ARUSHA: MKUU wa Chuo cha Uhasibu (IAA) mkoani Arusha, Profesa Eliamani Sedoyeka amesema mwaka wa fedha Julai 2025 hadi Juni 2026, chuo hicho kimetenga Sh bilioni 4 kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunza ili kuendani na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Sedoyeka amesema tayari utekelezaji wa mpango wa madarasa janja ‘smart Class’ kwa lengo la kuwa na kampasi janja ‘smart campus’ na kutumia Tehama kikamilifu katika ufundishaji, kutumia mifumo ya kisasa ya kidijitali na kujifunzia kwa njia ya mtandao.

Amesema chuo hicho kimeendelea kupanua wigo wa programu zake za kitaaluma ikihakikisha viwango vya ubora vinazingatiwa miongozo ya kitaifa na kimataifa na kwa mwaka huu wa masomo ulioisha kulikuwa na jumla ya kozi 81, kati ya hizo kozi 19 ni za astashahada, kozi 20 ni stashahada, kozi 27 ni za shahada na kozi 15 ni za ngazi ya shahada ya uzamili.
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi IAA, Dk Mwamini Tulli amesema chuo kinaendelea kuboresha na kupanua miundombinu ya kufundishia na kujifunzia ikiwemo madarasa, ofisi za wahadhiri, maktaba na miundombinu ya Tehama katika kampasi zake zote za Arusha, Babati, Dar es Salaam, Dodoma na Songea. Vile vile, chuo kinaendelea kujipanga kuwekeza nguvu na rasilimali katika ujenzi wa kampasi mpya ya Bukombe.
