Elimu ni haki ya msingi ya kila mtoto, lakini pia ni jukumu linalohitaji maandalizi ya kifedha.

Kwa bahati mbaya, wazazi wengi hukumbwa na changamoto kubwa hasa mwisho wa mwaka, kipindi ambacho mahitaji ya kifedha huwa mengi: ada za shule, sherehe za mwisho wa mwaka, sikukuu, safari, pamoja na mahitaji mengine ya kifamilia.

Hali hii husababisha mzigo mkubwa wa kifedha na wakati mwingine watoto kuchelewa au kukosa kwenda shule kwa wakati.

Mwisho wa mwaka ni kipindi kigumu kwa wazazi wengi kwa sababu mapato yao mara nyingi hayalingani na matumizi. 

Wafanyakazi wengi hupokea mishahara ileile ilhali mahitaji huongezeka. Wafanyabiashara wadogo hupata mtikisiko wa biashara kutokana na ushindani au mabadiliko ya soko. Wakulima nao mara nyingi hawakuwa wameuza mazao yao au wanakutana na bei ndogo sokoni. Katika mazingira haya, ada ya shule huonekana kama mzigo mkubwa.

Changamoto nyingine ni ukosefu wa mipango ya kifedha ya mapema. Wazazi wengi husubiri hadi shule itakapofungua ndipo waanze kuhangaika kutafuta ada. Wengine hukopa kwa riba kubwa, huuza mali za familia, au kuomba msaada wa dharura. 

Hali hii huleta msongo wa mawazo kwa wazazi na pia huathiri kisaikolojia watoto wanapochelewa kuripoti shuleni.

Mzazi fanya haya

Ili kupunguza au kuondoa mzigo wa ada, wazazi wanapaswa kutumia mbinu mbalimbali za kifedha na kimaisha.

Kwanza, kupanga bajeti ya mwaka mzima ni jambo la msingi. 

Wazazi wanapaswa kujua mapato yao ya mwaka na kuyagawa kulingana na vipaumbele.

Ada ya shule inapaswa kupewa kipaumbele cha juu kuliko mambo mengi yasiyo ya lazima. Ni vyema mzazi akaweka akiba ndogo kila mwezi kwa ajili ya ada badala ya kusubiri msimu wa kufungua shule.

Pili, kuweka akiba maalum ya elimu ni mbinu yenye mafanikio. Akaunti ya benki, kikundi cha kuweka na kukopa , au hata sanduku la akiba nyumbani vinaweza kusaidia. 

Akiba ya kidogo kidogo hujenga kiasi kikubwa baada ya muda bila mzigo mkubwa.

Tatu, kuongeza vyanzo vya kipato. Wazazi wanaweza kuanzisha miradi midogo kama kilimo cha umwagiliaji, ufugaji wa kuku, biashara ndogondogo, au kazi za ziada. 

Kipato cha ziada kinaweza kuelekezwa moja kwa moja kwenye ada ya shule bila kuathiri matumizi ya kila siku ya familia.

Nne, kuzungumza mapema na uongozi wa shule. Shule nyingi huwa tayari kusaidia wazazi wenye nia njema kwa kuwaruhusu kulipa ada kwa awamu endapo watawasiliana mapema. Kukaa kimya hadi deni liwe kubwa huongeza ugumu zaidi.

Moja ya sababu kubwa zinazofanya wazazi washindwe kulipa ada kwa wakati ni matumizi ya anasa na starehe. Sherehe kubwa zisizo na mipango, ununuzi wa simu za gharama kubwa, nguo za bei ya juu, pombe, safari zisizo za lazima, na matumizi ya burudani kupita kiasi huathiri sana bajeti ya familia.

Ni muhimu wazazi wakajiuliza: Je, matumizi haya yanachangiaje maisha ya mtoto wangu baadaye? Fedha inayotumika kwenye starehe za muda mfupi ingeweza kulipa ada ya shule, kununua vitabu, sare, au vifaa vya kujifunzia. 

Kupunguza anasa hakumaanishi kuacha furaha kabisa, bali ni kuweka uwiano na vipaumbele sahihi.

Wazazi wanapaswa kujifunza nidhamu ya fedha kwa vitendo. Mtoto anayewaona wazazi wake wakitumia fedha kwa busara hujifunza pia thamani ya fedha na umuhimu wa kupanga maisha.

Mpe urithi mtoto

Elimu ni urithi wa kudumu ambao mzazi anaweza kumpa mtoto. Mali zinaweza kuharibika au kupotea, lakini elimu hubaki na kumsaidia mtoto maisha yake yote. 

Mtoto aliyepata elimu bora ana nafasi kubwa ya kupata ajira, kujiajiri, kusaidia familia yake, na kuchangia maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Wazazi wanapaswa kukumbuka kuwa elimu ndiyo msingi wa mafanikio ya mtoto. Kumchelewesha mtoto shule kwa sababu ya ada ni sawa na kuchelewesha ndoto zake. 

Mtoto anayekosa masomo kwa muda hupoteza mwelekeo, huathirika kisaikolojia, na wakati mwingine hupoteza kabisa hamasa ya kusoma.

Ni wajibu wa mzazi kuhakikisha mtoto anapata elimu bila vikwazo vinavyoweza kuepukika. Hata katika mazingira magumu, juhudi za ziada zinahitajika kwa sababu matokeo ya elimu ni ya muda mrefu kuliko matatizo ya kifedha ya muda mfupi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *