Leo ni Jumanne tarehe Pili Rajab 1447 Hijria sawa na tarehe 23 Disemba 2025 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1226 iliyopita, kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alizaliwa Ibn Rumi, malenga mashuhuri wa Kiarabu huko Baghdad, Iraq.

Alianza kusoma elimu ya awali kwa baba yake akiwa kijana mdogo, na baadaye akasoma kwa walimu wakubwa wa enzi zake. Alifunza pia elimu za zama zake kama vile fasihi na mashairi. Ibn Rumi alikuwa akisoma sana mashairi ya kumsifu Imam Hassan Askari, mmoja wa Ahlubaiti wa Mtume (saw) kutokana na mapenzi yake makubwa kwa watu wa familia ya Mtume wa Allah (as).

Malenga huyo alifariki dunia mwaka 283 Hijiria.

Ibn Rumi

Miaka 1007  iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Abu Raihan Biruni msomi, mnajimu na mwanahisabati mkubwa wa Kiirani huko katika mji wa Ghazne katikati mwa Afghanistan ya sasa.

Abu Raihan Biruni alikuwa hodari katika elimu za historia, jiografia na hisabati, tiba na utengenezaji wa dawa. Akiwa safarini nchini India, msomi huyo wa Kiirani alikutana na kufanya mijadala na maulama na watawala wa zama hizo. Abu Raihan alikusanya taarifa muhimu alizokuwa akizihitaji kwa ajili ya kuandika kitabu chake alichokiita ‘Tahqiq Ma Lilhind’ baada ya kujifunza lugha ya Sanskriti yaani lugha ya Kihindi ya kale. Katika kitabu hicho, Abu Raihan ameandika taarifa muhimu kuhusu sayansi, itikadi, mila na desturi za Wahindi.

Msomi huyo wa Kiirani ameandika vitabu vingine vingi kuhusu elimu ya nujumu, mantiki na falsafa.

Katika siku kama ya leo miaka 100 iliyopita mji wa Jeddah ulitekwa na Ibn Saud na kwa msingi huo utawala wa ukoo wa Hashemi ukahitimishwa katika mji huo.

Baada ya kusambaratishwa uasi wa Mawahabi katika nusu ya kwanza ya karne ya 19 kundi hilo liliendelea kuwachochea watu dhidi ya serikali ya utawala wa Othmaniya. Mwanzoni mwa karne ya 20, Abdul Aziz ibn Abdulrahman ibn Saud, kinara wa moja kati ya makabila ya Hijaz aliamua kuteka moja ya maeneo ambayo yalikuwa yakitawaliwa na Utawala wa Uthmaniya ambayo alidai yalikuwa yameghusubiwa. Kwa msingi huo mwaka 1906, baada ya kuteka eneo la Riyadh, alijitangaza kuwa mtawala wa eneo hilo. Baada ya hapo watawala wa Othmaniya walimpa eneo la Al Ahsa la mashariki mwa Hijaz na akapata tamaa ya kuendelea kuteka maeneo mengine.

Mwaka 1924, Shariff Hussein, Amiri wa Makka ambaye alikuwa kutoka ukoo wa Hashimi, alijitangaza Khalifa na hapo Abdul Aziz ibn Saud kwa kisingizo kuwa Amiri aliyekuwa amejipachika cheo asichostahiki, alianza vita dhidi yake na katika uasi wake huo alifanikiwa kupata uungaji mkono wa makabila na mashekhe wa Kiwahabi.

Hatimaye Disemba 23 mwaka 1925, ukoo wa Hashimi ulisalimu amri na 8 Januari 1926, Abdul Aziz ibn Saud alijitangaza kuwa mfalme wa eneo lote la Hijaz. Hatua hiyo ilikuwa utangulizi na kuundwa rasmi Ufalme wa Saudi Arabia mnamo September 18 mwaka 1932. 

Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita watu saba miongoni mwa viongozi mashuhuri wa Japan wakati wa Vita vya Pili vya Dunia walinyongwa, kufuatia hukumu iliyotolewa na mahakama moja ya kimataifa huko Tokyo mji mkuu wa nchi hiyo.

Mahakama hiyo ambayo iliundwa ikiwa ni katika muendelezo wa mahakama ya Nuremberg ya Ujerumani kwa ajili ya kuwahukumu watenda jinai za kivita huko Japan, iliwahukumu viongozi 25 wa Japan ambapo 15 kati yao walihukumiwa kwenda jela. 

Tarehe 23 Disemba miaka 72 iliyopita mkuu wa zamani wa shirika la kuogofya la usalama na la siri la Russia ya zamani ambaye pia alikuwa kiongozi nambari mbili wa nchi hiyo katika zama za Joseph Stalin, Lavrentiy Pavlovich Beria, alihukumiwa kifo na kunyongwa kwa tuhuma za kwenda kinyume na misingi ya sheria za Chama cha Kikomonisti sambamba na kufanya njama dhidi ya serikali.

Katika kipindi cha utawala wa Stalin, Pavlovicha Beria alitoa amri ya kuuliwa watu wengi na akafanya umwagaji damu ndani ya Chama cha Kikomonisti na katika Jeshi Jekundu la Urusi ya zamani. 

Lavrentiy Pavlovich Beria

Siku kama ya leo, tarehe 23 Disemba mwaka 2013, aliaga dunia Mrussia, Mikhail Kalashnikov ambaye ndiye aliyevumbua bunduki mashuhuri ya Kalashnikov ambayo inajulikana kama AK-47.

Alizaliwa mwaka 1919 katika familia masikini kaskazini mwa Russia, na hakufanikiwa kupata masomo ya juu na hivyo alijiunga na Jeshi la Shirikisho la Sovieti akiwa na umri mdogo. Mwaka 1941, kufuatia shambulizi la Jeshi la Shirikisho la Sovieti dhidi ya wanajeshi wa Ujerumani ya Kinazi, Klashnikov alijeruhiwa na kulazwa hospitalini.

Akiwa hospitalini alitumia muda wa kuuguza majeraha kufanya uchunguzi kuhusu sifa za kipekee za bunduki ya Kimarekani ya M1 Garand na bunduki ya StG 44 ya Ujerumani na kwa kutegemea sifa za silaha hizo mbili akaanza kuunda silaha mpya.

Uundwaji silaha hiyo  ulikamilika mwaka 1947 na kukabidhiwa rasmi Jeshi la Shirikisho la Sovieti mwaka 1951. Bunduki hiyo ilipewa jina la AK-47.   

Mwishoni mwa Umri wake, Klashnikov alikuwa amelazwa hospitalini mjini Moscow kutokana na matatizo ya moyo na Septemba 2013 alihamishwa na kupelekwa katika hospitali moja huko Izhevsk, mji mkuu wa Jamhuri ya Udmurtia katika Shirikisho la Russia na hatimaye 23 Disemba 2013, akiwa na umri wa miaka 94 aliaga dunia akiwa anapata matibabu hospitalini.   

Mikhail Kalashnikov

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *