Maelekezo ya utu ujenzi wa barabara yazingatiweMaelekezo ya utu ujenzi wa barabara yazingatiwe

WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amewataka wakandarasi kuweka kipaumbele utu na kuondoa kero kwa wananchi kila wanapopewa kazi za ujenzi akisisitiza kuwa ndiyo mwelekeo wa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza mkoani Ruvuma, Ulega alisema kila kwenye kazi ya ujenzi ni muhimu kwa mkandarasi kwanza kufanya mambo yatakayorahisisha maisha ya watu na kulinda utu wao badala ya kufikiria tu kumaliza ujenzi wa barabara.

Maelekezo ya Waziri Ulega ni ya msingi na muafaka, yanayopaswa kuungwa mkono kikamilifu na wadau wote wa sekta ya ujenzi.

Kauli yake kwamba ‘barabara ni utu’ inaweka wazi mwelekeo unaomtanguliza mwananchi mbele ya mradi.

Haya ni maelekezo ambayo yamezingatia hali halisi ambayo wananchi wamekuwa wakikumbwa na vitendo visivyozingatia utu wakati wa utekelezaji wa miradi ya barabara.

Baadhi ya wakandarasi wamekuwa wakifanya ujenzi kwa mtazamo wa kukamilisha kazi kwa mujibu wa mkataba, bila kuzingatia athari kwa maisha ya kila siku ya wananchi.

Matokeo yake, kumekuwapo usumbufu mkubwa, ajali zisizo za lazima, hasara za kiuchumi na hata kupotea kwa maisha hasa ujenzi unapofanyika bila kuzingatia usalama.

Ni jambo la kawaida kushuhudia mashimo yaliyoachwa wazi barabarani bila alama za tahadhari, taa wala uzio, hali inayowaweka hatarini watumiaji wa barabara hususani usiku.

Vitendo hivi si tu uzembe, bali vinaashiria kupuuzwa kwa thamani ya uhai wa binadamu.

Aidha, kumekuwapo tabia ya wakandarasi kuzuia magari kupita kwenye barabara zilizokwishakamilika au sehemu zake, hata katika nyakati za dharura.

Hali hii imekuwa ikionekana zaidi katika miji mikubwa kama Dar es Salaam ambako foleni ni sehemu ya maisha ya kila siku.

Kufunga barabara bila mpango mbadala au bila kuzingatia nyakati nyeti kama asubuhi na jioni ni kinyume cha utu na maslahi ya wananchi.

Hata kama muda wa kukabidhi barabara haujatimia, inapotokea dharura, mkandarasi na wadau wengine wa usafirishaji barabarani wanaojali utu, wataelekeza zitumike kwa dharura.

Tunampongeza waziri kwa kusisitiza kuwa mkandarasi anapaswa kwanza kufikiria namna ya kurahisisha maisha ya watu kabla ya kuendelea na ujenzi.

Ametaja mambo kadhaa kama vile kuweka kalvati mapema ili kuzuia maji kuingia kwenye makazi ya watu, kuwasha taa za barabarani pale miundombinu inapokamilika na kufungua sehemu zinazoweza kupitisha magari ili kupunguza foleni ni mifano ya vitendo vinavyoakisi ujenzi wenye utu.

Kwa maelekezo haya, yameendelea kudhihirisha dhamira ya serikali kwamba si kujenga barabara tu za kiwango cha lami, bali kujenga kwa kuzingatia maslahi ya wananchi wanaozunguka miradi hiyo. Huu ni ujumbe mzito kwa wakandarasi wote nchini.

Ni wakati sasa kwa wakandarasi kuzingatia kwamba serikali imetoa mwelekeo na wao wanapaswa kutekeleza kwa vitendo na kudhihirisha uwajibikaji na utu katika ujenzi wa taifa chini ya Falsafa ya Rais Samia ya ‘Kazi na Utu, Tunasonga Mbele’.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *