Zijue athari za ongezeko la vina vya maji KenyaZijue athari za ongezeko la vina vya maji Kenya

Mkulima mmoja anayeitwa Dickson Ngome amesema, alianza kulima katika eneo la Ziwa Naivasha mwaka 2008, shamba lake wakati huo likiwa kwenye umbali wa zaidi ya kilomita mbili kutoka ufukweni mwa ziwa hilo. Katika shamba lake hilo la ekari moja na nusu, alilima mboga kwa ajili ya kuuza sokoni. Wakati huo, kiwango cha maji ya ziwa kilikuwa kinapungua, na wakazi waliogopa kwamba lingeweza kukauka kabisa.

Lakini hali imebadilika kwa kasi. TMwaka huu, mvua zilianza mapema mwezi Septemba na kuendelea kwa miezi kadhaa. Siku moja mwishoni mwa Oktoba, Ngome na familia yake waliamka na kushangaa kukuta nyumba na shamba lao vikiwa ndani ya maji. Usiku mmoja tu, maji yalipanda na kufunika kila kitu kwa kina cha zaidi ya futi moja.

Mke wake, Rose Wafula, anasema tukio hilo liliwashitua sana, kwani hawakutarajia maji kufika nyumbani mwao kwa ghafla. Kwa sasa, familia hiyo yenye watoto wanne imelazimika kuondoka nyumbani na wanaishi katika jengo la shule lililoachwa karibu na eneo hilo. Kwa mujibu wa takwimu, zaidi ya watu elfu tano wamehamishwa makazi yao mwaka huu pekee kutokana na kuongezeka kwa maji ya Ziwa Naivasha. Wanasayansi wanasema hali hii inahusishwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha mvua nyingi na mabadiliko ya joto.

Hasara kubwa yaonekana pia kwa sekta ya kilimo cha maua

Si Ziwa Naivasha pekee lililoathirika. Maziwa ya Baringo, Nakuru na Turkana nayo yamekuwa yakiongezeka kwa zaidi ya miaka 15 sasa. Wataalamu wa mazingira wanasema baadhi ya maziwa haya yamefikia viwango vya juu zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia.

Kuongezeka kwa maji kumesababisha pia hasara kubwa kwa sekta ya kilimo cha maua, hasa katika Ziwa Naivasha, ambapo mashamba mengi ya maua yamefunikwa na maji. Sekta hii ni muhimu sana kwa uchumi wa Kenya, ikichangia mapato ya zaidi ya dola bilioni moja kwa mwaka. Stanley Wachanga ni mwenyekiti wa wakaazi wa eneo la Kihoto yaliko mashamba makubwa ya maua na anahisi hawajatendewa haki.

“Karibu zaidi ya miaka sitini tuko hapa na sasa ndio wanasema hatustahili kuwa kwenye sehemu ile. Na yale maneno wananena hatuhusishwi. Kwahiyo ni mambo ambayo sio watu wa Kihoto wanakaa chini kuelezana yale mambo hayastahili.”

Kenya, Kilimo cha maua
Kuongezeka kwa maji kumesababisha pia hasara kubwa kwa sekta ya kilimo cha maua, hasa katika Ziwa Naivasha, ambapo mashamba mengi ya maua yamefunikwa na maji. Picha: PATRICK MEINHARDT/AFP via Getty Images

Utafiti unaonyesha kuwa kati ya mwaka 2011 na 2023, maeneo ya maziwa Afrika Mashariki yameongezeka kwa zaidi ya kilomita za mraba elfu sabini, hali iliyosababisha zaidi ya kaya elfu sabini na tano kuhamishwa katika Bonde la Ufa pekee.

Serikali ya Kaunti ya Nakuru imesema inakabiliana na hali hiyo kama dharura, ikitoa msaada wa magari ya kuhamisha wakazi na kusaidia kulipia kodi kwa familia zisizo na uwezo. Alex Mbugua ni mwakilishi wa wadi ya Lakeview katika kaunti ya Nakuru ambako athari za maji ni nyingi na anakiri hali ni mbaya.

” Kuna wale ambao wamewekeza kwa kiasi kikubwa. Kuna wale wamezaliwa  hapa Kihoto. Wanapoambiwa waondoke wahame bila kutengewa sehemu mbadala sio sawa… kwa mara ya kwanza naiomba serikali iwasikilize watu hawa. Ukiwaambia waondoke wanaenda wapi?”

Hata hivyo, wataalamu wanatoa wito wa kuwepo kwa suluhisho la muda mrefu, ikiwemo mipango bora ya makazi, uhifadhi wa mazingira, na juhudi za kimataifa kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa familia ya Ngome, matumaini bado ni madogo. Wakiwa bado wanaishi katika shule iliyoachwa, hawajui ni lini, au kama kabisa, watarejea kwenye ardhi yao. Kuendelea kuongezeka kwa maji ya Ziwa Naivasha kunaacha maswali mengi juu ya mustakabali wao na wa maelfu ya wengine wanaoishi kandokando ya maziwa ya Bonde la Ufa.

Kuongezeka kina cha maji ziwa Turkana

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *