
Maswa. Licha ya Serikali kupiga marufuku ajira kwa watoto wadogo na kuweka sheria kali za kulinda haki zao, vitendo vya kuwatumikisha bado vinaendelea kwa kasi katika mnada mjini Maswa, mkoani Simiyu, hali inayozua maswali kuhusu utekelezaji wa sheria na uwajibikaji wake.
Ufuatiliaji uliofanywa na Mwananchi kwa siku kadhaa umebaini watoto wenye umri wa kati ya miaka tisa hadi 15 wanafanya kazi ya kutenga chakula kwa wateja kuanzia asubuhi hadi jioni katika mazingira yasiyo salama, wakilipwa ujira mdogo wa Sh1,000 kwa kutwa.
Baadhi ya watoto waliozungumza kwa sharti la kutotajwa majina wamesema hulazimika kufanya kazi ili kusaidia familia zao.
Wengine wameeleza hushindwa kuhudhuria masomo ipasavyo kutokana na uchovu na muda mrefu wanaoutumia kazini.
“Nikifanya kazi napata elfu moja. Nikirudi nyumbani jioni huwa nimechoka sana, wakati mwingine nashindwa kufanya kazi za shule,” amesema mmoja wa watoto hao ambaye ni wa kiume.
Mkazi wa mjini Maswa, Mary Nyamhanga amesema hali hiyo ni ya kusikitisha na inahitaji hatua za haraka kuishughulikia.
“Watoto hawa wanapaswa kuwa shuleni. Huu ni unyonyaji wa waziwazi. Serikali isipokaa macho, tutapoteza kizazi,” amesema.
Mfanyabiashara katika mnada huo, Said Halfan amekiri kuwapo tatizo hilo, akieleza umasikini wa familia ndio chanzo kikuu.
“Wazazi wengine wanawalazimisha watoto wafanye kazi ili kusaidia familia. Hata hivyo, kisheria hili haliruhusiwi,” amesema.
Basila Bruno, Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Maswa anayeshughulikia masuala ya watoto amesema ajira kwa watoto ni kosa la kisheria na zinakiuka haki za msingi za mtoto.
“Sheria ya mtoto na sheria ya ajira haziruhusu mtoto kufanya kazi nzito wala kufanya kazi kwa muda mrefu. Tunachokiona hapa mnadani ni ukiukwaji wa wazi wa sheria. Tutachukua hatua za kisheria kwa wazazi na waajiri watakaobainika kuhusika,” amesema.
Amesema ofisi yake kwa kushirikiana na maofisa ustawi wa jamii imeanza kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara ya ajira kwa watoto.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa, amesema halmashauri haitavumilia vitendo vinavyokiuka haki za mtoto.
“Halmashauri imejipanga kuimarisha doria katika minada na maeneo yote ya biashara. Hatutasita kuchukua hatua kali kwa yeyote atakayebainika kuwatumikisha watoto kinyume cha sheria,” amesema.
Amesema serikali ya wilaya itaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi, maofisa kazi na wadau wa ustawi wa jamii kuhakikisha watoto wanarudishwa shuleni na kulindwa dhidi ya aina zote za unyonyaji.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, mtoto haruhusiwi kufanya kazi hatarishi au kazi nzito zinazoweza kuhatarisha afya, usalama na maendeleo yake.
Hata hivyo, hali halisi katika mnada wa Maswa inaonyesha pengo kubwa kati ya sera na utekelezaji wake.
John Bosco, mdau wa haki za mtoto mkoani Simiyu anasema bila ukaguzi wa mara kwa mara, adhabu kali kwa wanaokiuka sheria na kampeni endelevu za elimu kwa jamii, jitihada za kupambana na ajira kwa watoto zitabaki kuwa ahadi tu kwenye karatasi.
“Hali hiyo inaathiri moja kwa moja haki ya mtoto kupata elimu, afya na malezi salama kama inavyotamkwa katika sheria ya mtoto na mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania tumeridhia,” amesema.