Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa sanjari na kusisitiza umuhimu wa kusitisha vita nchini Sudan, ameonya kuhusu utambulisho wake tata na athari zake zinazopanuka kwa nchi jirani na eneo kwa ujumla.
Mohamed Khaled al-Khiari, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na Masuala ya Kisiasa na Amani, amesema: Matukio ya nchini Sudan yanaonyesha utambulisho unaozidi kuwa tata wa mzozo huu na kuchukua wigo mpana kikanda, na ikiwa hakutachukuliwa hatua za kuupatia ufumbuzi basi kuna uwezekano hatari yake ikayakumba pia majirani wa Sudan.”
Onyo hili linakuja wakati Volker Türk, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu amekuwa akionya kwa miezi kadhaa sasa kuhusu hatari za kuongezeka kwa uhasama katika maeneo mbalimbali kama vile Kordofan na kutoa mwito wa kuchukuliwa hatua za haraka ili kuzuia kukaririwa uhalifu uliorekodiwa katika Darfur Kaskazini, hasa El-Fasher.
Mzozo wa Sudan ambao ulianza tangu Aprili 2023 umegeuka kuwa mgogoro wa umwagaji damu kati ya jeshi na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF), umechukua sura mpya. Kwa hakika, Sudan bado haijaweza kupata njia ya utulivu baada ya miongo kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, kujitenga kwa Sudan Kusini, na mizozo ya Darfur. Vita vya kuwania madaraka kati ya jeshi na wanamgambo, migogoro ya kikabila na kikaumu, na maslahi ya kiuchumi, hasa yanayohusiana na rasilimali asilia, yameandaa mazingira ya vita vya sasa.
Fauka ya hayo, kudumu kwa muda mrefu kwa mgogoro huu kunatokana na kushindwa mfululizo kwa upatanishi, uingiliaji wa kigeni, na kutoaminiana kati ya pande zinazozozana.
Ugumu na utata wa vita hivi unaonyesha kuwa mgogoro nchini Sudan ni zaidi ya mzozo wa kijeshi wa kawaida. Pande zinazohusika kila moja ina msingi wake wa kijamii na kiuchumi, na hii imemaanisha kuwa hakuna upande wowote unaotaka kujiondoa au kukubali masharti ya mazungumzo. Mapigano katika miji mikubwa kama Khartoum na Omdurman,na katika maeneo nyeti kama Kordofan na Darfur, yanaonyesha mgawanyiko mkubwa wa kijamii ambao umefanya maelewano kuwa magumu na hali hiyo imeuingiza mgogoro katika hatua ambayo haiwezi tena kuchukuliwa kama vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Lakini vita hii pia ina engo za kikanda. Sudan iko katikati mwa Afrika na ina mipaka na nchi zilizojaa migogoro. Mipaka yake mirefu isiyodhibitiwa, mtiririko wa wahamiaji, usafirishaji haramu na ushindani wa kijiografia na kisiasa vinaiweka nchi hiyo katika hatari ya mgogoro huo kuenea kwa majirani zake. Chad, Sudan Kusini, Misri na Ethiopia kila moja imeathirika na mgogoro huu kwa njia tofauti. Kulingana na ripoti za Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu milioni nne nchini Sudan wamehamishwa makwao, na mgogoro huu wa ukimbizi umeenea pia katika nchi jirani. Kuchukua wigo mpana wa mgogoro kikanda kunaweza kusababisha ongezeko la kutokuwa na utulivu katika nchi jirani. Kama onyo kutoka kwa maafisa wa Umoja wa Mataifa, akiwemo Volker Türk, linavyoashiria, ikiwa hatua za kivitendo hazitachukuliwa na nchi za kanda na mashirika ya kimataifa, vita nchini Sudan vinaweza kuwa kitovu cha mzozo wa kikanda, na kusababisha madhara kwa bara zima la Afrika.
Kwa upande mwingine, wachezaji wa kigeni pia wana nafasi na mchango mkubwa katika vita vya Sudan. Nafasi ya kijiografia ya Sudan na rasilimali zake za asili, ikiwemo dhahabu, mafuta, na njia za biashara, zimeifanya nchi hiyo kuwa kipaumbele cha mataifa ya kigeni. Ushindani wa kupata rasilimali hizi umewafanya wahusika nchini Sudan kupokea msaada kutoka kwa wachezaji wa kigeni. Hususan uingiliaji wa kigeni kutoka kwa baadhi ya nguvu za kikanda na zisizo za kikanda ambao umechangia kwa kiasi kikubwa kurefusha mgogoro huo. Uingiliaji huu haujazuia tu mchakato wa amani bali pia umeongeza utata wa mgogoro wenyewe.
Hata hivyo, engo ya kibinadamu na haki za binadamu ya vita nchini Sudan ni miongoni mwa nyanja za kutisha zaidi za mgogoro huu. Mamilioni wamehamishwa makwao, na mamia ya maelfu zaidi wako hatarini kufa njaa na kuugua magonjwa. Ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Sudan umekuwa jambo la kila siku. Kulingana na ripoti za mashirika ya kimataifa, wanawake na watoto ndio waliouathirika zaidi na mgogoro huu. Zaidi ya hayo, miji kama El-Fasher imeshuhudia kukaririwa kwa ukatili wa Darfur, uhalifu ambao jamii ya kimataifa bado haijapona majeraha yake. Hasa kwa kutiliana maanani kwamba, ripoti nyingi zimeibuka za ukatili wa kingono, mauaji ya raia na uharibifu wa miundombinu muhimu.

Vita hii pia imekuwa na madhara makubwa kiuchumi; kusambaratika kwa miundombinu, kusitishwa kwa uzalishaji na biashara, mgogoro wa chakula, wimbi la wakimbizi na uharibifu wa uchumi wa eneo hilo ni miongoni mwa madhara ya mgogoro huu. Vipengele hivi vya kibinadamu na kiuchumi ni kiungo cha mwisho katika mnyororo ulioanza na vita vya kuwania madaraka na sasa umegeuka kuwa janga kamili.
Hii leo Sudan iko katika kingo za kusambaratika kikamilifu; nchi inayozama zaidi katika kimbunga cha ghasia kila siku, na ambapo hatari ya mgogoro huu kuenea kwa majirani zake inaongezeka na kuwa mbaya zaidi. Iwapo vita hii itazidi kuwa mgogoro wa kikanda, si Sudan pekee bali Afrika yote itakabiliwa na wimbi la ukosefu wa utulivu, wimbi kubwa la wakimbizi, kuporomoka kwa uchumi, na migogoro ya umwagaji damu.
Ni dhahiri shahiri kwamba, indhari za Umoja wa Mataifa ni kengele ya hatari kwa wadau wote wa kimataifa; kwani kuupuza hali hii leo kutamaanisha moto usioweza kudhibitiwa hapo kesho.
Mintarafu hiyo, ni muhimu jamii ya kimataifa kuchukuliwa hatua za haraka na thabiti ili kuzuia mgogoro huu kusambaa zaidi.