Krismasi ni mojawapo ya sikukuu zinazoadhimishwa zaidi duniani, ikichanganya imani ya Kikristo, mila za kale na utamaduni wa kisasa. Ingawa wengi huihusisha na kuzaliwa kwa Yesu Kristo, historia yake ni ndefu na imejaa mageuzi mengi ya kijamii na kitamaduni.

Cha kushangaza, Wakristo wa mwanzo hawakuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu kila mwaka. Badala yake, walizingatia zaidi kuadhimisha ufufuo wake kupitia sikukuu ya Pasaka, ambayo ilikuwa msingi wa imani yao.

Hadithi ya kuzaliwa kwa Yesu inaonekana katika Injili mbili pekee kati ya nne za Agano Jipya—Mathayo na Luka. Ingawa zote zinakubaliana kuwa Yesu alizaliwa Bethlehemu, zinatofautiana katika maelezo mengine muhimu.

Tarehe halisi ya kuzaliwa kwa Yesu haijulikani. Hakuna kumbukumbu sahihi ya siku, mwezi wala mwaka. Ndiyo maana watafiti wa historia ya Ukristo wanakubaliana kuwa Desemba 25 haikuwa tarehe ya kihistoria, bali ya kimila.

Mji wa Vatican 2025 | Krismasi katika Vatican
Papa Leo XIV akiongoza sala ya Angelus kutoka kwenye dirisha la Ikulu ya Kitume, huku mti wa Krismasi ukionekana katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, Vatican, tarehe 14 Desemba 2025.Picha: Remo Casilli/REUTERS

Ni katika karne ya nne ndipo Wakristo walianza rasmi kuadhimisha Krismasi tarehe 25 Desemba. Kipindi hiki kilikuwa muhimu sana, hasa wakati Ukristo ulipoanza kukubalika waziwazi chini ya utawala wa Mfalme Constantine.

Asili ya Krismasi na ushawishi wa mila za kale

Baadhi ya wanahistoria wanaamini kuwa Desemba 25 ilichaguliwa ili kuendana na sherehe za kipagani za majira ya baridi, kama sikukuu ya Warumi ya Sol Invictus, iliyoadhimisha “Jua Lisiloshindwa.”

Hadi leo, si Wakristo wote wanaoadhimisha Krismasi tarehe 25 Desemba. Baadhi ya makanisa ya Orthodox ya Mashariki huadhimisha sikukuu hii Januari 7, kutokana na matumizi ya kalenda ya Julian ambayo iko nyuma kwa siku 13 ikilinganishwa na kalenda ya Gregorian.

Katika zama za Kati, Krismasi haikuwa sherehe ya utulivu kama ilivyo leo. Ilijulikana kwa shamrashamra, karamu kubwa, unywaji pombe na sherehe za mitaani.

Kwa sababu hiyo, baadhi ya madhehebu, hasa Wapuritani, walipinga Krismasi wakiona haina maadili ya Kikristo. Kwa muda mrefu, sikukuu hiyo haikuheshimiwa sana kidini.

Mageuzi makubwa yalitokea katika karne ya 19, ambapo Krismasi ilianza kuhusishwa na familia, watoto, zawadi na sherehe za nyumbani—taswira inayotambulika hadi leo.

Korea Kusini, Seoul 2025 | Gwaride la Krismasi la Furaha katika Lotte World Adventure
Krismasi ilitoka kuwa sherehe ya kidini na kuwa utamaduni wa kimataifa unaoadhimishwa na Wakristo na hata watu wasiokuwa na dini.Picha: Kwak Kyung-keun/Matrix Images/picture alliance

Kuzaliwa kwa Krismasi ya kisasa

Mizizi ya Krismasi ya kisasa inaweza kufuatiliwa hadi Ujerumani, ambako desturi ya kupamba mti wa Krismasi na kubadilishana zawadi ilianza kuenea mwishoni mwa karne ya 19.

Desturi hizi zilisambaa hadi Uingereza na Marekani, zikisaidia kufufua Krismasi kama sikukuu muhimu ya kijamii na kitamaduni.

Umaarufu wa Krismasi uliongezeka zaidi baada ya kuchapishwa kwa riwaya A Christmas Carol ya Charles Dickens mwaka 1843, iliyosisitiza huruma, ukarimu na mshikamano wa kijamii.

Nchini Marekani, maandishi ya Washington Irving pia yalichangia kuimarisha sherehe za Krismasi na kumtambulisha St. Nicholas kama sehemu ya utamaduni wa sikukuu hiyo.

Mwaka 1931, wafanyakazi waliweka mti wa kwanza wa Krismasi katika Rockefeller Center, New York, ili kuinua mori wakati wa Mdororo Mkuu wa Uchumi. Tangu hapo, tukio hilo limekuwa kivutio kikubwa cha kila mwaka.

Santa Claus na asili yake ya Kikristo

Santa Claus wa kisasa ana mizizi yake kwa St. Nicholas, askofu wa Kikristo wa karne ya nne kutoka Myra, eneo lililoko Uturuki ya leo. Alijulikana kwa ukarimu na msaada kwa maskini na watoto.

Mbali na kutoa zawadi, St. Nicholas anahusishwa na hadithi za kuokoa mabaharia, kusaidia wafungwa waliodhulumiwa na kutenda miujiza.

Ibada ya St. Nicholas ilienea Ulaya katika zama za kati, lakini ilipungua baada ya Mageuzi ya Kiprotestanti katika karne ya 16, isipokuwa Uholanzi ambako aliendelea kujulikana kama Sinterklaas.

China, Shanghai 2025 | Santa Claus katika soko la Krismasi wilayani Huangpu
Mwanaume aliyevaa mavazi ya Santa Claus akifanya ishara siku ya kwanza ya soko la Krismasi katika wilaya ya Huangpu, jijini Shanghai, tarehe 26 Novemba 2025.Picha: Hector Retamal/AFP/Getty Images

Wahamiaji wa Kiholanzi walileta desturi hiyo New York, ambako baadaye ilibadilika na kumzaa Santa Claus wa kisekula anayejulikana leo.

Si Santa pekee anayetoa zawadi duniani. Nchini Uingereza kuna Father Christmas, Ugiriki na Cyprus ni St. Basil, Italia kuna St. Lucy na Befana, huku Iceland watoto wakitembelewa na Yule Lads 13 wenye utundu.

Mila za Kikristo na utamaduni wa Krismasi

Miongoni mwa mila za kale zaidi ni kuingiza mimea ya kijani kama mivinje, holly na miti ya milele majumbani. Kwa Wakristo, miti hiyo huashiria uzima wa milele na ufufuo.

Desturi ya kupamba mti wa Krismasi ilianza Ujerumani katika karne ya 16 kabla ya kuenea Ulaya na Amerika.

Mistletoe, mmea wa kijani kibichi, ulikuwa sehemu ya sherehe za kale za Druids na uliashiria uzima na matumaini wakati wa majira ya baridi kali.

Mila nyingine ni ibada za Krismasi, maonyesho ya kuzaliwa kwa Yesu (Nativity scenes) na nyimbo za Krismasi, ambazo asili yake ni matembezi ya kijamii ya Ulaya ya kuimarisha mahusiano ya kijamii.

Katika nyakati za kisasa, Nativity scenes katika maeneo ya umma, hasa Marekani, zimezua mijadala ya kisheria kuhusu utenganisho wa dini na serikali.

Mji wa Vatican | Papa Fransisko akiwa na hori ya Kuzaliwa kwa Yesu (Krismasi) katika Uwanja wa Mtakatifu Petro
Maonyesho ya kuzaliwa kwa Yesu ni mila nyingine muhimu katika maadhimisho ya Sikukuu ya KrismasiPicha: Andreas Solaro/AFP/Getty Images

Krismasi ya Kipekee ya KFC nchini Japan

Miongoni mwa mila za kisasa na za kipekee zaidi ni desturi ya kula Kentucky Fried Chicken (KFC) wakati wa Krismasi nchini Japan.

Mila hii ilianza mwaka 1974 baada ya KFC kuanzisha kampeni ya kuuza kuku wa kukaanga na mvinyo kama chakula cha sherehe ya Krismasi.

Inasemekana wazo hilo lilitokana na mteja wa kigeni aliyelalamika kukosa bata mzinga nchini Japan, hivyo kulazimika kusherehekea kwa KFC.

Hadi leo, watu nchini Japan huagiza KFC miezi kadhaa kabla ya Krismasi ili kuhakikisha wanapata chakula hicho maalum siku ya sikukuu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *