Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro inatarajia kuwa mwenyeji wa mbio za Rombo Marathon zitakazofanyika Desemba 23, 2025, zikitarajiwa kuwahusisha zaidi ya wanariadha na wakimbiaji 3,000.

Tukio hilo, linalofanyika kwa mara ya nne, linalenga kukuza michezo, kuhamasisha utalii wa ndani na kuimarisha uhifadhi wa mazingira.

Mbali na mashindano ya mbio, kutakuwa na matukio mbalimbali ya burudani yakiwemo nyama choma festival, matembezi na kukimbia msituni, pamoja na vyakula vya asili kama ng’ande, ngararimo na kinywaji cha jadi cha mbege.

Akizungumza kuhusu maandalizi hayo, Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala, amesema Rombo Marathon ya mwaka huu itakuwa ya kipekee kwa kuwa itafanyika kwa siku tatu na kuambatana na Ndafu Festival.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Kamati ya Maandalizi ya Rombo Marathon, Joseph Katembo, amesema usajili unaendelea vizuri na zawadi zimeandaliwa kwa washindi wa makundi mbalimbali ya mbio. Amesema washiriki wa kilomita 21, 10 na tano watapata zawadi kulingana na nafasi zao, hatua inayolenga kuongeza hamasa na ushiriki.

Mbio hizo zitafanyika katika msitu wa Rongai, eneo lenye mandhari ya Mlima Kilimanjaro linalovutia wakimbiaji na watalii.

Kwa upande wa mazingira, wilaya imepanga kupanda miti zaidi ya 10,000 Desemba 24, 2025, kama sehemu ya juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
#StarTvUpdate

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *