
Dar es Salaam. Jaji Mkuu wa Tanzania, George Masaju, amesema hakuna sababu ya msingi ya kucheleweshwa kwa kesi katika mahakama za mwanzo, akibainisha kuwa chanzo kikuu cha hali hiyo ni uzembe.
Masaju alitoa kauli hiyo jana, Desemba 22, 2025, jijini Dodoma, wakati wa kikao chake na wasajili pamoja na manaibu wasajili wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani.
Amesema mahakama za mwanzo ndizo zinazohudumia idadi kubwa ya Watanzania, hivyo ndiko kunakoonesha picha halisi ya utoaji haki, sambamba na Mahakama ya Rufani, ikiwemo aina ya mashauri yanayosikilizwa na namna yanavyohitimishwa.
Masaju amesisitiza kuwa ucheleweshaji wa kesi haukubaliki, hasa ikizingatiwa kuwa fedha na miundombinu ya kusikiliza mashauri ipo, akieleza kuwa utaratibu huo hauwezi kuendelezwa.
“Mfano, mahakama za mwanzo sioni sababu kwa nini kesi za jinai zichelewe. Kesi za jinai tuna muongozo tangu 2020 kwamba kesi inapopelekwa siku hiyo, inaanza kusikilizwa siku hiyo hiyo. Sasa kama ni hivi, kwa nini tuchelewe hadi miezi sita? Ni uzembe,” amesema.
Masaju amesema anachokiona ni kwamba wasajili pamoja na mahakimu wafawidhi wa wilaya hawajatekeleza wajibu wao kwa ufanisi unaostahili katika kuhakikisha mahakama za mwanzo zinatekeleza majukumu yake ipasavyo.
Ameeleza kuwa kesi kukaa muda mrefu mahakamani kunasababisha wananchi kupoteza imani kwa taasisi hiyo muhimu kwa mustakabali wa taifa.
Hivyo, amewataka wasajili hao kuzingatia Katiba pamoja na masharti ya kaulimbiu yao ya “Haki sawa kwa wote”, akibainisha kuwa zipo kesi ambazo kisheria zinapaswa kumalizika ndani ya muda mfupi, lakini zimekuwa zikiendeshwa hadi miaka miwili.
Kauli kuhusu ucheleweshaji kesi, iliwahi pia kutolewa na Rais Samia Suluhu Hassan Februari mosi, 2024, wakati wa kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Sheria.
Aidha, hoja hiyo ilisisitizwa tena Julai 2024 na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mustapher Siyani, akiwa mkoani Tanga, wakati akifungua mafunzo kwa majaji wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Maagizo kwa wasajili
Jaji Masaju amewataka wasajili na manaibu wasajili kusimamia majukumu yao ipasavyo, ili kumaliza mlolongo wa kesi kukaa muda mrefu mahakamani.
“Kila rekodi inayoletwa mahakamani iwe imekamilika. Hatutaki tuwe na mashauri ambayo yanaletwa mahakamani, rekodi hazijakamilika.
“Yanakaa tu kule mahakamani, siku kesi imepangwa mtu ndio anasema sijaweka sijui kitu gani. Nyie mlikuwa wapi? Hatutaki kuifanya mahakama kuwa sehemu ya kuegesha mashauri,” amesema.
Jaji huyo amesema baadhi ya mawakili ni unscrupulous (wasio waadilifu), hawana maadili, kutokana na kwamba hupeleka rekodi ambazo hazijakamilika mahakamani, lakini wakati kesi ikiitwa kusikilizwa huomba muda wa kukamilisha.
Amesema kitendo hicho ni matumizi mabaya ya mifumo ya mahakama na ni kinyume cha kanuni ya 96.
Jaji Masaju amewataka wasajili hao kuwa makini na kuhakikisha anayepeleka rekodi yake ipo sahihi, na kama haijakamilika, aelezwe.
“Mwingine analeta rufaa yake amechelewa, na bado tunapokea, na yenyewe inaonekana shauri lipo humo ndani.
“Ushauri wangu kwa mawakili wa Serikali na wale wa kujitegemea, wasiitumie vibaya mifumo ya mahakama, wasitumie hekima ya majaji kuathiri mifumo. Nitawashauri majaji wa Mahakama ya Rufani wawe wakali katika hili,” amesema.