Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu adhabu ya kulipa faini ya Sh15 milioni au kwenda jela, wanafunzi watatu wa vyuo vikuu vitatu tofauti nchini, waliokuwa na kesi ya kumpiga na kumjeruhi mwanachuo mwenzao, baada ya kutiwa hatiani kwa makosa saba likiwemo la kutishia kuua na kusambaza taarifa za uongo.

‎Waliohukumiwa adhabu hiyo ni Mary Matogolo (22) ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ‎Ryner Mkwawili, wa Chuo Kikuu Ardhi Dar es Salaam na Asha Juma, mwanafunzi wa Chuo cha Uhasibu, Dar es Salaam (TIA).

Washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka manane katika kesi ya jinai namba 13199 ya mwaka 2025.

‎Hukumu hiyo imetolewa leo Jumatatu, Desemba 22, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Gwantwa Mwankuga, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutolewa hukumu.

‎Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mwankuga alisema upande wa Jamhuri ulipeleka mashahidi 12 na vielelezo 16 ambao walidhibitisha mashtaka pasi na kuacha shaka katika mashtaka saba kati ya manane waliyoshtakiwa nayo.

Hata hivyo, hadi saa 10:48 Alasiri mshtakiwa wa pili (Ryner) na watatu (Asha) wamefanikiwa kulipa faini hiyo na kukwepa adhabu ya kifungo, huku mshtakiwa wa kwanza (Mary) akipelekwa gerezani kwenda kuanza kutumikia adhabu baada ya kushindwa kulipa faini hiyo.

Hakimu Mwankuga akichambua hukumu alisema pamoja na upande wa mashtaka kujitahidi kuonyesha washtakiwa walitenda kosa hilo, lakini mahakama ya juu ilishawahi kuweka utaratibu wa kosa la kula njama lijitegemee lenyewe na sio kuliunganisha na kosa lingine.

“Hivyo haikuwa sahihi kwa upande wa mashtaka kuweka shtaka la kula njama na kuchanganya na shtaka la kusambaza taarifa za uongo, hivyo kwa hali hiyo shtaka la kula njama limekufa,” amesema hakimu.

Amesema mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo ikiwemo video, maelezo ya mlalamikaji na daktari ambaye alithibitisha mlalamikaji alipata majeraha sehemu mbalimbali ya mwili wake.

Mshtakiwa Mary Matogolo (aliyejifunika mtandio mweusi) akiwa chini ya ulinzi wa askari kanzu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Jumatatu Desemba 22, 2025. Picha na Hadija Jumanne

“Hivyo basi ushahidi huu wa Jamhuri umetosha kuthibitisha mashtaka pasi na kutacha shaka yoyote, hivyo washtakiwa wametiwa hatiani kama walivyoshtakiwa,” amesema Hakimu Mwankuga.

Hakimu Mwankuga amesema mshtakiwa wa tatu katika kesi hiyo (Asha) amemtia hatiani kwa mashtaka matatu, hivyo amepigwa faini ya kulipa jumla ya Sh7 milioni au kwenda jela miaka mitatu na miezi sita.

‎Akifafanua faini hiyo, hakimu Mwankuga amesema mashtaka yaliyomtia hatiani Asha ni kusambaza taarifa za uongo  katika mtandao wa WhatsApp yenye maneno kuwa  “Toa  sauti umefanya mapenzi na Mwijaku lini na wapi”. “Mshtakiwa shtaka hili, mahakama inakuhukumu kulipa faini ya Sh5 milioni na ukikosa utatumikia kifungo cha miaka mitatu gerezani” amesema Hakimu Mwankuga.

‎Vile vile Asha ametiwa hatiani katika shtaka la kusababisha madhara ya mwili ambapo atatakiwa kulipa faini ya Sh1 milioni au kwenda jela miezi sita, huku shtaka la kutishia kumuua, mshtakiwa huyo amepigwa faini ya Sh1 milioni au kwenda jela miezi sita.

‎Kwa upande wa mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo (Mary) yeye amemtia hatiani katika mashtaka matano na amepigwa kulipa faini ya jumla ya Sh5 milioni au kwenda jela miezi sita.

‎”Mahakama imemtia hatiani Mary kwa makosa matano na kila kosa atatakiwa kulipa faini ya Sh1 milioni au u kwenda jela miezi sita kwa kila kosa” amesema Hakimu Mwankuga.

‎Akiendelea kuchambua hukumu hiyo, hakimu Mwankuga amesema Mary ametiwa hatiani katika mashtaka ya kusababisha madhara kichwani kwa kumpiga na chuma mlalamikaji, pia kumvuta nywele, kuharibu mali ya mlalamikaji ambayo ni simu aina ya Samsung pamoja na laini yake na kutishia kumuua mlalamikaji.

‎Kwa upande wa mshtakiwa Ryner, Mahakama hiyo imemtia hatiani kwa makosa matatu na kumpigwa faini ya jumla ya Sh3 milioni au kwenda jela miezi sita kwa kila kosa.

‎Hakimu Mwankuga amesema mashtaka yaliyomtia hatiani Ryner ni kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa WhatsApp, kutumia nguvu kumvuta nywele Magnificati na kusababisha madhara makubwa pamoja na kutishia kuua, ambapo kila shtaka atatakiwa kulipa faini ya Sh1 milioni au kwenda jela miezi sita kwa kila shtaka.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Bernardo Chalo aliomba mahakama itoe adhabu kali dhidi ya washtakiwa hao hasa ikizingatiwa kuwa ni wanachuo na wasomi.

“Upande wa Jamhuri hatuna kumbukumbu ya makosa ya nyuma ya washtakiwa hawa, lakini, tunaomba wapewe adhabu kali  ili iwe fundisho kwa wengine kwa kuwa  hawa ni wasomi  kutoka vyuo vikuu na  kitendo walichokifanya hakikubaliki katika jamii” amesema wakili Chalo.

Mmoja ya washtakiwa ambao ni wanachuo wanadaiwa kujeruhi mwanachuo mwenzao akiwa chini ya ulinzi wa askari Polisi leo Jumatatu Desemba 22, 2025 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne

Kwa upande wake wakili wa utetezi, Peter Shapa aliomba mahakama iwahurumie kwa kuwa upande wa mashtaka hawana rekodi za makosa ya jinai dhidi ya washtakiwa hao, lakini pia ni wanafunzi bado wanaendelea kusoma na pia wanategemewa na wazazi wao.

Hakimu Mwankuga amesema mahakama imezingatia ushahidi wa utetezi ulioletwa haukuwa na nyaraka wala vielelezo vilivyotolewa mahakamani hapo.

“Hivyo, Mahakama inaona upande wa utetezi haukuibua utetezi wowote ili kupunguza ushahidi wa upande wa mashtaka, hivyo mahakama inawatia hatiani kama walivyoshtakiwa,”amesema.

Pia, amesema mahakama imezingatia washtakiwa ni wakosefu wa mara ya kwanza na shufaa waliyoitoa kupitia wakili wao, mahakama inatoa adhabu nafuu.

“Pamoja na adhabu hii kuwa nafuu kwa washtakiwa hawa ambao ni wanafunzi lakini sheria lazima ifuate mkondo wake” amesema Hakimu na kuwahukumu adhabu hiyo.

Katika kesi ya msingi kwa pamoja washtakiwa Machi 14, 2025, eneo la Sinza wilayani Ubungo, Dar es Salaam walikula njama kwa nia ya kutenda kosa la kuchapisha taarifa za uongo.

‎Shtaka la pili  ambalo ni kusambaza  taarifa za uongo linawakabili  Mary na Asha, ambapo  siku hiyo walisambaza taarifa za uongo, katika mtandao wa WhatsApp yenye maneno kuwa  “Toa  sauti umefanya mapenzi na Mwijaku lini na wapi”.

‎Shtaka la tatu ambalo pia ni kusambaza taarifa za uongo linalomkabili, Ryner peke yake, ambapo alisambaza taarifa hizo kupitia mtandao wa WhatsApp.

‎Shtaka la nne ambalo ni kusababisha madhara makubwa, linamkabili Mary peke yake, akidaiwa kuwa siku hiyo alimshambulia Magnificant Kimario kwa kumpiga kichwani na chuma na hivyo kumsababishia maumivu makali.

‎Shtaka la tano ambalo ni kusababisha madhara makubwa, linawakabili washitakiwa wote.

‎Inadaiwa kuwa washtakiwa hao kwa pamoja kwa kutumia nguvu walimvuta nywele Magnificati na kusababisha madhara makubwa.

‎Shtaka la sita na saba, ni kuharibu mali, pia yanamkabili Mary peke yake, ambapo aliharibu laini ya simu na simu aina ya Samsung yenye thamani ya Sh700,000 mali ya Magnificati.

‎Shtaka la nane ni kutishia kuua, lililokuwa linawakabili washtakiwa wote, ambapo siku ya tukio, walimtishia kumuua. Magnificati kwa kutumia kisu.

‎Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Mei 30, 2025 na kusomewa mashtaka hayo.

Hata hivyo, ‎Novemba 21, 2025 washtakiwa hao walikutwa na kesi ya kujibu na kutakiwa kuanza kujitetea Novemba 26, 2025.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *