Chanzo cha picha, Getty Images
Muda wa kusoma: Dakika 5
Tanzania inakadiriwa kuwa na zaidi ya asilimia 6 ya rasilimali zote za maji barani Afrika, kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Nile Basin Initiative. Rasilimali hizi zinajumuisha Maziwa Makuu, mito mikubwa kama Rufiji, Pangani na Ruvuma, pamoja na vyanzo vikubwa vya maji chini ya ardhi.
Hata hivyo, licha ya utajiri huo, takribani Watanzania milioni 26 bado hawana uhakika wa upatikanaji wa maji safi na salama karibu na makazi yao, kulingana na takwimu za Wizara ya Maji na Shirika la Kimataifa la Kuhudunia Watoto (UNICEF).
Changamoto hii imeendelea kuwepo kwa miongo kadhaa, hali inayozua mjadala, je, tatizo ni uhaba wa maji au ni namna yanavyosimamiwa?
Lakini kwa upande mwingine, ongezeko la mahitaji ya maji kutokana na ukuaji wa idadi ya watu unaokaribia asilimia 3 kwa mwaka, ukame kutokana na mabadiliko ya tabianchi, upanuzi wa miji, na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi, linaibua hoja kuwa mifumo ya sasa huenda isiweze kukidhi mahitaji ya muda mrefu. Ndipo wazo la gridi ya maji ya taifa linapoingia mezani kama suluhisho la kimkakati.
Katika wazo hili, ukiacha ukame Serikali ya Tanzania inasisitiza kuwa, ongezeko la mahitaji ya maji katika sekta mbalimbali ikiwemo migodi, kilimo, ufugaji, uvuvi, viwanda na matumizi ya majumbani linahitaji suluhisho la kimkakati la muda mrefu. Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema mahitaji hayo hayawezi tena kushughulikiwa kwa kutegemea miradi ya eneo husika pekee.
Gridi ya maji ya taifa inavyofanya kazi
Chanzo cha picha, URT
Akifafanua dhana ya gridi ya maji ya taifa, mchambuzi wa masuala ya kijamii, Abdulkarim Atiki, aliwahi kueleza kuwa hili ni wazo jipya kwa nchi nyingi za Afrika. Anasema ni mfumo wa kukusanya maji kutoka vyanzo vikubwa na vya uhakika, kuyatibu, na kuyasambaza kwa watumiaji nchi nzima, kwa mtandao mmoja uliounganishwa, sawa na gridi ya umeme.
Kwa mujibu wa Atiki, mfumo huu unahusisha mabomba makubwa ya kitaifa yanayounganisha maziwa, mito au mabwawa makuu, pamoja na vituo vya kisasa vya kusafisha na hifadhi za maji.
Faida yake kubwa, anasema, ni uhakika wa upatikanaji wa maji safi na salama kwa maeneo ya mijini na vijijini, hata pale chanzo kimoja kinapokumbwa na ukame au hitilafu.
Mtazamo huu unaungwa mkono na tafiti za UNESCO na Global Water Partnership, ambazo zinaonesha kuwa nchi zenye mifumo iliyounganishwa kitaifa huweza kudhibiti vyema tofauti za kijiografia za upatikanaji wa maji na kupunguza hatari ya kukatika kwa huduma.
Suluhisho la kudumu au tatizo la usimamizi?
Chanzo cha picha, URT
Hoja kuu katika mjadala wa gridi ya maji ya taifa ni iwapo mfumo huo unaweza kuwa suluhisho la kudumu kwa changamoto ya maji Tanzania, au kama tatizo halisi lipo kwenye usimamizi wa miradi iliyopo. Baadhi ya wadau wanaonya kuwa bila kurekebisha mifumo ya usimamizi, hata gridi ya maji ya taifa inaweza kuishia kuwa mradi mwingine mkubwa usiofikia malengo yake.
Kwa mtazamo huo, Fulgence Massawe, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (THRC), aliyehojiwa na Mwananchi anaeleza kuwa Tanzania haina uhaba wa maji, bali inakabiliwa na changamoto ya usimamizi wa miradi ya maji. Anasema mijadala kuhusu gridi ya taifa inapaswa kwenda sambamba na maswali ya uwajibikaji, uendelevu na ufanisi wa matumizi ya rasilimali zilizopo, badala ya kuanzisha miundombinu mipya bila kushughulikia udhaifu wa mifumo ya sasa.
Hata hivyo, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dk. Yohana Lawi, ana mtazamo tofauti. Akizungumzia wazo la gridi ya maji ya taifa, Dk. Lawi amesema mfumo huo unaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la maji na kuwa suluhisho la muda mrefu, iwapo utaandaliwa na kusimamiwa kwa misingi ya kitaalamu na kisera. Kwa mujibu wake, kuunganisha vyanzo vikubwa vya maji kitaifa kunatoa fursa ya kudhibiti athari za ukame na ongezeko la mahitaji ya maji kwa njia endelevu.
Katika kujibu hoja kwamba gridi ya maji ya taifa ni wazo lisilowezekana, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso anasema “hii safari tumeshaianza ya gridi ya maji ya taifa, kuna baadhi ya maeneo yana maji mengi, kuna maeneo yana uhaba wa maji”, akimaanisha gridi ya taifa itaunganisha maeneno yote.
Aweso anaeleza kuwa baadhi ya miradi mikubwa tayari inaakisi utekelezaji wa dhana hiyo. Anataja ujenzi wa Bwawa la Kidunda, unaoendelea kufikia takribani asilimia 40, kama sehemu ya mkakati mpana wa gridi ya maji ya taifa. Kwa mujibu wa wizara, bwawa hilo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi takribani lita bilioni 190 za maji, likitumia Mto Rufiji kuongeza uzalishaji wa maji kwa matumizi ya binadamu na shughuli za kiuchumi.
Waziri Aweso anasisitiza kuwa mradi huo ambao ni moyo wa jiji la Dar es Salaam na mkoa wa Pwani ni wa kimkakati, akieleza kuwa zaidi ya Shilingi bilioni 335 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wake.
Hata hivyo, kwa wachambuzi wa sera za maji, maswali bado yanabaki kuhusu gharama, muda wa utekelezaji na uwezo wa nchi kusimamia mfumo mkubwa wa kitaifa kwa ufanisi. Kwa mtazamo wao, mafanikio ya gridi ya maji ya taifa hayatategemea tu ukubwa wa miundombinu itakayojengwa, bali pia mageuzi ya usimamizi, taasisi imara na uwazi katika utekelezaji wake.
Dira ya kisiasa na uzoefu wa kimataifa
Chanzo cha picha, Getty Images
Rais Samia Suluhu Hassan amezungumzia wazi mpango wa gridi ya maji ya taifa, akieleza kuwa mpango huo unalenga kutumia vyanzo vitatu vikubwa: Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa na Ziwa Victoria.
Kwa mujibu wa Rais, maji kutoka njia hizo tatu yataunganishwa na kutengeneza hifadhi kubwa ya taifa, itakayokuwa mhimili wa gridi ya maji ya Tanzania.
Kwa nchi nyingine, uzoefu unaonesha kuwa mifumo kama hiyo inawezekana, ingawa ni ya gharama kubwa na inayohitaji muda mrefu. Israel, Afrika Kusini na China zimewekeza katika gridi au miradi ya kitaifa ya kuhamisha maji ili kukabiliana na ukame na mahitaji yanayoongezeka, kwa mujibu wa taarifa za Benki ya Dunia na UNESCO.
Kwa Tanzania, swali kubwa linaendelea kubaki: je, gridi ya maji ya taifa itakuwa suluhisho la kimkakati linalounganisha rasilimali zilizopo kwa ufanisi, au itahitaji kwanza mageuzi makubwa ya usimamizi ili isiwe ndoto nyingine ya maendeleo?
Kama ilivyo kwa gridi ya umeme, jibu lake linaweza lisipatikane mara moja, bali kupitia utekelezaji wa hatua kwa hatua na mjadala mpana wa kitaifa.