jedwali la timu 16, pointi mbili juu ya eneo la kushushwa daraja. Shams Azar pia iko katika nafasi ya 15 katika jedwali. Sepahan inaongoza jedwali ikiwa na pointi 27 na mchezo mmoja mkononi.

Sataranji: Watoto wa Kiirani wang’ara

Ramtin Kakavand na Rosha Akbari kutoka Iran walishinda medali mbili za dhahabu katika Mashindano ya Dunia ya Sataranji safu ya Rapid na Blitz kwa vijana wenye chini ya miaka 9 na 17 kwa usanjari huo. Kakavand alishinda medali ya dhahabu kwenye pambano la wazi la vijana kiumewenye chini ya miaka 13, akizoa pointi nane kati ya michezo tisa, na Akbari akaibuka wa kwanza kwa pointi 7.5 kutokana na michezo tisa safu ya watoto wa kike wenye chini miaka 15.

Mtoto wa Kiirani aimakinika kwenye mchezo wa chesi

Mashindano hayo yalifanyika Antalya, Uturuki, kuanzia Desemba 15 hadi 21. Wanasataranji wapatao 310, wakiwemo wachezaji 98 watajika na washikilizi wa tuzo ya kifahari ya Grandmasters 2, walikuwa wamesajili tukio la Blitz.

Muirani ateuliwa uongozi handiboli Asia

Shirikisho la Handiboli la Asia (AHF) limetangaza kuwa Alireza Pakdel, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Mikono la Iran, alichaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa AHF kwa muhula wa 2025-2029. Wakati wa Kongamano la 25 la Shirikisho la Mpira wa Mikono la Asia, lililofanyika Misri siku ya Jumamosi, Pakdel alichaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa AHF. Mbali na uchaguzi wa Pakdel, kongamano hilo pia lilifanya uchaguzi wa rais, makamu wa rais, na wajumbe wa kamati kuu ya AHF. Bader Mohammed Al-Theyab alichaguliwa rasmi kuwa Rais wa AHF kwa miaka minne ijayo.

 

AFCON yaanza kurindima Morocco

Duru ya 35 ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON iling’oa nanga Jumapili kwa mchuano wa kusisimua kati ya mwenyeji Morocco dhidi ya Comoro (Kisiwa cha Ngazija). Bao la ufunguzi la Brahim Diaz na mpira wa kuvutia wa Ayoub El Kaabi uliopigwa juu ya kichwa uliwafanya wenyeji Kombe la Mataifa ya Afrika Morocco kuwashinda Comoros 2-0 katika mchezo wa ufunguzi wa mashindano Jumapili, huku timu zinazopigiwa upatu kushinda zikitimiza wajibu wao licha ya kutofurahia mchezo wa marudiano ambao baadhi ya watu walitarajia. Soufiane Rahimi aliokoa penalti yake katika kipindi cha kwanza kabla ya Diaz, ambaye alikuwa mfungaji bora wakati wa kampeni ya kufuzu, kumaliza akiwa karibu na goli katika dakika ya 55 kufuatia krosi kutoka kwa Noussair Mazraoui na kuwasaidia Atlas Lions hatimaye kuwashinda wachezaji watatu. Dakika 20 baadaye, mchezaji wa akiba El Kaabi aliongeza bao la pili, akipiga mpira mbele ya lango na kutuma mpira uliopigwa kwa Anass Salah-Eddine na kutuma mpira wa juu zaidi ya Yannick Pandor bora katika lango la Comoro ili kuhakikisha ushindi.

Timu 24 zinazoshiriki michuano ya Afcon 2025

Timu zingine mbili za Kundi A — Mali na Zambia — zimeanza kampeni yao mjini Casablanca Jumatatu, huku Morocco ikitarajiwa kukabiliana na Mali mjini Rabat Desembe 26, ambapo mwenyeji anatazamiwa kusonga mbele hadi hatua ya mtoano. Comoros watatafuta pointi zao za kwanza ubaoni dhidi ya Zambia mjini Casablanca tarehe 26.

Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limetangaza rasmi muundo wa zawadi za fedha kwa ajili ya Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, itakayofanyika nchini Morocco na kushirikisha mataifa 24 kutoka barani Afrika. Kwa mujibu wa muundo huo mpya, bingwa wa AFCON 2025 atajinyakulia kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 7. Mshindi wa pili atapokea Dola Milioni 4. Timu zitakazofanikiwa kufuzu hatua ya nusu fainali zitapokea Dola Milioni 2.5 kila moja, huku zile zitakazofika robo fainali zikipata Dola Milioni 1.3 kila timu. Kwa upande wa timu zitakazomaliza safari yao katika hatua ya raundi ya 16, CAF imetenga zawadi ya Dola 800,000 kwa kila timu, sawa na takribani Shilingi Bilioni 1.98 za Tanzania. Hali kadhalika, Shirikisho la Soka la Afrika lilisema Jumamosi kuwa, Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika sasa imepangwa kufanyika kila baada ya miaka minne badala ya miaka miwili. Uamuzi huo wa ghafla ulitolewa katika kikao cha kamati kuu ya baraza hilo katika mji mkuu wa Morocco na kutangazwa katika mkutano na waandishi wa habari na Rais wa CAF Patrice Motsepe. Michuano hiyo inayoingiza takriban asilimia 80 ya mapato ya CAF, imekuwa ikifanyika kila baada ya miaka miwili tangu kuanzishwa kwake mwaka 1957.

Rais wa CAF Patrice Motsepe

Motsepe alisema fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika zilizopangwa kufanyika mwaka 2027 nchini Kenya, Tanzania na Uganda zitaendelea na kisha michuano mingine kufanyika mwaka 2028 lakini baada ya hapo itaandaliwa kila baada ya miaka minne. Motsepe alitangaza kuzindua Ligi ya Mataifa ya Afrika kila mwaka kuanzia 2029 ili kuziba pengo hilo, akiiga mfano wa Ulaya ambayo huwa na michhuano ya ubingwa kila baada ya miaka minne.

Shirikisho la Soka la Asia siku ya Jumapili lilitangaza uamuzi wake wa kuanzisha Ligi ya Mataifa ya AFC, mashindano mapya yanayolenga kuimarisha ubora na ushindani wa soka ya kimataifa miongoni mwa vyama vyake wanachama. Tangazo hilo linakuja siku moja baada ya AFC kusema itaanzisha mashindano kama hayo mwaka wa 2029. Hatua hiyo inafuatia kuanzishwa kwa Ligi ya Mataifa na UEFA mwaka wa 2018, ambapo timu za kitaifa za Ulaya zimegawanywa katika ngazi na hucheza wakati wa madirisha maalum ya kimataifa. Katika michuano hiyo, Tanzania (Taifa Stars) chini ya kocha Miguel Gamondi, itaanza kampeni yake kwa kibarua kigumu dhidi ya moja ya miamba wa soka barani Afrika, Nigeria, Jumanne hii ya Desemba 23, kuanzia saa mbili na nusu usiku kwa saa za Afrika Mashariki. Nigeria inalenga kufanya vizuri zaidi kuliko fainali za 2023. Mwakilishi mwengine wa Afrika Mashariki, Uganda, inanza kampeni yake Jumanne kwa kuchuana na Tunisia.

 

Riadha: Tanzania na Ethiopia kidedea India

Mwanariadha wa Tanzania na Jeshi la Wananchi (JWTZ), Alphonce Felix Simbu, ameendelea kuonyesha kiwango cha juu kimataifa baada ya kumaliza nafasi ya pili katika mbio za Kolkata 25KM zilizofanyika Jumapili, Desemba 21, 2025 Kolkata India. Katika mbio hizo, Simbu alitumia saa 1:11:56 kumaliza wa pili nyuma ya Joshua Cheptegei wa Uganda aliyeshinda kwa saa 1:11:49, huku ushindani ukiwa mkali kati ya wanariadha hao bora. Nafasi ya tatu ilichukuliwa na Tebello Ramagoana wa Lithuania alietumia saa 1:11:59, wakati Collins Kipkorir wa Kenya alimaliza nafasi ya nne kwa saa 1:12:02.

Kwa upande wa Wanawake, wanariadha wa Ethiopia walitawala kwa kuchukua nafasi nne za juu, Degitu Azimeraw akiibuka mshindi kwa saa 1:19:36 , akifuatiwa na Situme Kabede kwa saa 1:20:28, Meselech Alemayehu kwa saa 1:20:48 na Kuftu Tayri kwa saa 1:23:32. Matokeo hayo yanaendeleza mafanikio ya Simbu mwaka huu, ikiwemo kumaliza nafasi ya pili katika Boston Marathon, Marekani, kushinda medali ya dhahabu katika mashindano ya dunia yaliyofanyika Septemba Tokyo, Japan, na kuweka rekodi ya Mtanzania wa kwanza kushinda marathoni za dunia. Pia aliingia kwenye fainali ya mwanariadha bora wa kiume wa mwaka 2025, kipengele cha wanariadha wanaokimbia nje ya uwanja, napo aliweka rekodi ya kuwa Manzanita wa kwanza kuingia fainali za tuzo zinazoandaliwa na Shirikisho la riadha la dunia. Shirikisho la riadha la Tanzania (RT), limeeleza kuwa mafanikio ya Simbu yanaendelea kuitangaza Tanzania kimataifa na kuchochea maendeleo ya riadha nchini, huku yakitajwa kuwa chachu kwa wanariadha chipukizi kuamini uwezo wao kujituma zaidi.

Mkenya ang’ara mashindano ya dunia ya dart

Rais wa Kenya, William Samoei Ruto, amempongeza David Munyua baada ya ushindi wake wa ajabu katika raundi ya ufunguzi ya Mashindano ya Darts Duniani. Munyua, daktari wa mifugo mwenye umri wa miaka 30 ambaye hajawahi kuondoka Afrika kabla ya mashindano haya, alimshinda Mike De Decker, nambari 18, katika wakati wa kihistoria. Tayari alikuwa ameandika historia kama Mkenya wa kwanza kuingia katika shindano hilo baada ya kushinda kufuzu kwa Mashindano ya Kundi la Darts Afrika na akashikilia rekodi ya kupiga mara mbili 20 na kushinda 3-2, na kuzua shangwe katika Jumba la Alexandra. Haikuwa London pekee ambapo mashabiki walifurahishwa na ushindi wake, huku habari zikienea nchini mwake kuhusu ushindi wake mkubwa na rais wake akimpongeza kwa X.

Munyua aitoa Kenya na Afrika Mashariki kimasomaso London

Rais Ruto amesema: “Hongera David Munyua kwa ushindi wako wa ajabu katika raundi ya kwanza katika Mashindano ya Darts Duniani ya Paddy Power. Sasa Munyua anawajihiwa na pambano kati yake na mshindi wa mgaragazano baina ya Kevin Doets na Matthew Dennant katika raundi ya pili huku akitafuta kutengeneza historia zaidi na kusonga mbele hadi raundi ya tatu. Aliiambia Sky Sports: “Ni jambo la kushangaza. Sikutarajia. Lakini sasa imetokea na ninafurahi kuhusu hilo. “Ni wakati mkubwa sana kwa mchezo wenyewe, kwa Afrika na Kenya. Ni jambo la unyenyekevu. Mchezo unaweza kukua. Ninafurahi kwamba nilifanya kila niwezalo.”

Kila duru ya mashindano hayo inazidi kuwa kubwa nay a kufana zaidi, na mwaka huu mambo sii tofauti. PDC imethibitisha kwamba, hundi ya kuvunja rekodi inamsubiri mshindi mnamo Januari 3 huku wachezaji 128 wakijimwaya mwaya uwanjani kwa ajili ya sehemu ya mfuko wa pauni milioni 5. Alama ya hivi punde katika ukuaji wa kasi wa mchezo huo inakuja baada ya Luke Littler kutwaa taji la kwanza la dunia katika taaluma yake mwaka jana, mafanikio ambayo kipaji hicho cha miaka 18 kilijipatia pauni 500,000.

Dondoo za Hapa na Pale

Kocha maarufu wa timu ya Ligi Kuu ya Uingereza ya Mancester City kwa mara nyingine tena ameonesha uungwana na amechukua hatua ya kibinadamu ya kuwahami na kuwakingia kifua wananchi madhlumu wa Palestina. Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, Pep Guardiola anahesabiwa kuwa muungaji mkono maarufu zaidi wa Palestina kwenye fani ya mpira wa miguu. Kwa mujibu wa ripoti ya leo Ijumaa ya mwandishi wa gazeti la kila siku la Marca la Uhispania, Leila Hamed, kocha huyo ametangaza kuwa atahudhuria tamasha la kuiunga mkono Palestina huko Barcelona.

Guardiola amekuwa akitangaza wazi mshikamano na Wapalestina

Kocha wa Manchester City ameshatangaza kuwaunga mkono watu wa Palestina na Ghaza mara saba kwa njia tofauti katika miezi sita iliyopita. Mwezi uliopita, wakati timu ya taifa ya Palestina ilipokwenda Uhispania kucheza mechi mbili za hisani dhidi ya timu za Catalonia na Basque, Guardiola aliwahimiza watu wa nchi yake kuhudhuria kwa wingi kenye mechi hizo, na mwito wake ulipelekea kukusanywa zaidi ya dola milioni 2 za kuwasaidia wananchi wa Ghaza. Mwandishi wa habari za Michezo, Leila Hamed, ameripoti pia kwamba, tamasha hilo limeandaliwa na kundi la “Act Palestine” ili kuchangisha fedha kwa ajili ya harakati za Wapalestina na litafanyika Barcelona Januari 29, 2026. Kwa mujibu wa mwandishi huyo wa habari za michezo za gazeti la Marca la Uhispania, Pep Guardiola ndiye mtu mashuhuri zaidi na wa kwanza kujitolea kuhudhuria tamasha hilo ili watu wengi zaidi waweze kushiriki na kuweze kuchangishwa fedha nyingi zaidi kwa ajili ya wananchi madlumu wa Palestina.

Mbali na hayo, mshambuliaji wa Ufaransa Ousmane Dembele alishinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Wanaume wa FIFA ya 2025, huku kiungo wa Barcelona Aitana Bonmati akishinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Wanawake kwa mwaka wa tatu mfululizo, FIFA ilitangaza Jumanne usiku. Dembele alifunga mara nane na kutoa pasi sita za mabao ili kuiongoza Paris Saint-Germain kutwaa taji lao la kwanza la Ligi ya Mabingwa ya UEFA. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 pia alitajwa kuwa MVP katika mashindano ya bara na Ligue 1 katika msimu wa 2024/25 na kuisaidia timu yake kufika fainali ya Kombe la Dunia la Klabu la FIFA.

 

Dembele wa PSG na timu ya taifa ya Ufaransa kidedea

Bonmati, 27, ambaye alifanyiwa upasuaji wa fibula iliyovunjika mapema Desemba, alishinda tuzo za MVP katika Ligi ya Mabingwa ya Wanawake ya UEFA na Euro ya Wanawake 2025, ingawa alishindwa kuiongoza klabu yake au timu yake ya taifa kushinda taji lolote. Luis Enrique wa Uhispania alishinda tuzo ya Kocha Bora wa Wanaume, na kocha wa Uingereza Sarina Wiegman alichaguliwa kuwa Kocha Bora wa Wanawake kwa mara ya tano iliyorekodiwa. Enrique aliiongoza PSG kuishinda Inter Milan katika fainali ya Ligi ya Mabingwa, na pia kushinda mataji matatu ya ndani ya Ligue 1, Coupe de France na Trophee des Champions. Wiegman aliiongoza Uingereza kwenye taji la Euro la Wanawake la 2025, akiwashinda mabingwa wa dunia Uhispania kwa mikwaju ya penalti. Wachezaji sita walioisaidia PSG kushinda taji lao la Ligi ya Mabingwa ya UEFA na kufikia fainali ya Kombe la Dunia la Klabu la FIFA wamepigiwa kura katika 11 Bora ya Wanaume ya FIFA, huku wachezaji saba wa Uhispania na wanne kutoka Uingereza wakitajwa katika 11 Bora ya Wanawake ya FIFA. Gianluigi Donnarumma wa PSG alitajwa kuwa Kipa Bora wa Wanaume, huku Hannah Hampton wa Chelsea akitajwa kuwa Kipa Bora wa Wanawake. Bao la Santiago Montiel kwa Independiente dhidi ya Independiente Rivadavia mnamo Mei 11, 2025 katika Torneo Apertura ya Argentina lilishinda Tuzo ya Puskas ya 2025 kwa bao bora la mwaka.

Kwengineko, klabu ya Simba ya Tanzania imemtangaza Steven Barker, raia wa Afrika Kusini kuwa Kocha wao mpya, Steven Barker (57) alikuwa Kocha wa Stellenbosch ya Afrika Kusini toka 2017. Steven Barker amewahi kufundisha timu za University of Pretoria (2008-2014) na Amazulu (2014-2016) na amewahi kuzichezea timu Wits University (1990-1998) na SuperSport United 1999-2000. Awali, Simba SC ilikuwa imemteua Hemed Suleiman ‘Morocco’ kuwa kocha mkuu wa muda wa timu hiyo. Hemed Morocco, ambaye pia ni kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, alitwikwa jukumu hilo Septemba kukaimu hadi pale klabu hiyo itakapompata kocha mpya wa kudumu. Wasimamizi na mashabiki wa Simba wametangaza kuridhishwa na uteuzi wa Barker nwakimtaja kama mkufunzi mwenye haiba.

Huku hayo yakiarifiwa, IFFHS imeachia hadharani orodha ya Klabu 500 bora Duniani kuanzia Disemba Mosi,2024 hadi Novemba 30,2025 ambapo Afrika imejumuisha Klab7 31, Yanga wakiwa nafasi ya 7 wakati Simba ikikamata nafasi ya 11. Kwa Afrika, Pyramids ndio Vinara na ni ya 30 Duniani. Hata hivyo, Simba inasisitiza kuwa wao ndio klabu namba 2 barani Afrika baada ya Al Ahly ya Misri kwa kuwa na wafuasi wengi. “Si rahisi klabu kuwa na wadhamini na washirika 18 Kwa ukanda wa Afrika Mashariki,’’ Amesema Crescentius Magori Mwenyekiti wa bodi klabu ya Simba akijivunia wadhamini wengi Simba kuliko klabu yoyote Afrika Mashariki

Na bondia Anthony Joshua ameendelea kuihakikishia dunia kuwa ni moto wa kuote mbali. Hii mi baada ya kumshinda Jake Paul kwa TKO, kwenye raundi ya sita ya pambano lililofanyika usiku wa Ijumaa, Desemba 19, 2025, kwenye uwanja wa Kaseya Center mjini Miami, Florida. Joshua, ambaye ni bingwa wa uzito wa juu, alikuwa na kiwango bora sana na kufanya iwe ngumu kwa Paul kummudu tangu raundi za mwanzoni na hatimae kulamba mchanga raundi ya 6.

……………….TAMATI……………

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *